Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar zitaendelea kuimarisha uhusiano wa undugu na hisitoria baina yake na Burundi pamoja na kuhakikisha amani ya Burundi inadumu.
Dk. Shein aliyasema hayo jana, Ikulu mjini Zanzibar alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Burundi nchini, Gervais Abayeho, ambaye alifika Ikulu kujitambulisha.
Dk. Shein alisema SMZ imejizatiti kushirikiana na Burundi kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo na kuimarisha amani na utulivu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema juhudi zilizochukuliwa na viongozi wa pande hizo mbili hizo katika kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza likiwamo suala la amani nchini Burundi ambako Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa alikuwa msuluhishi kwa usimamizi wa Rais Yoweri Museven kwa kushirikiana na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza.
Rais Shein alipongeza amani na utulivu uliopo Burundi pamoja na kueleza juhudi za muda mrefu zilizochukuliwa na viongozi wa Tanzania kuhakikisha Burundi inakuwa salama.
Alitumia fursa hiyo kupongeza hatua zilizochukuliwa kuipata Katiba mpya ya nchi hiyo.
“Burundi na Zanzibar zilikuwa ni nchi zenye ushirikiano mzuri siku zilizopita, vikundi mbali mbali vya taarabu kutoka Zanzibar vilikuwa vikienda kutumbuiza nchi humo katika hafla mbalimbali na vile vya Burundi vilikuja Zanzibar hivyo ni vema uhusiano huo urejeshwe,” alisema Dk. Shein.
Alieleza juhudi ya SMZ kuimarisha sekta ya utalii na kueleza haja ya kuwapo ushirikiano katika kuimarisha sekta hiyo.
Dk Shein alieleza azma ya SMZ ya kuimarisha sekta ya uvuvi ambayo inaweza kuimarisha sekta ya biashara ya samaki kati ya Zanzibar na Burundi.
Naye Balozi Abayeho, alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Burundi katika kuhakikisha iko salama na wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu mkubwa.
Alisifu uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na wananchi wa Tanzania ikiwamo Zanzibar na nchi ya Burundi.
Balozi Abayeho aliipongeza Tanzania kwa kuwapatia uraia wakimbizi wenye asili ya Burundi zaidi ya 200,000 ambao waliishi kwa muda mrefu nchini.