26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TRENI YA UMEME KUIPA HESHIMA TANZANIA

NA EVANS MAGEGE – Dar es Salaam

UJENZI wa reli ya kiwango cha kimataifa cha Standard Gauge, ambao unatarajiwa kuanza mwezi mmoja na nusu ujao, utaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye huduma ya usafiri wa haraka zaidi duniani.

Reli hiyo ambayo awamu yake ya kwanza itakuwa na urefu wa kilometa 300, itaiwezesha Tanzania kutumia treni ya umeme yenye kusafiri kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa.

Kukamilika kwa reli hiyo kutaifanya Tanzania kwenda sanjari na India ambayo nayo tayari ina treni yenye kusafiri kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa kutoka New Delhi hadi Agra.

Kwa bara la Afrika, Morocco tayari ina kilometa 1,300 zilizounganishwa kwa reli ya Standard Gauge, yenye uwezo wa kusafiri kwa kasi ya kilometa 200 kwa saa.

Mazingira hayo yameifanya nchi hiyo kumiliki treni ya umeme yenye kasi zaidi barani Afrika ambayo kiwango chake cha juu cha mwendokasi ni kilometa 320 kwa saa.

Pia nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Ethiopia nazo zina reli ya kiwango cha Standard Gauge yenye uwezo wa mwendokasi wa kilometa 120 kwa saa.

TRENI YA MOROCCO

Taifa la Morocco limeingiza treni ya umeme yenye kasi zaidi barani Afrika, mradi uliofadhiliwa kwa ushirikiano na nchi za Ufaransa, Saudi Arabia na Kuwait.

Treni hiyo uwezo wake wa juu wa mwendokasi ni kilometa 320 kwa saa. Pia ina uwezo wa kubeba abiria 533 ambao 121 wanakaa daraja la kwanza na 412 daraja la pili.

Taarifa iliyochapwa kwenye tovuti ya Kampuni ya Reli ya Morocco (ONCF), inatanabaisha kwamba njia kuu ya reli ni kilomita 502 ambayo inatoka Tingier hadi Marrakech.

Kwamba treni hiyo ya umeme itaanza majaribio ya safari kupitia njia kuu kutoka mji wa Tingier hadi Casablanca ambayo ina urefu wa kilometa 293.

Treni hiyo inakadiriwa kutumia saa mbili kutoka Tingier hadi Casablanca wakati treni zilizopo kwa sasa zinatumia saa tano katika safari za miji hiyo miwili.

RELI ZENYE MWENDOKASI ZAIDI

Kwa mujibu ya takwimu iliyotolewa Januari mwaka huu na Shirika la Habari la CNN la Marekani, kati ya mwaka 1969 hadi 2008, Ujerumani ilikuwa na reli ya mwendokasi wa kilometa 449 kwa saa.

Mwaka 2003 katika mji wa Shanghai, nchini China kulikuwa na reli ya mwendokasi wa kilometa 500.5 kwa saa.

Pia mwaka 2010 China ilianza kutumia reli nyingine ya mwendokasi wa kilometa 486 kwa saa.

Mwaka 1964 mtandao wa reli za mwendokasi wa Shinkansen nchini Japan unaoendeshwa na Kampuni ya Japan Railways Group, ulitengeneza reli za mwendokasi wa kilometa 442.57 kwa saa na mwaka 1992 nchini Ufaransa kulikuwa na reli yenye mwendokasi wa kilometa 379.8 kwa saa.

Takwimu hizo zinakwenda mbali zaidi na kutanabaisha mipango ya Marekani kwamba kwa sasa wanatarajia kujenga reli ya mwendokasi wa kilometa 1,126.5 kwa saa.

Serikali ya Japan nayo imekusudia kupanua mtandao wa reli zake wa Shinkansen ikitarajia kujenga reli ya mwendokasi wa kilometa 601.89 kwa saa kwenda miji ya Okayama, Hiroshima na Fukuoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles