25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Hakimu, wakili kizimbani kwa uhujumu uchumi

JANETH MUSHI-ARUSHA

WATU watano akiwemo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, Benard Nganga, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, wakikabiliwa na mashtaka 11 yakiwamo ya utakatishaji fedha haramu na kuongoza mtandao wa kupanga uhalifu.

Makosa mengine ni kujihusisha na rushwa kuharibu ushahidi, kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Washtakiwa wengine ni Wakili wa Serikali Fortunatus Mhalila, Wakili Maneno Mbunda, mtuhumiwa anayedaiwa kukutwa na nyara za Serikali, Nelson Kangelo na Tumaini Mdee.

Katika shauri hilo la uhujumu uchumi namba 34 la mwaka huu, upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Javelin Rugaihuruza akisaidiana na mawakili waandamizi Shedrack Kimaro na Theopil Mutakyawa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Niku Mwakatobe, Wakili Javelin alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Juni mosi mwaka jana hadi Aprili 15, mwaka huu.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili Mkuu huyo alisema shitaka la kwanza linawakabili Kangelo na Mdee ambalo ni kuongoza mtandao wa kupanga uhalifu kinyume na Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Wanadaiwa kati ya kipindi hicho katika maeneo tofauti ya Jiji la Arusha wakiwa si watumishi wa umma, walishirikiana na watumishi wa umma kwa makusudi na kwa malengo ya kuhakikisha genge la uhalifu linafanya vitendo vya rushwa ili kujipatia faida zitokanazo na vitendo hivyo.

Kosa la pili ambalo pia ni la kuongoza mtandao wa kupanga uhalifu, linawakabili Mbunda, Nganga na Mhalila, ambao wanadaiwa wakiwa watumishi wa umma walikwenda kinyume cha sheria na shughuli zao ambapo kwa pamoja na kwa makusudi kwa malengo ya kufanikisha genge la uhalifu na waliomba na kupokea rushwa ili kumwezesha Kangelo kuzuia haki kutendeka na kuendelea kujipatia manufaa faida zitokanazo na vitendo hivyo.

Alidai kosa la tatu ambalo ni kujihusisha na rushwa,  linawakabili Kangelo na Mdee, ambao kwa pamoja kwa vitendo vya rushwa walitoa Sh milioni 31.5 kwa Mbunda, Nganga na Mhlalila, kama ushawishi wa kumwezesha Kangelo kuachiliwa mwenye dhima ya jinai, hivyo kuzuia haki kutendeka.

Alidai kosa la tano ni kuharibu ushahidi ambalo linawakabili Mbunda, Nganga na Mhalila, huku wakijua jalada la kesi la mahakama linalohusiana na kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2018  la Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, litahitajika kwenye ushahidi katika mwenendo wa kesi, kwa pamoja waliteketeza/waliharibu jalada hilo kwa nia ya kuzuia kutumika katika ushahidi.

“Kosa la sita linalowakabili Mbunda, Nganga na Mhalila ni kughushi ambapo wakiwa na nia ovu walitengeneza nyaraka ya uongo (hati ya mashtaka) inayohusiana na kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2018 ikionyesha thamani ya nyaraka za Serikali iliyokuwa inahusishwa katika kesi hiyo ilikuwa ni shilingi milioni 9.8 suala ambalo siyo kweli,” alidai.

Wakili Javelin alidai kosa la saba ambalo ni kuwasilisha nyaraka za uongo linawakabili Mbunda na Mhalila ambao wanadaiwa kati ya Mei 15 mwaka jana na Juni 6 mwaka huo, wakijua na kwa uongo  kwa pamoja waliwasilisha  nyaraka ya uongo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, ambayo ilikuwa ni hati ya mashtaka ya kesi ya uhujumu uchumi namba 2/2018, kuonyesha thamani ya nyaraka ni sh milioni 9.8 wakati siyo kweli.

Alidai mahakamani hapo kosa la nane ni utakatishaji fedha haramu ambalo linawakabili Mbunda, Nganga na Mhalila ambao wanadaiwa kujipatia Sh milioni 31.5 kutoka kwa Kangelo na Mdee huku wakijua wakati wakipokea fedha hizo kwamba ni zao la kosa tangulizi ambalo ni la kujihusisha na rushwa.

Shtaka la tisa ambalo ni utakatishaji fedha haramu, linawakabili Kangelo na Mdee ambao wanadaiwa kutoa Sh milioni 31.5 kwa watuhumiwa wenzao watatu huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi (kughushi na kujihusisha na rushwa).

Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kuisikiliza ambapo imeahirishwa hadi Mei 20, mwaka huu kutokana na upelelezi wake kutokukamilika.

Wakati huohuo, Kangelo alisomewa shtaka jingine la uhujumu uchumi ambapo katika shauri hilo namba 35 la mwaka huu anadaiwa kukutwa na nyara za Serikali kinyume na sheria ya uhifadhi wa wanyamapori na sheria ya uhujumu uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles