30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Busungu ‘out’ Yanga

Malimi BusunguNA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Yanga, Malimi Busungu, huenda akalazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu na kukosa baadhi ya mechi muhimu baada ya kupata majeraha ya kuchanika mbavu na kupasuka utosini.

Busungu alipata majeraha hayo juzi wakati wa mchezo wa hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola uliochezwa katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa juzi ambao Yanga ilishinda mabao 2-0, straika huyo alitolewa uwanjani kwa machela baada ya kuumia wakati akiwania mpira langoni mwa Esperanca na  kugongana na kipa wa timu hiyo, Yuri Jose Tavazes ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Geofrey Mwashiuya.

Mshambuliaji huyo ambaye juzi alianza katika kikosi cha kwanza cha Yanga, alipatiwa matibabu ya awali lakini baadaye alikimbizwa katika Hospitali ya Temeke ambako alifanyiwa vipimo vya X-Ray vilivyobainisha amepata majeraha ya ndani hivyo hatakiwi kucheza kwa muda huo.

Daktari wa Yanga, Edward Bavu, aliliambia  MTANZANIA jana kuwa Busungu alishonwa nyuzi tatu katika jeraha alilopata kichwani lakini bado anasubiri kufanyiwa vipimo zaidi baada ya siku saba ili kufahamu ataweza kupona baada ya muda gani.

“Sidhani kama anaweza kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kulingana na jeraha alilopata kwani kwenye mbavu amechanika nyama ya juu ambayo anaweza kupona ndani ya siku saba.

“Nimeongea naye akaniambia hajambo lakini haina maana kuwa anaweza kuingia uwanjani, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa madaktari waliomtibu wamemtaka awe chini ya uangalizi wao kwa muda wa wiki moja kutokana na tatizo lake,” alisema Bavu.

Bavu alisema wachezaji wanapona haraka kutokana na mazoezi wanayofanya, hivyo hawezi kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu ingawa upo uwezekano wa kukosa michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kutokana na majeraha yanayomkabili, Busungu atashindwa kuichezea Yanga katika mechi za Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City na Ndanda FC pamoja na ile ya marudiano dhidi ya Sagrada Esperanca itakayochezwa Mei 17, mwaka huu nchini Angola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles