30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

TANESCO: KUKATIKA KWA UMEME ITAKUWA HISTORIA

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kuanzia Aprili, mwaka huu kukatika kwa umeme Jiji la Dar es Salaam itabaki historia kutokana na kuendelea kuimarisha miundombinu yake.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, mara baada ya kutembelea vituo vitatu vya kusambaza umeme vilivyoko Mbagala, Kurasini na Kariakoo.

Alisema lengo la kuboreshwa kwa miundombinu hiyo ni kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata umeme wa uhakika.

“Kukamilika kwa uboreshwaji wa miundombinu mipya kutafanya maeneo mengi yakiwamo ya Mbagala na Kigamboni kuwa na umeme wa uhakika.

“Dar es Salaam imekuwa ni miongoni mwa majiji ambayo yanakua sana barani Afrika na hivyo kujikuta ukuaji huo ukileta changamoto kwa uwezo wetu wa kusambaza umeme.

“Kwani siyo rahisi sana kuangalia miundombinu ya umeme na vituo vya kusambaza umeme ukabaini kuwa vimezidiwa, lakini ukweli ni kuwa miundombinu yetu kwa sasa imezidiwa na ndiyo maana muda mwingine inatokea kukatika kwa umeme,” alisema Dk. Mwinuka.

Alisema wameamua kuboresha vituo 19 vya kusambaza umeme ili kusaidia upatikanaji wa nishati hiyo katika maeneo hayo ili kuungana na ukubwa wa umeme unaosambazwa na Tanesco katika jiji hilo, kwa kuwa maeneo mengine yapo katika msongo wa Kv 33 ambao hauna uwezo wa kupeleka umeme mwingi katika sehemu moja.

“Kukamilika kwa vituo hivi ambavyo vyote viko asilimia 85 ya kukamilika, kutawezesha upatikanaji wa umeme wa msongo wa Kv 132 utakaosaidia kusogeza umeme kwenye vituo vya Kurasini, Mbagala, Kipawa hadi Ubungo, na hivyo kuwezesha Watanzania wengi zaidi kupata umeme wa uhakika.

“Kwa sasa licha ya kuwa hali ya umeme iliyopo nchini haijatengemaa, lakini Serikali na Tanesco tunajitahidi kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika na kwa bei nafuu,” alisema Dk. Mwinuka.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Mahende Mugaya, alisema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaondoa malalamiko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakitolewa na wananchi.

 Naye, Frank Mshalo ambaye ni Mhandisi Mkuu wa miradi ya usafirishaji umeme, alisema kuwa mradi huo unaotekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro chini ya mkandarasi wa kigeni kwa kushirikiana na mafundi wa ndani utagharimu kiasi cha  Dola za Marekani milioni 80 zinazotolewa na Benki ya Dunia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles