Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Kodi na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake, hadi Agosti 23 mwaka huu.
Wakili wa Serikali, Christopher Msigwa alidai mbele ya Hakimu, Huruma Shahidi, kuwa upande wa Jamhuri haujakamilisha upelelezi na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 23 mwaka huu itakapotajwa tena.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Haroun Mpande wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA, Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema , Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary , Meneja wa Oparesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan .
Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka kadhaa likiwamo la kudaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 17, 2015 walikula njama kwa kuidanganya Serikali.
Wanadaiwa kudanganya kuwa makontena 329 yaliyokuwapo katika Bandari Kavu ya Azam (AICD) yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati haikuwa kweli.
Katika kesi nyingine, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeshindwa kusikiliza rufaa ya Mkurugenzi wa Mshitaka (DPP) dhidi ya aliyekuwa Kamishna wa TRA, Harry Kitilya na wenzake, kwa vile mawakili wa washitakiwa hao kutofika mahakamani.
Katika rufaa hiyo, DPP anapinga uamuzi wa washitakiwa hao kufutiwa shtaka la nane la utakatishaji fedha uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchaulu.
Shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Jaji Edson Mkasimongwa.
Wakili wa Utetezi, Dk. Masumbuko Lamwai alidai mawakili wawili wa upande wa utetezi walishindwa kufika mahakamani hapo kutokana na udhuru.
Mawakili hao ni Alex Mgongolwa ambaye ni mgonjwa na Majula Magafu ambaye alikuwa na kesi nyingine.