Na ESTHER MNYIKA
-DAR ES SALAAM
CHAMA cha NCCR –Mageuzi kimesema hakuna kiongozi yeyote mwenye mamlaka ya kuuza au kununua mali za chama bila kupata kibali kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya aliyewahi kuwa Mkuu wa Idara ya Kampeni, Faustine Sungura kuwataka Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia, Katibu Mkuu wake, Martin Danda na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Mohamed Tibanyendera kujiuzulu ndani ya siku tatu kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwamo ubadhirifu wa fedha na kutaka kukiua chama hicho.
Ofisa Habari wa chama hicho, Florian Mbeo amesema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho Ibara ya 27 na Ibara ndogo ya 7, kifungu A na B usimamizi wa mali zote za chama zinazohamishika na zisizohamishika zipo chini ya uangalizi wa Baraza la Wadhamini.
Amesema wanachama wanapaswa kufuata taratibu zilizowekwa na katiba na kanuni za chama katika kuwasilisha taarifa zao kwenye mamlaka stahiki za chama.
“Kwa hiyo Mbatia na wenzake hawana mamlaka ya kuuza mali za chama na ili waweze kuuza au kununua lazima wapate kibali kutoka RITA, na baraza ndio linalo tambulika na RITA na si viongozi, jambo ambalo halikufanyika,” amesema Mbeo
Amesema suala kama hilo lilishatolewa ufafanuzi Desemba mwaka jana, baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao kuwa baadhi ya viongozi wanabinafsisha mali hizo, ukweli ni kwamba hakuna mali yoyote ya chama iliyotwaliwa binafsi na mwenyekiti wa au kiongozi yeyote kutoka lakini pia anayo haki ya kununua, kumiliki na kutumia mali yoyote ambayo amepata kihalali kwa jitihada zake mwenyewe.