30 waruhusiwa kutoka karantini Simiyu

0
727
Antony Mtaka

Derick Milton, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka amesema kuwa jumla ya watu 30 waliokuwa kwenye eneo la kujitenga (Karantini) baada ya kurejea nchini kutoka nje ya nchi wametoka na hawana ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Aprili 18, wakati akiongea na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Bariadi kwenye ibada ambayo iliambatana na maombi maalumu ya kuliombea taifa kuepuka na janga la corona.

Mtaka amesema watu hao ni kati ya 120 ambao walijitenga, wote wakiwa ni raia wa Tanzania na wakazi wa Simiyu ambao walifanya safari zao kwenye nchi za Kenya na Uganda.

Amesema wengine 90 ambao nao wote ni watanzania wakazi wa mkoa huo, wanaendelea kukaa karatini, hali zao zinaendelea vizuri na mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye amebainika kuwa na virusi hivyo.

“Hadi siku ya leo watu 30 wametoka Karantini kati ya 120 wote wako salama, na watu hawa walijipeleka wenyewe baada ya kutoka safari nje ya nchi,”

“Mpaka sasa Mkoa wa Simiyu hauna mtu hata mmoja ambaye ameambukizwa na virusi vya corona, ni jambo la faraja kuwa sasa Watanzania wameanza kuelewa jinsi gani ya kujikinga na ugonjwa huu,” amesema Mtaka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here