26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Vigogo waanza maisha ya ‘kishetani’ Kisutu

MTZ jmosi new july.indd*Yumo bosi wa zamani wa TRA na Miss Tanzania wa zamani

*Mbunge Ndassa naye aunganishwa tuhuma za rushwa

 

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

KAMISHINA Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, aliyekuwa Ofisa Mwandamizi wa Benki ya Stanbic tawi la Tanzania, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa benki hiyo, Sioi Solomon, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka nane.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakikabiliwa na mashitaka hayo, yakiwamo ya kula njama, kughushi kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola milioni sita za Marekani, sawa na zaidi ya Sh bilioni 12 ambazo ni mali ya Serikali ya Tanzania.

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani hapo kutokana na tuhuma za ufisadi zilizowahi kuibuka baada ya Serikali ya Tanzania kudaiwa kupoteza zaidi ya Sh trilioni 1.3 katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2013, wakati ikiuza hati fungani zake kwa Benki ya Stanbic inayomilikiwa na Standard Group ya Afrika Kusini.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya kwa kushirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, waliwasomea washitakiwa mashitaka hayo.

Katika shitaka la kwanza, washitakiwa hao  katika tarehe tofauti kati ya Agosti, 2012 na Machi, 2013 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Shitaka la pili hadi la tano yanamkabili  Shose peke yake, aliyewahi kuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, ambapo ilidaiwa kwamba Agosti 2, 2012 akiwa katika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Dar es Salaam, kwa nia ya kudanganya alighushi  hati ya mapendekezo ya uwezeshwaji wa kifedha ya Agosti 2, 2012 kwa lengo la kuonyesha kuwa benki hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Standard ya Uingereza watatoa mkopo wa dola milioni 550 za Marekani kwa Serikali ya Tanzania kwa ada ya asilimia 2.4 ya mkopo huo  wakati akijua si kweli.

Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kwamba Agosti 13, 2012 katika ofisi za Wizara ya Fedha aliwasilisha hati hiyo.

Shose pia anadaiwa kwamba Septemba 20, 2012, akiwa katika makao makuu ya benki hiyo yaliyopo Wilaya ya Kinondoni, alighushi barua ya pendekezo la mkopo huo ya Septemba 20, 2013, akionyesha kwamba Benki ya Standard Plc kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic tawi la Tanzania wangetoa mkopo huo kwa Serikali kama benki hizo zitapewa kazi ya kutafuta mkopo huo kwa riba ya asilimia 2.4, wakati akijua si kweli.

Mshitakiwa huyo pia anadaiwa kuwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha.

Shitaka la sita linawakabili washitakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa Novemba 5, 2012, wakiwa katika makao makuu hayo kwa nia ya kudanganya walighushi mkataba wa ushirikiano wa tarehe hiyo kwamba Benki ya Stanbic Tanzania Limited imeanzisha ushirikiano na Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited kwa ajili ya kutafuta mkopo huo kwa Serikali.

Ilidaiwa kwamba Egma pia ingewezesha na kuandaa mikutano na nyaraka mbalimbali  ambazo zingetakiwa na mamlaka za Tanzania wakati wakijua si kweli.

Katika shitaka la saba, washitakiwa hao wanadaiwa kwamba katika tarehe tofauti Machi 2013, ndani ya Dar es Salaam kwa udanganyifu walijipatia dola milioni sita kutoka serikalini kwa kudanganya kwamba fedha hizo ni ada ya malipo kwa Egma na Benki ya Stanbic tawi la Tanzania kwa kuwezesha Serikali kupata mkopo wa dola milioni 600 za Marekani.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kutakatisha kiasi hicho cha fedha kwa kuzihamisha katika akaunti mbalimbali, ikiwemo zenye namba 0240026633702, 0240026633701 na 9120001251935 zinazomilikiwa na Egma katika Benki ya Stanbic tawi la Tanzania na akaunti namba 3300605539 na 3300603692 ambazo pia zinamilikiwa na Egma katika Benki ya KBC, wakati wakijua fedha hizo si za Egma bali ni zao.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, wote waliyakana na upande wa mashitaka ulidai kutokamilisha upelelezi.

Hata hivyo, kulizuka mabishano ya kisheria kuhusu dhamana ya washitakiwa hao, ambapo upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Dk. Ringo Tenga, alitaka washitakiwa hao wapate dhamana, huku upande wa mashitaka ukipinga kwa madai ya kwamba shitaka la utakatishaji fedha halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kutokana na mabishano hayo, hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8, mwaka huu, atakapotoa uamuzi. Washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi tarehe hiyo.

 

NDASSA KORTINI

 

Kabla ya kina Kitilya kufikishwa, Takukuru ilimburuta mahakamani hapo Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa (56), kwa tuhuma ya kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba.

Ndassa, aliyefikishwa kortini hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Emmilius Mchauru, anakuwa mbunge wa nne kufikishwa mahakamani hapo baada ya wenzake watatu wa CCM (Kangi Lugola wa Mwibara, Sadiq Murad wa Mvomero na Victor Mwambalaswa wa Lupa), wakiwa ni wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (LAAC) kufikishwa juzi kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta, ili wamsaidie kutoa mapendekezo mazuri ya taarifa ya hesabu za halmashauri hiyo za mwaka 2015/2016.

Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Dennis Lekayo, alimsomea Ndassa mashtaka hayo mawili ya kujihusisha na vitendo vya rushwa anayodaiwa kuyatenda Machi 13, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Lekayo alidai siku hiyo, Ndassa akiwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kushawishi kupewa Sh milioni 30 kutoka kwa Mramba, ikiwa ni ushawishi kwa wajumbe wenzake wa kamati hiyo ili kutoa mapendekezo mazuri kwa Tanesco katika ripoti yao ya hesabu kwa mwaka 2015/2016.

Pia Ndassa anadaiwa siku hiyo katika jiji hilo akiwa mbunge na mjumbe wa kamati hiyo, alijihusisha na vitendo vya rushwa kwa kushawishi kupatiwa huduma ya umeme kutoka kwa Mramba kwa kumpatia mdogo wake, Matanga Mbushi na rafiki yake, Lameck Mahewa kama faida ili awashawishi wajumbe wenzake wa kamati hiyo watoe mapendekezo mazuri katika hesabu za Tanesco za mwaka huo wa fedha.

Mshitakiwa huyo anayewakilishwa na Wakili Erasto Lugenge kwa niaba ya Wakili Aloyce Mandebebe, alikana shitaka hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.

Pia Lekayo aliomba mahakama kutoa masharti magumu ya dhamana kama itakavyoona inafaa, akihofu kuwa kutokana na nafasi ya mshitakiwa katika jamii, anaweza kuingilia uchunguzi.

Upande wa utetezi ulidai hawaoni sababu za mshitakiwa kupewa masharti magumu kwa kuwa upande wa Jamhuri haujaeleza namna anavyoweza kuingilia upelelezi.

Hakimu Mchauru alitoa masharti ya dhamana yaliyomtaka Ndassa kutia saini dhamana ya Sh milioni 10 na kuwa na mdhamini mmoja wa kuaminika

ambaye naye atatia saini kiasi hicho cha fedha.

Ndassa alitimiza masharti hayo na aliachiwa kwa dhamana hadi Aprili 18, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Ndassa akiwa anajiandaa kutoka katika viwanja vya mahakama hiyo alisema: “Hivi mbunge akiomba nguzo kwa ajili ya wapigakura wake ili Tanesco iweze kupata mapato ni kosa.”

Kitendo cha wabunge hao kufikishwa mahakamani kwa siku mbili mfululizo kimekuja baada ya gazeti hili kuripoti hivi karibuni kuwa kuna baadhi ya wabunge waliomba rushwa katika taasisi za Serikali na Machi 22, mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alifanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe wa Kamati za Bunge, kisha akawapangua wenyeviti na makamu wenyeviti watano wa kamati walizoziongoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles