Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Tarime Vijijini, (Chadema) John Heche anadaiwa kushikiliwa na Jeshi la Polisi Tarime kwa madai ya kutoa kauli bungeni ya kuhamasisha wananchi kuzuia shughuli za Kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia, Nyamongo North Mara.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari Chadema, Tumaini Makene ilieleza kuwa, Heche alikamatwa jana huku Mbunge wa Tarime Mjini kupitia chama hicho, Esther Matiko akisakwa na jeshi hilo.
“Jeshi hilo linadai Heche kupitia mkutano wa hadhara alisema atapeleka hoja bungeni ili bangi ihalalishwe kuuzwa nje ya nchi, polisi wanasema kauli hiyo inachochea ulimaji bangi,” alisema Makene.
Makene alisema Matiko anasakwa ili kuunganishwa katika madai hayo kuwa alitoa kauli katika mkutano huo zinazochochea kilimo cha bangi.
Alisema jeshi hilo linashikilia simu za Heche na kwamba limeagiza simu nyingine iliyopo Dar es Salaam kwenye matengenezo ipelekwe mkoani humo.