KHAMIS SHARIF, ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amempongeza Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma, kwa kuamua kutenga maeneo huru ya uwekezaji ambayo yamechochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi.
Pamoja na hilo amesema hatua hiyo imesaidia kukua kwa maendeleo ya jamii na ujenzi wa miundombinu jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na kila mwananchi wa Zanzibar.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini hapa alipotembelea eneo la uwekezaji unaofanywa na Kampuni ya Union Property ambayo imejenga Shule ya Sekondari ya Kombeni mjini Unguja.
“Wananchi wanapaswa kujua kuwa Zanzibar inakuwa na kuendelea kukuza ujuzi na taaluma ili kuzalisha wataalamu wazalendo kwa lengo la kusaidia jamii,” alisema Dk. Shein.
Alisema hatua ya kampuni hiyo kujenga shule hiyo ni kuthamini kwa vitendo umuhimu wa elimu katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwapuuza watu wenye kutoa kauli za kubeza maendeleo na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar zinazolenga kuwachonganisha na kuwakatisha tamaa na kufikia malengo ya maendeleo.
“Watu wanaopita kutoa kauli kuhusu maendeleo na muungano wetu, wapuuzeni kwani inawezekana wamechanganyikiwa kwani kila mmoja ulimwenguni anaona hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa,” alisema.
Alisema Zanzibar itatumia dola milioni 28 kwa ajili ya mradi wa mji salama.
Awali akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu ujenzi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk. Idrisa Muslih Hija, alisema jengo hilo lina madarasa 19, maabara mbili ambapo yatatumika kama shule ya maandalizi, msingi na sekondari.