20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Makonda atangaza vita na wapandisha bei sukari

Na BRIGHITER MASAKI-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza vita na wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ghali tofauti na bei elekezi ya Serikali.

Alisema ifikapo leo kikosi kazi kitafanya ukaguzi na watakaobainika kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu watakamatwa na sukari kutaifishwa na Serikali.

Akizungumza jana wakati wa ziara Wilaya ya Kigamboni wakati wa ukaguzi wa uhakiki wa taarifa za wananchi katika daftari la kudumu la mpigakura, ikiwa jana ndiyo ilikuwa siku ya mwisho, alisema kuwa hakuna sababu ya kutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kupandisha bei ya sukari ambapo bei elekezi ya Serikali ni Sh 2,600 kwa kilo moja, lakini watu wanauza hadi Sh 3,500 kwa kilo.

“Kuanzia kesho (leo) tunakamata wafanyabiashara wote wanaouza sukari kwa bei ya juu tofauti na iliyotolewa na Serikali,” alisema Makonda. 

Pia aliwataka wakuu wote wa wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha msako huo unaanza leo na asisalie mfanyabiashara yeyote anayeuza sukari hiyo kwa bei ya juu.

“Nimebaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya hadi Sh 4,500 kinyume na bei elekezi ya Serikali ya Sh 2,600 jambo linalopelekea maumivu na gharama kwa wananchi,” alisema Makonda. 

Pia aliiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mbunge akiingia bungeni kupitia Viti Maalumu anatakiwa kutafuta jimbo la kugombea na sio kurudi tena bungeni kupitia Viti Maalumu kwa kuwa wanawanyima nafasi wanawake wengine wanaotakiwa kupata uzoefu.

“Nichukue nafasi hii kuwaomba Tume ya Uchaguzi, ni mawazo tu yangu kama mwananchi, na Mtanzania nikitumia uhuru wangu wa Katiba kujieleza.

“Kuanzisha mfumo wa viti maalumu ikiwa na lengo la kuwajengea kwa kuwawezesha wakinamama wapate nafasi kuingia bungeni kupata uwezo na uzoefu wa kugombea katika majimbo.

“Swala la mtu ameshakuwa bungeni na alishapata uzoefu, na alikuwa mbunge wa jimbo awamu ya kwanza na ya pili, hatakiwi kupewa nafasi kuingia tena bungeni kupitia viti maalumu, anawanyima nafasi wengine kujipatia uzoefu.  Tunahitaji kuwapa nafasi wakinamama na sio kurudi kama viti maalumu bali mmiliki wa jimbo,” alisema Makonda.

Pia aliwaasa wananchi kutoitumia hotuba ya Rais Dk. John Magufuli kusambaza taarifa mbaya na za kupotosha jamii.

“Lengo la Rais kupima sampuli za wanyama na matunda  ni kukagua kipimo ambacho kinatumika kupima ugonjwa wa corona na sio wanyama na mimea imeathirika na ugonjwa huo, kuleni matunda kwani yanajenga afya ya mwili,” alisema Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles