23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Utani hufichua yaliyojificha moyoni mwa mtu

CHRISTIAN BWAYA

BILA shaka umewahi kutaniwa kwa namna moja au nyingine. Kutaniwa maana yake kuambiwa maneno yenye mzaha, kejeli, masihara kwa lengo la kuchekesha. Desturi hii ya utani imekuwa sehemu ya maisha yetu kwa muda mrefu na imesaidia kujenga uhusiano wa karibu baina ya watu.

Kupitia utani, mathalani, unaweza kubaini kiwango cha ukaribu wa watu. Ikiwa ndugu, marafiki, majirani au wafanyakazi wanaweza kuambiana maneno ya mzaha na wakacheka, basi unajua wana uhusiano wa karibu baina yao.

Kuna nyakati ambazo utani huvuka mipaka ya uhusiano wa mtu mmoja mmoja  na kuhusisha jamii kubwa ya watu. Nayafahamu makabila mbalimbali yenye desturi ya kutaniana. Wanyaturu wa Singida, kwa mfano, wamekuwa wakiwatania na majirani zao Wanyiramba kuwa wanakula nyama ya punda.

Mnyaturu anapomwambia Mnyiramba maneno hayo, halengi kumuudhi, bali kumwambia kuwa yeye ni ndugu yake wa karibu wanaweza kuambiana maneno ya mzaha, wakacheka na maisha yakaendelea.

Wakati mwingine, Mnyaturu aliposafiri kwenda maeneo wanayoishi Wanyiramba, alibeba nyama akiamini ingetosha kumfanya Mnyiramba amkaribishe. Huo ulikuwa ni utani wenye lengo la kujenga ukaribu baina ya makabila hayo mawili.

Kwa upande mwingine, tunafahamu utani wakati mwingine umesababisha ugomvi na hata mifarakano baina ya watu. Tumeona uhusiano baina ya watu ukiharibika kwa sababu ya aina ya mizaha waliyofanyiana.

Chukulia mfano marafiki wanaotukanana mbele ya watu kwa maelezo kuwa wanataniana. Fikiria mtu anayemshushua mwenzake hadharani na kumwambia maneno yanayodhalilisha haiba yake lakini akicheka kumaanisha anatania. Katika mazingira kama haya, upo uwezekano wa moja wapo kutafsiri utani huo vibaya na hivyo kutibua hisia ambazo, kimsingi, hazikupaswa kuwapo.

Ningependa tuitazame desturi hii ya utani kama nyenzo ya kuwaelewa watu. Nitarejea tafsiri niliyotangulia kuianisha awali kuwa nazungumzia utani kwa mantiki ya yale maneno yanayomponyoka mtu bila kukusudia lakini kwa minajili ya kufurahisha kadamnasi au mtu.

Ninajenga hoja kwamba utani hubeba ujumbe uliojificha unaoweza kukusaidia kumwelewa mtu. Nitatumia nadharia kuwa hakuna kitu anachokifanya mwanadamu kwa bahati mbaya.

Ipo nguvu isiyoonekana, nguvu tusiyoweza kuidhibiti, nguvu ambayo endapo ikiainishwa vyema inaweza kutusaidia kuelewa kilichojificha nyuma ya hicho kinachoitwa utani. Hapa ninaanisha mambo matatu yanayobebwa na utani.

Kwanza kabisa, utani huwakilisha ushindani. Bila shaka umewahi kukutana na watu wanaochekeshwa na udhaifu wa wengine. Mtu, mathalani, akikutana na watu wake wa karibu wasio na uwezo kama yeye anawachekesha kwa kuwaambia maneno ya utani lakini yanayojenga taswira kuwa hawana hadhi kama aliyonayo yeye.

Tabia hii ya kuwatania anaowazidi inaweza kuwa na maana kuwa ndani yake anawaona baadhi ya watu kuwa hawana hadhi aliyonayo yeye. Imani hiyo inamsukuma kutumia maneno ya utani kufunua kile kilichojificha ndani yake. Inapotokea kuwa mtu huyu anakuwa na tabia ya kurudia maneno hayo hayo mara kwa mara anapokutana na watu, hiyo inaweza kuwa na maana kwamba mtu huyu ana fukuto la kushindana na watu. Ingawa anaweza asijue anachokifanya, lakini upo uwezekano kuwa nafsi yake inatamani kupata heshima.

Lakini pia, utani unaweza kuwakilisha kisasi au maumivu yaliyojificha. Umewahi kujiuliza kwanini, kuna mtu kila mara huchekesha kwa kutumia mifano inayowadhalilisha wanawake? Kwanini mtu huyu, mara kwa mara, achekeshwe na tabia fulani ya wanawake? Kuna uwezekano kuwa mtu huyu, japo huonekana kama anafurahisha baraza, amewahi kukutana na mikasa ya uhusiano yaliyomwacha na majeraha makubwa moyoni. Kwa kuwa hawezi kusema waziwazi, mtu huyu hujikuta akifurahia utani unaochafua taswira na heshima ya mwanamke.

Vile vile, utani unaweza kuwakilisha hali ya mtu kutokujiamini. Kisaikolojia, wachekeshaji wengi ni watu wasiojiamini. Ingawa hadharani wanaonekana kuwa watu mahiri kusisimua hadhara, lakini ndani yao ni watu wenye ombwe la kujiamini.

Katika kufidia ombwe hili, watu hawa hutumia vichekesho kama namna ya kutafuta kukubalika mbele ya macho ya watu. Bila shaka utakuwa unawafahamu baadhi ya watu wenye tabia ya kuweka utani hata kwa mambo ambayo yangehitaji tafakuri pana.

Mara nyingi watu wa namna hii wanaopenda utani ni wale wanaoishi na hisia za uduni ndani yao na utani ni namna ya kuwafanya watu wawasikilize.

Ninachojaribu kusema ni kwamba; utani mara nyingi hufunua yaliyoujaa moyo wa mtu. Kinachokuchekesha mara kwa mara, inawezekana kimebeba utambulisho wako. Ndio kusema, wakati mwingine kuwa makini na maneno ya utani yanayomponyoka mtu kwa njia ya utani.

Cheka lakini usiyachukulie kirahisi. Mtu anapokwambia neno linalokera lakini kwa lugha inayochekesha, usichukulie kijuu juu. Inawezekana mtu huyu, kama tulivyokwisha kueleza, anatumia utani kufunua yaliyoujaa moyo wake.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya, Simu: 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles