33.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

CUF yapukutika Zanzibar

Viongozi wake wa wilaya 11, majimbo 54, Kata 101 wahamia ACT-Wazalendo

Na Fredy Azzah-Pemba

SIKU sita tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharf Hamad, kuhamia ACT Wazalendo, chama hicho ambacho ngome yake ilikuwa Zanzibar kimepukutika baada ya viongozi wake kuanzia ngazi ya matawi hadi juu visiwani humo kukihama.

Akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa ACT katika eneo la Ngezi Chambani katika Wilaya ya Mkoani iliyopo Kusini Pemba, Maalim Seif, alisema mara baada ya kutangaza kuhama CUF aliyoijenga kwa zaidi ya miaka 30 visiwani humo, Pemba yote ilibadilika kutoka nyekundu na nyeupe, kuwa ya zambarau.

“Kuanzia Machi 18, Pemba yote ni ngome ya ACT Wazalendo, wapo wachache walikwenda hadi mkutano wao mkuu (wa CUF), wakajipanga wakirudi wafanye sherehe lakini ngoma zao zililowa, mimi niliyefukuzwa nina furaha, wao walionifukuza wanalia, walifikiri watanimaliza, mimi Maalim Seif?

“Walidhani baada ya kutangazwa Lipumba (Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa Mwenyekiti halali wa CUF), mngeingia barabarani ili wawadhuru, bado hawajui kuwa hamchokozeki. Baada ya kusema tu tunashusha tanga, tunapandisha tanga, Pemba ilibadilika hapohapo,” alisema Maalim Seif.

Akizungumza katika mkutano huo, Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe, alisema baada ya Maalim Seif kuhamia ACT, sasa Zanzibar na hususani Pemba ni ngome ya chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2014.

Alisema kwa taarifa alizopewa na wanachama wake wapya ambao awali walikuwa viongozi wa CUF visiwani humo, Unguja na Pemba CUF kwa sensa ya chama ya 2017, kulikuwa na wanachama 125,000 ambao sasa wapo tayari kubadilisha kadi zao na kuchukua za ACT.

Alisema Pemba ilikuwa na wanachama 84,000 huku Unguja wakiwa 41,000.

Alisema wengine waliohama ni viongozi wa CUF wa wilaya zote 11, viongozi wa majimbo yote 54 na wale wa kata 101.

Pia alisema viongozi wa matawi ya CUF 675, wameshusha bendera za chama hicho na kupandisha za ACT huku kwingine wakisubiri bendera hizo ili waziweke katika matawi yao.

“Mbali na hawa waliojitokeza ili wabadilishiwe kadi, wapo pia wapya 20,000, tunaanza kazi ya kuwaandikisha sasa hadi Aprili, tunashusha tanga, tunapandisha tanga, tuendelee na safari, kilichofanyika ni kwamba tunahama kwenye jahazi la zamani tuende na jahazi jipya hadi tumalize safari,” alisema Zitto.

Awali Maalim Seif aliwaeleza wananchi hao kuwa, dhamira yake ya kufanya visiwa hivyo kuwa kama Singapore bado ipo palepale.

Katika kampeni za mwaka 2015, moja ya ahadi zake ni kuigeuza visiwa vya Zanzibar kuwa na maendeleo kama ilivyo Singapore.

Alisema kwa sasa dhamira hiyo ina nguvu zaidi kwa kuwa wapo katika jahazi lenye nahodha madhubuti ambaye hayumbi na yupo makini.

“Hapa hakuna kusikitika, ni safari tu,” alisema.

Hata hivyo, aliwatahadharisha wafuasi wake kwa kuwaeleza kuwa kuna mkakati wa kuwachokoza ili fujo ianze na kuwasihi wakati wote wawe wapole.

Baba Mzazi Makamu wa

Lipumba aenda ACT

 Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baba mzazi wa Makamu Mwenyekiti wa CUF, Abassi Juma Muhunzi, mzee Juma Muhunzi, alijitokeza kwenye mkutano huo na kuchukua kadi ya ACT huku akiwa analia.

Kitendo cha mzee huyo na sehemu ya familia yake walipojitokeza kuchukua kadi, kiliamsha shangwe kwenye ukumbi huo.

Wabunge 22 CUF matatani

Katika hatua nyingine, wabunge 22 wa CUF kutoka Zanzibar, wako katika wakati mgumu baada ya viongozi wa majimbo yao yote kuhamia ACT.

Hali hiyo inatokana pia na CUF kutaka kuwatumia kuzunguka Zanzibar kutangaza viongozi wapya huku wapiga kura wao wakiwa ACT-Wazalendo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles