26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MBARONI KWA KUANZISHA KIWANDA BUBU CHA VIROBA

Na JUDITH NYANGE-MWANZA

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Deus Chacha (20), mkazi wa Mtaa wa Nyanza, Kata ya Mkolani, wilayani Nyamagana, kwa tuhuma za kuanzisha kiwanda bubu cha viroba.

Kiwanda hicho kinadaiwa kujihusisha na kubadili  vifungashio vya pombe zilizohifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama viroba aina Pama Dry Gin na kuzihifadhi kwenye chupa za plastiki zenye ujazo wa mililita 100 na 200 kisha kubandika stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Agosti 1, mwaka huu, saa 10:30 jioni katika Mtaa wa Nyanza, Kata ya Mkolani, akiwa na boksi 33 za chupa za plastiki ambazo huzitumia kufungasha upya pombe hizo aina ya viroba ambazo zilipigwa marufuku na serikali Machi, mwaka huu, pamoja na bando la  stika zenye nembo ya TRA.

 

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akikata pombe hizo na kuweka kwenye ndoo na kisha kuziweka katika chupa hizo zilizokuwa na lebo ya blue sky na baadaye kuweka  stika zenye nembo ya TRA.

 

Alisema awali polisi walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa katika  maeneo ya Nyanza yupo mfanyabiashara mwenye kiwanda bubu kinachotengeneza pombe zinazohifadhiwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama viroba vikiwa na nembo ya TRA, kisha kuwauzia  watu wa maeneo jirani.

Alisema polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TRA walifanya ufuatiliaji, msako na upelelezi wa kumtafuta mtu huyo anayedaiwa kufanya biashara hiyo haramu ya pombe za viroba na waliweza kubaini mahali anapoishi na kufanikiwa kumkamata, huku akiwa na boksi 33 za pombe za viroba.

“Kitu kilichotushangaza zaidi ni polisi kumkuta mtuhumiwa akiwa na bando la stika zenye nembo ya TRA ambazo huzibandika kwenye chupa baada ya kumaliza kufungasha upya pombe hizo ili kuwadanganya wananchi kuwa bidhaa inatambulika na mamlaka hiyo.

“Tutawashirikisha TRA katika uchunguzi ili tuweze kufahamu uhalali wa stika hizo, upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa unaendelea na pindi utakapokamilika atafikishwa mahakamani, msako dhidi ya wafanyabiashara wengine wanaoshirikiana na mtuhumiwa kwa namna moja au nyingine katika  biashara haramu ya pombe za viroba bado unaendelea,” alisema Kamanda Msangi.

 

Kamanda Msangi amewaomba wakazi wa jiji la Mwanza kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pale wanapoona au kubaini kuwapo kwa watu wanaofanya uhalifu kama huu, kwani vitendo hivi vinahatarisha afya za watumiaji, lakini pia kukosesha serikali mapato.

 

Katika tukio jingine, polisi wanawashikilia Seif waziri (37) na Daud Mwakalinga (35), wote wakazi wa mkoani Dodoma, kwa tuhuma za kupatikana na  Sh milioni 2, dola elfu 20 pamoja na silaha aina ya shotgun yenye namba 011765714 na CAR namba 00107210.

 

Kamanda Msangi alisema watuhumiwa hao walikamatwa mkoani Singida wakiwa na vitu hivyo, ambavyo walivipora mkoani Mwanza Julai 14, mwaka huu, eneo la Kiseke A, wilayani Ilemela, baada ya kuvamia Kampuni ya Weish AST Ltd, ambayo hujishughulisha na  biashara ya mabondo, ambapo walipora fedha kiasi cha Sh milioni 40, dola 190,000 pamoja na silaha aina ya shotgun.

Kamanda Msangi alisema polisi wapo katika mahojiano na watuhumiwa wote watatu na pindi uchunguzi utakapokamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani, msako wa kuwasaka wenzao wawili ambao bado hawajapatikana unaendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles