22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Samia: Ongezeko la watu changamoto kwa mazingira

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema taifa linakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi, hatua inayohitaji mjadala wa kitaifa wa namna ya kukabiliana nayo.

Hayo aliyasema Dar es Salaam jana katika uzinduzi wa ripoti ya kitaifa ya mazingira iliyoandaliwa na Benki ya Dunia.

Alisema suala hilo ni muhimu kupatiwa mwafaka kwa kuwa inahitajika utatuzi wa changamoto hizo ufanyike bila kuathiri ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi.

“Tanzania ni nchi iliyojaliwa rasilimali za asili ikiwemo misitu, maji, samaki, ardhi ya kutosha na wanyamapori ambazo zinatakiwa kulindwa. Ripoti hii itakuwa ishara ya kutoa wito kwetu sote kuzilinda.

“Kama mjuavyo uchumi wetu kwa kiasi kikubwa unategemea rasilimali za asili na zaidi ya nusu ya watu nchini wanaishi katika maeneo ya vijijini na wanategemea rasilimali hizi kwa chakula, nishati na makazi. Rasilimali za asili ni nguzo ya uchumi wetu na zinasaidia kuimarisha maisha ya watu wetu.

“Kwa kiasi kikubwa uchumi unategemea wanyamapori na kupitia sekta ya utalii taifa limekuwa likinufaika, hivyo ni vyema kuhakikisha vivutio vilivyopo vinatunzwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

Samia alisema matumizi ya ardhi pia yanatakiwa kufanyiwa tathmini ya kina na kuwekewa mipaka kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu kwa kuhakikisha sekta zote zinazotegemea matumizi ya ardhi zinarutubishwa bila kuathiri mazingira na uoto wa asili.

Alisema suala jingine la kuimarisha ulinzi wa mazingira ni kuhakikisha taasisi zinazosimamia masuala ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira kwa kuanzisha vituo maalumu vya ufuatiliaji ili kuziba pengo lililopo kwa sasa.

Samia alisema ripoti hiyo iliyozinduliwa jana ni muhimu kwa kuwa inaweka uwiano baina ya uchumi wa taifa na mazingira na kutoa mwelekeo namna ya kushughulikia suala hilo ili kufikia lengo la 13 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) kuhusu kuchukua hatua za dharura kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Malawi, Somalia na Burundi, Bella Bird, alisema pamoja na ukuaji mkubwa wa kiuchumi ambao Tanzania imeushuhudia, utajiri wa jumla wa pato la kila mtu, jumla ya pato halisi na la asili lilipungua kati ya mwaka 1995 na 2014.

Alisema kupungua huko kunahusishwa na kukua kwa kasi kwa idadi ya watu ambayo imeongezeka na kuathiri rasilimali za asili, hivyo kusababisha pato la kichwa kupungua kwa asilimia 35 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita na kwa rasilimali za asili zisizotegemea ardhi pato la kichwa lilipungua kwa asilimia 47.

Samia alisema Tanzania ina idadi kubwa ya watu masikini katika bara la Afrika, ikiwa na watu milioni 21.3 wanaoishi chini ya mstari wa umasikini, wengi wao wakitegemea rasilimali za asili kuendesha maisha yao, hatua inayochangia matumizi mabaya ya rasilimali hizo na hatimaye kupunguza uwezo wao wa kuendelea kuzalisha bidhaa na huduma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba, alisema iwapo watu wanaongezeka na kusababisha changamoto kwa fursa zilizopo, kama taifa hatua za kudhibiti rasilimali za asili na mazingira zinatakiwa kuchukuliwa hatua kwa hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles