33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

SHAYIRI ZAO LA BIASHARA LENYE FURSA KUBWA

Na PATRICIA KIMELEMETA


ZAO la Shayiri ni miongoni mwa mazao machache yanayolimwa nchini Tanzania ambayo wakulima wake wanaweza kuhesabika.

Shayiri inahitaji fedha nyingi katika uwekezaji wake, jambo ambalo linachangia wakulima wachache kulima huku wengine wakijikita kwenye kilimo cha kawaida kulingana na hali halisi ya maisha.

Shayiri ni zao la nafaka, linalotokana na nyasi zikuazo kwa mwaka‘Hardeum vulgare’ shayiri hutumika hasa kulishia mifugo huku kiasi kidogo kikitumika kutengenezea vileo(Bia na vinywaji vingine) na kwenye chakula chenye nguvu.

Shayiri hutumika kwenye supu michemsho na mikate katika nchi mbalimbali kama vile uskochi na Afrika.

Kwa upande wa Tanzania, zao hilo linalimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara baada ya kampuni mbalimbali zinazotengeneza pombe kujitokeza kuwahamasisha wakulima ili waweze kulima zao hilo kwa kilimo cha mkataba.

Akizungumza na Mwandishi wa Makala haya hivi Karibuni,Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Global Agency, Fidelis Bashasha anasema kuwa, takwimu zilizotolewa mwaka 2007, kulingana na takwimu za mazao ya nafaka duniani, shayiri lilikuwa zao la nne kwa wingi wa tani milioni 136, likichukua kilomita za mraba 560,000 katika eneo la uzalishaji.

Anasema  kibaiolojia mmea wa shayiri ni miongoni mwa familia ya nyasi,hujichavusha wenyewe, wenye kromosomu 14 wakati binadamu ana kromosomu 38 kwa ulinganishi tu.

Historia

Akizungumzia kuhusu historia ya zao hilo, Kashasha anasema, Shayiri ndiyo nafaka ya kwanza kuanza kupandwa huko Mashariki Karibu wakati ambao ngano nayo ilipoanza kutumika.Upatikanaje wake ulianzia kaskazini mwa Afrika  upande wa Mashariki.

Anasema bia ya shayiri pengine ndiyo kinywaji cha kwanza kuwahi kutengenezwa na watu wa Neolithic.

“Hupenda kukua katika hali ya baridi, lakini haitishiwi sana na mazingira ya baridi,lakini baadhi ya watu katika nchi zilizoendelea, hutumia shayiri kama chakula cha wanyama na mifugo.

“Kiasi kikubwa cha shayiri hutumika kuchemsha pombe ambapo shayiri huhitaji chaguo sahihi,”anasema Bashasha.

Bashasha anasema, zao hilo linavunwa baada ya miezi mitatu, hivyo basi kama umewekeza vizuri unaweza kuvuna kila baada ya miezi mitatu.

Anasema, kinachotakiwa ni kufuata ushauri wa watalaamu wa kilimo ambao wataangalia aina ya udongo uliopo pamoja na ulimaji wake, jambo ambalo linaweza kusaidia kutopata hasara.

Anaongeza, kwa upande wa Tanzania, zao hilo hulimwa mkoani Arusha  na Kilimanjaro katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Rukwa na Mkoani Kagera katika Wilaya ya Karagwe.

Anasema, katika kipindi cha miaka mitano, aliweza kufanya utafiti kuhusiana na soko la zao hilo, aina ya udongo unaostawi pamoja na mazingira ya kilimo, jambo ambalo lilimfanya afanikiwe kulima wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

Anasema, baada ya kumaliza kazi hiyo, aliingia makubaliano na taasisi mbalimbali za fedha ili waweze kumfadhili katika kilimo hicho, jambo ambalo alifanikiwa.

Anasema, kutokana na hali hiyo, aliweza kuandaa shamba lenye hekta 8000 katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera kwa ajili ya kulima zao hilo.

 “Niliamua kutafuta wafadhili ili niweze kulima shayiri baada ya kuona kuwa, zao hilo linahitajika sana… lakini pia linalipa ikiwa utafanikiwa kuuza kwa sababu soko lake lipo wazi kabisa,”anasema Bashasha.

Anaongeza katika shamba hilo anatumia kilimo cha umwagiliaji ili kuepusha hasara ambayo alishawahi kuipata wakati analima zao hilo ambapo alikua anasubiri mvua za msimu.

Anasema, katika msimu huo aliwekeza sh bilioni 1.6 kwa ajili ya kilimo cha zao hilo lakini hakupata hata shilingi, kutokana na kutegemea mvua za msimu, hali iliyomfanya aingie kwenye kilimo cha umwagiliaji baada ya kupata ushauri kutoka kwa watalaamu wa kilimo ndani na nje ya nchi.

Anasema, katika kilimo cha mwaka huu, ametumia sh bilioni 2.6 kwa ajili ya kuandaa shamba hadi kilimo huku ikienda sambamba na kuweka mashine za kumwagilia, hivyo anaamini kuwa, fedha hiyo itarudi kutokana na aina ya uwekezaji wake.

“Nilikopa Sh bilioni 2.6 kutoka taasisi za fedha ili kulima shayiri, matarajio yangu ni kuingiza sh bilioni 8.9, ambapo faida ni Sh bilioni 6.3,”anasema.

Anasema, soko la zao hilo lipo wazi, ambapo kampuni yanayozalisha pombe yanakuja kununua zao hilo shambani.

Bashasha anasema, mpaka sasa baadhi ya  nchi za Afrika Mashariki zimeingia mkataba wa kuuzia za hilo pindi litakapovunwa, hali inayoonyesha wazi kuwa, soko lake ni kubwa ndani na nje ya nchi.

Anazitaja nchi hizo ni pamoja na Tanzania yenyewe, Rwanda, Burundi na Uganda, huku akiendelea kufanya mawasiliano na wateja kutoka nje ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuuza shayiri.

“Nawashauri wananchi wenye uwezo kuwekeza kwenye soko la shayiri linalipa… licha ya uwekezaji wake kuwa mkubwa, lakini kuna fursa ya kuongea na taasisi za kifedha ili waweze kukopa na wanapomaliza kuvuna wanarudisha fedha zao,”anasema.

Anaongeza, mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, anaendelea kulima zao hilo ili aweze kupata faida zaidi huku akiwafundisha wakulima wanaolima jirani na shamba hilo ili waweze kujifunza kutoka kwake.

“Ukiwa mkulima wa shayiri hutakiwi kuwa mchoyo wa elimu, kwa sababu huwezi kukidhi matakwa ya soko kama hujashirikisha na wengine, hivyo basi nitaendelea kutoa elimu kwenye mashamba yaliyo jirani na mimi ili na wenyewe waweze kunufaika nayo,”anasema.

Anasema mkakati uliopo ni kuhakikisha kuwa, anaingia mkataba na makampuni makubwa ndani na nje ya nchi ili aweze kuuza shayiri inayozalishwa Tanzania, jambo ambalo linaweza kukuza uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles