30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

JAMMEH AKOMBA HAZINA GAMBIA

Wandishi Wetu/Mashirika


Yahya JammehRAIS wa zamani wa Gambia aliyekwenda uhamishoni  Equatorial Guinea, Yahya Jammeh, anadaiwa kuchota mamilioni ya dola katika wiki zake za mwisho madarakani, akiiacha hazina ya nchi hiyo ikiwa tupu.

Kwa mujibu wa Mia Ahmad Fatty ambaye ni mshauri maalumu wa Rais mpya wa Gambia, Adama Barrow, zaidi ya Dola za Marekani milioni 11  ( Sh bilioni 24) zinaaminika kutoweka.

Aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Senegal, Dakar, kuwa wataalamu wa masuala ya fedha wanatathmini kujua ni kiasi gani kwa sasa kimepotea.

“Kipindi cha wiki mbili, zaidi ya dalasi milioni 500 za Gambia (Dola milioni 11) zilichotwa. Tunaingia madarakani Serikali ikiwa haina kitu,” alisema.

Kwa sasa Rais Barrow amekuwa akifanya kazi na timu ya wataalamu wa masuala ya fedha na wengine kutoka Benki Kuu ya nchi hiyo, kupata kiasi halisi kilichosalia.

Taarifa zinasema magari ya kifahari na mali nyingine zilionekana zikipakiwa katika ndege ya mizigo ya Chad kwa niaba ya Rais Jammeh siku alipoondoka nchini humo.

Maelfu ya watu walikusanyika katika Ikulu ya nchi hiyo juzi jioni wakiyaangalia majeshi ya Senegal yakiingia kuweka usalama kabla ya kurejea nchini Rais mpya, Barrow.

Rais Barrow yupo  Senegal na bado haijulikani ni lini hasa atarudi Gambia na kuingia ofisini, ila alisema atarejea baada ya kuhakikishiwa usalama wake.

Wakati huo huo, viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wamekana taarifa za kukubaliana kumpa Jammeh kinga ya kutoshtakiwa wakati wa mazungumzo yao ambayo yalimshawishi kuachia ngazi na kukimbilia uhamishoni.

Jammeh ambaye anashutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ameiongoza nchi yake kwa miaka 22.

Alikataa kukubali kushindwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba, mwaka jana.

Aliondoka kwa ndege kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Banjul kuelekea Equatorial Guinea Jumamosi usiku wa manane wakati kikosi cha kanda hiyo kikiwa kinajiandaa kumwondoa kwa nguvu.

Kumalizika kwa amani kwa mkwamo huo wa siasa kutamwezesha kiongozi wa upinzani, Barrow ambaye ameapishwa kama Rais wa Gambia kwenye ubalozi wa nchi hiyo nchini Senegal Alhamisi iliyopita, kushika madaraka.

Uamuzi wa Jammeh kung’atuka ulikuwa umezusha tetesi juu ya masharti waliyokubaliana wakati wa mazungumzo yao ya siku mbili yaliyoongozwa na Rais Alha Conde wa Guinea na Mohammed Ould Abdel Aziz wa Mauritania.

Lakini Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal, Mankeur Ndiaye ameliambia Shirika la Habari la Uingereaza, Reuters kuwa viongozi wa kanda hawakwenda mbali kukubali kumpa kinga ya kutoshtakiwa licha ya juhudi za Jammeh kutaka apatiwe kinga hiyo.

Jammeh na timu yake walitaka kuidhinishwa azimio na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Mataifa (UN) na Umoja wa Afrika (AU) ambalo litampa pamoja na mambo mengine, kinga ya kutoshtakiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles