27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

TAIFA NJIAPANDA

MTZ jmosi new july.indd*Wabobezi wa uchumi wasema hakuna namna

*Wasema nchi ijiandae kufunga mkanda

*Msimamo wa Uingereza kujulikana baada ya kufanya tathmini ya Escrow, Cjina kuleta matumaini?

 

NA EVANS MAGEGE

UAMUZI wa mataifa 11 yenye uanachama wa Jumuiya ya Ulaya (EU) kusitisha kuchangia Bajeti Kuu ya Tanzania, umeliacha Taifa njiapanda na kuwagawa wananchi.

Hali hiyo imekolezwa zaidi na uamuzi huo wa sasa wa mataifa hayo 11 ambao ulitanguliwa na ule wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake Changamoto za Milenia (MCC) kusitisha msaada wa zaidi ya shilingi trilioni moja zilizokuwa ziende kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kutokana na hali hiyo wabobezi wa masuala ya uchumi wanabashiri hatua hiyo huenda ikasababisha mtikisiko wa uchumi katika siku chache zijazo ambao pamoja na mambo mengine utailazimisha Serikali au Taifa kwa ujumla kufunga mkanda.

Wachumi hao wanasema endapo Serikali haitaamua kuchukua hatua ya kukabiliana na hali hiyo matokeo ya uamuzi huo yataonekana katika bajeti kuu ya mwaka 2016/17 na watakaoathirika zaidi ni Watanzania wa kawaida.

Mtaalamu wa uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, amesema uamuzi wa MCC na ule wa mataifa 11 kuondoa msaada wao kwenye Bajeti Kuu ya Serikali utaathiri kwa kiasi kikubwa mipango ya maendeleo ya nchi.

Prof. Ngowi amesema athari za kukosekana kwa misaada hiyo zinaweza zikawagusa na zisiwaumize watawala lakini zikawaumiza zaidi wananchi wa kawaida wenye uhitaji wa kujinasua kwenye umasikini na kujiendeleza kiuchumi.

Kwa mujibu wa Prof. Ngowi, ingawa fedha za msaada wa MCC zinatafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kwamba ni ndogo, lakini malengo ya ufadhili wake yangesaidia kuinua uchumi wa wananchi wengi.

“Nadhani hili jambo litaakisi ama kuonekana katika bajeti kuu ijayo, mataifa haya 11 kuondoa ufadhili wao katika Bajeti Kuu ya Serikali, itailazimu Serikali itafute fedha za kufidia pengo,” alisema Profesa Ngowi.

Alisema ili Serikali ifidie pengo hilo itahitaji mambo matatu ambayo ni kukopa, kupandisha kodi au kuongeza vyanzo vingine vya mapato.

“Maswali ya kujiuliza, kama Serikali itakopa ina maana lazima itafute fedha za kurejesha mkopo, kama Serikali itapandisha kodi ina maana itawaumiza tena wananchi wake ambao wanakabiliwa na utitiri wa kodi na kama itaongeza vyanzo vipya vya mapato, je, ina muda wa kutosha wa kupata fedha ya kuziba pengo la wafadhili katika bajeti kuu? alihoji Profesa Ngowi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kupunguza Umasikini (REPOA), Profesa Samweli Wangwe, amesema wafadhili kuondoa misaada yao katika Bajeti Kuu ya Serikali na miradi ya maendeleo ni pigo kwa uchumi wa nchi.

Alisema pamoja na pigo kutokea Serikali inabidi iweke mpango mkakati wa kukabiliana na pigo hilo kwa kupunguza matumizi yake yasiyokuwa na ulazima.

“Si vyema sana kusifu ukubwa wa kiasi walichokuwa watufadhili… Ingawa ni kweli walikuwa wanachangia fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Inabidi kufanyike utafiti wa kufahamu ni kiasi gani walifadhili nchini na kiasi gani wamekirejesha kwao kupitia taasisi na kampuni zao zinazofanya kazi hapa nchini,” alisema Profesa Wangwe.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, alisema kuondolewa kwa misaada hiyo ni mtihani mkubwa kwa Taifa.

Alisema kabla ya wahisani kuondoa misaada yao kulikuwapo dalili zilizoashiria mwenendo wa Serikali  katika kusimamia demokrasia hauwapendezi na walionya mara kwa mara lakini Serikali haikusikia.

Kibamba aliongeza kuwa kitendo cha wafadhili kuondoa misaada yao kinamaanisha kuwa miradi ya maendeleo itakwama na matokeo yake kuwaumiza wananchi.

Alisema kuondolewa kwa misaada hiyo kunaiumiza nchi hususani wananchi masikini, kwamba watawala wanaweza wasiugulie maumivu kwa sababu wao wana akiba tofauti na mwananchi wa kawaida.

“Nawashangaa wanaosema eti tutajitegemea na hatuwezi kuwapigia magoti wafadhili, kweli ni hoja lakini Tanzania imefikia kiwango hicho wanachokifikiria? Kwanza hapa si kwamba tunawapigia magoti wafadhili bali itabidi tupigiane magoti wenyewe kwa sababu tumekoseana kwa kukiuka misingi ya demokrasia, huko Zanzibar jamii imepasuka vipande viwili….Sawa wafadhili hawatakiwi kuingilia mambo ya ndani ya nchi lakini je, wataendelea kufadhili watu waliokosana kutokana na kukiukwa kwa misingi ya demokrasia?

“Hata hili la kukosa msaada wa fedha za MCC huo ni mradi mmoja tu miongoni mwa miradi mingi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani hapa nchini, tujiulize itakuwaje kama ikifunga na hiyo miradi mingine?,” alisema Kibamba.

Katika hatua nyingine gazeti hili lilimtafuta Rais wa Mahakama ya Afrika, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, ili kufahamu mtazamo kuhusiana na uamuzi huo wa baadhi ya nchi za Magharibi ambapo alikataa kuzungumza chochote kwa hofu ya kugombana na wanasiasa.

“Siwezi kuzungumza lolote kuhusu jambo hilo, niulizeni mambo ya kisheria katika Mahakama ya Afrika, lakini  hayo mambo siwezi kabisa kuyasemea, nitajikuta nagombana bure na wanasiasa,” alisema Jaji Ramadhani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, alisema jambo hilo ni kubwa na kutaka liachwe kwa Serikali yenyewe.

“Hapana haya mambo ya dunia ni makubwa na unaweza kuzungumza chochote ukajikuta unachonganisha mataifa, unajua mambo haya yana siasa nyingi nadhani ni bora tukaiachia Serikali ikatafuta ufumbuzi wa jambo hili,” alisema Butiku.

Ikumbukwe wakati wa sakata la kashfa ya Escrow, Serikali ya Uingereza ilipunguza msaada wake wa kuchangia bajeti kuu ya Serikali kwa asilimia 12.

Taarifa iliyolifikia gazeti hili kutoka katika chanzo chake cha kuaminika inadai kuwa Serikali ya Uingereza bado haijasitisha msaada wake wa kuchangia  Bajeti Kuu ya Serikali lakini itakaa wiki ijayo kutathmini uwajibikaji wa kashfa  baada ya sakata la Escrow.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kikao hicho cha tathmini ya sakata la Escrow ndicho kitakachotoa uamuzi wa Serikali ya Uingereza wa kujitoa katika kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali au la.

Mwaka jana Serikali ambayo ilikuwa ikitegemea msaada wa nchi wahisani kwa asilimia 34, Uingereza ililazimika kuchangia asilimia 8 tu kati ya 20 ilizokuwa ikichangia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles