Na HERIETH FAUSTINE-DAR ES SALAAM
MSANII maarufu anayepamba video za wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ‘bongo fleva’ Agnes Gerald maarufu Masogange ameendelea kusota rumande huku jalada la kesi yake likiwa mikononi mwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Masogange (25), alikamatwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa tuhuma za kujihusisha na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya.
Wiki iliyopita, alitarajiwa kupandishwa kizimbani lakini ilishindikana kutokana na majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali ya vipimo vya kuonesha kama anatumia au hatumii dawa hizo kutokamilika.
Wakili wa Masogange, Nick Kitege anaendelea anaendelea kulifanyia kazi suala hilo na pindi litakapokamilika muda wowote anaweza kupelekwa mahakamani.
“Kuhusu ucheleweshwaji wa jesi hiyo ni kutokana na taratibu za kisheria, hivyo Polisi waachwe wafanye kazi yao na sisi tunaangalia hatua zinazoendelea, unajua hivi ni vyombo vya sheria na wanafanya kazi yao, wanahitaji muda kuchunguza na kutoa hoja zilizojitosheleza, bado wanahangaika kushughulikia suala hilo naamini leo tutapata jibu kamili juu hatua inayofuata,” alisema Kitege.