Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametoa rai kwa wadau wa nyumba kulipa kodi halali katika uendeshaji wa shughuli zao ili kwenda sawa na kasi ya ukuaji uchumi kupitia mapato ya ndani.
Kauli hiyo aliitoa mwishoni mwa wiki katika maonyesho ya milki kuu, nyumba na nyezo yaliyofanyika katika viwanja vya Bunge jijini hapa.
Maonyesho hayo yaliandaliwa na kampuni ya Terranova ya Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali walijitokeza kuonyesha bidhaa mbalimbali katika sekta hiyo wakiwamo Nabaki Afrika, Fumba Developments, Ngorongoro Conservativation, Alrais Developers na Taasisi ya Mwanamke Ardhi.
Waziri Lukuvi alisema wadau wa nyumba wanatakiwa kulipa kodi halali katika uendeshaji wa shughuli zao kwenda sawa na kasi ya ukuaji uchumi kupitia mapato ya ndani.
“Rai yangu kwa wadau wa nyumba ni kulipa kodi halali katika uendeshaji wa shughuli zao kwenda sawa na kasi ya ukuaji uchumi kupitia mapato ya ndani,” alisema.
Aliupongeza uongozi wa kampuni ya hiyo ya wazalendo inayoongozwa na vijana waliopata elimu katika vyuo vikuu vya nchini, kwa kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwamo ya ardhi.
“Pamoja na ubunifu huo wa waandaji uliolenga kuwafikia watanzania wote kwa wakati mfupi kupitia wawakilishi wao, hatua hiyo itasaidia kufikisha elimu kuhusiana na sekta nzima ya ardhi na kuiletea Tanzania mendeleo makubwa kutokana na rasilimali hii,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Terranova, Emil Sylvester, alisema wataendelea kuhamasisha wawekezaji wafike Dodoma kwa ajili ya kuwekeza.
“Sisi tumeanza na tutazidi kuhamasisha wawekezaji wafike Dodoma , ili azma kuu ya serikali ya kuhamia makao makuu ya nchi izidi kupata tija kwa maendeleo yetu,” alisema.