30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau wachangia milioni 150/- kukabili corona

Na MWANDISHI WETU-DODOMA

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amepokea msaada wa hundi tatu zenye thamani ya Sh milioni 150 zilizotolewa na kampuni tatu zinazozalisha nguzo za umeme nchini kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (Covid- 19).

Amepokea michango hiyo kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana katika Ofisi ya Waziri Mkuu Mlimwa, Dodoma.

Michango hiyo imetolewa na Kampuni ya Mufindi Woodpoles Plant and Timber Ltd, Qwihaya General Enterprises Co Ltd na Poles (T) Ltd ambazo kila moja imetoa Sh milioni 50.

Akizungumza wakati wa kupokea michango hiyo, Jenista aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa Covid-19.

“Nawashukuru sana kwa niaba ya Serikali na hii inaonyesha uzalendo, utayari na kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa ni sehemu ya mapambano hayo kwa vitendo,” alisema Jenista.

Aidha Jenista alitumia fursa hiyo kuwasihi wakandarasi wengine pamoja na Watanzania kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha katika kukabiliana na janga hilo.

“Tunatoa wito kwa Watanzania wote kuona umuhimu na kuguswa na janga hili kwa kuchangia kwa kadiri inavyofaa ili kuendeleza uzalendo kwa hali ya kujali na kuonyesha utayari ili kudumisha hali ya utamaduni uliopo tangu awali wa umoja na mshikamano,” alisema Jenista. 

Aliwahakikishia wadau hao kuwa michango hiyo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaeleza kuwa imefika katika eneo salama.

Awali, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa michango waliyoitoa kwa Serikali ambayo inakwenda kuongeza nguvu katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

“Niwapongeze wakandarasi hawa kwa kuonyesha nia ya kushiriki katika mapambano haya… ni faraja kubwa mnayoitoa kwa Serikalini katika kuhudumia na kusaidia katika kipindi hiki. Pia nawaomba wakandarasi wengine waige, ” alisema Dk. Kalemani.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles