MGODI wa dhahabu wa Geita (GGM) kwa kushirikiana na Tume ya Kupambana na Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), imemteua msanii wa muziki wa asili, Mrisho Mpoto kuwa Balozi wa Kampeni ya ‘Kili Challenge’ ambaye atakuwa akielimisha jamii kuhusu mapambano ya Ukimwi.
Mpoto alisema amefurahia kuaminiwa na kupata fursa ya kipekee kwa kudai kwamba wataweza kupunguza vifo vya walioathirika na ugonjwa huo kwa kushirikiana.
“Naomba nitoe wito kwa Watanzania na Waafrika wote tuendelee na mapambano dhidi ya Ukimwi, tuzungumze na tuchukue hatua ili ugonjwa huu wa Ukimwi upungue, Tanzania bila Ukimwi inawezekana kama tutakuwa mstari wa mbele kuzidi kutoa elimu na kutumia njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huu,” alisema Mpoto.
Mpoto aliendelea kufafanua kwamba lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu juu ya ugonjwa huo vijijini na mjini.
“Hakuna kisichowezekana, tuhakikishe Tanzania tunafikia idadi ya zero katika maambukizi mapya, zero ya unyanyapaa na vifo vitokanavyo na Ukimwi inawezekana,” alimaliza.