31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

DK. SHEIN, BALOZI WA BURUNDI WATETA

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR


RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwamo Zanzibar zitaendelea kuimarisha uhusiano wa undugu na  hisitoria   baina yake na Burundi   pamoja na kuhakikisha amani ya Burundi inadumu.

Dk. Shein aliyasema hayo jana, Ikulu mjini Zanzibar  alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Burundi  nchini,  Gervais Abayeho, ambaye alifika Ikulu   kujitambulisha.

Dk. Shein alisema SMZ imejizatiti kushirikiana na Burundi kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo   na kuimarisha amani na utulivu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema juhudi zilizochukuliwa na viongozi wa pande hizo mbili hizo katika kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza likiwamo suala  la amani nchini Burundi ambako Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa alikuwa msuluhishi kwa usimamizi wa Rais Yoweri Museven kwa kushirikiana na Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza.

Rais Shein  alipongeza amani na utulivu uliopo Burundi pamoja na kueleza juhudi za muda mrefu zilizochukuliwa na viongozi wa Tanzania   kuhakikisha Burundi inakuwa salama.

Alitumia fursa hiyo kupongeza hatua zilizochukuliwa kuipata Katiba mpya ya nchi hiyo.

“Burundi na  Zanzibar zilikuwa ni nchi zenye ushirikiano mzuri   siku zilizopita, vikundi mbali mbali vya taarabu kutoka Zanzibar vilikuwa vikienda kutumbuiza nchi humo katika hafla mbalimbali na vile vya Burundi vilikuja Zanzibar hivyo ni vema uhusiano huo urejeshwe,” alisema Dk. Shein.

Alieleza juhudi ya SMZ kuimarisha sekta ya utalii na kueleza haja ya kuwapo ushirikiano katika kuimarisha sekta hiyo.

Dk Shein alieleza azma ya SMZ ya kuimarisha sekta ya uvuvi ambayo inaweza kuimarisha sekta ya biashara ya samaki kati ya Zanzibar na Burundi.

Naye Balozi   Abayeho, alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Burundi katika kuhakikisha iko salama na wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu mkubwa.

Alisifu uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na wananchi wa Tanzania ikiwamo Zanzibar na nchi ya Burundi.

Balozi Abayeho aliipongeza Tanzania kwa kuwapatia uraia wakimbizi wenye asili ya Burundi zaidi ya 200,000 ambao waliishi kwa muda mrefu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles