Na MAULI MUYENJWA,DAR ES SALAAM
UBAKAJI umeongezeka kwa kiasi kikubwa nchini ambako katika kipindi cha Januari hadi sasa, kesi 2,859 zimekwisha kuripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwanasheria Mtafiti wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Paul Mikongoti.
Alikuwa akitoa ripoti ya matukio ya haki za binadamu kwa nusu mwaka ambako alisema idadi hiyo ni watoto 1,491 ambao waliripotiwa kubakwa.
“Kwa upande wa watoto haki bado iko shakani kutokana na matukio mbalimbali ya unyanyasaji na taarifa zinaonyesha matukio haya ya ubakaji, ulawiti na unajisi hufanywa na watu wa karibu sana na watoto hawa,” alisema.
Alisema katika kipindi hicho idadi ya vifo vya watu kutokana na imani za ushirikina vimeongezeka ambako watu 394 waliripotiwa kuuawa ikilinganishwa na mwaka 2015 ambako vilikuwapo vifo 57.
“Kanda ya Ziwa katika mikoa ya Mwanza, Geita na Simiyu imeendelea kuwa kinara kwa mauaji hayo.
“Kuna uwezekano wa idadi hiyo kuwa ni kubwa zaidi kwa sababu matukio mengine hayajatolewa taarifa kwenye vyombo vya dola,” alisema Mikongoti.
Alisema idadi ya matukio ya mauaji ya watu kwa kujichukulia sheria mikononi imepungua ambako mwaka huu watu 135 wameripotiwa kuuawa tofauti na mwaka 2015 ambako watu 366 waliuawa.
“Katika kipindi cha nusu mwaka, jeshi la polisi linadai ni mtu mmoja ambaye alifia mikononi mwa jeshi hilo, lakini taarifa za LHRC zinaonyesha watu wawili walifia mikononi mwa vyombo vya dola, mmoja Mtwara na mwingine mkoani Shinyanga,”alisema.
LHRC ilitoa angalizo juu ya watu zaidi ya watatu ambao walifia mikononi mwa polisi. Watu hao ni wale watuhuniwa kwa mauaji msikiti wa Mwanza na kwenye mapango ya Amboni ya Tanga.
Alisema katika kipindi cha nusu mwaka uhuru wa upatikanaji wa habari umeminywa kwa kitendo cha kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, kitendo ambacho kimewanyima maelfu ya watanzania fursa ya kupata habari.
“Lakini pia kwa kipindi hicho yamekuwapo matukio ya kuhatarisha amani na usalama kama mauaji ya watu watatu katika msikiti Mwanza, watu wanane waliouawa Tanga, mauaji ya watu saba wa familia moja Sengerema Mwanza… matukio kama haya yameleta hali ya wasiwasi nchini,” alisema.
Mikongoti alisema kuwa katika kipindi cha nusu mwaka haki za siasa ziliminywa na maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, vilipigwa marufuku.
“Kama haitoshi kulikuwa na kauli mbalimbali kutoka kwa utawala wa juu wa serikali ambazo zimekuwa zinatishia uhuru wa vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa mujibu wa katiba.
“…Kama Rais Dkt John Magufuli aliposema vyama vya siasa viache kufanya siasa mpaka mwaka 2020 wakati wa uchaguzi mkuu,” alisema.