32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wasichana wa miaka 15 hadi 24 waathirika zaidi na VVU- TACAIDS

PENDO FUNDISHA-MBEYA

WASICHANA wenye umri wa miaka 15 hadi 24 nchini, wanatajwa kuathiriwa zaidi na maambukizo mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na matatizo ya afya ya uzazi.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dr. Leonard Maboko, wakati akizungumza na vyombo vya habari Mkoa wa Mbeya na kueleza lengo la uzinduzi wa programu ya usikilizaji wa vipindi vya redio kwa vijana itakayojulikana kwa jina la ‘Ongea’.

Alisema, utafiti wa viashiria vya ukimwi wa mwaka 2016/17, unaonyesha watu 72,000 wenye umri wa miaka 15 na kuendelea hupata maambukizo mapya ya VVU kila mwaka nchini.

Alisema, changamoto kubwa ipo kwenye kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 ambao huchangia kwa asilimia 40 ya maambukizo mapya kati ya maambukizo 72,000 kitaifa kwa mwaka.

Aidha, Maboko alisema miongoni mwa kundi hilo la vijana  changamoto kubwa ipo kwa wasichana ambao huchangia asilimia 80 ya maambukizo mapya ya VVU.

“Changamoto nyingine kwa wasichana ni kuhusu afya ya uzazi kwani asilimia 27 ya wasichana wamepata ujauzito au wameshapata mtoto katika umri wa miaka 15-19 huku ndoa za utotoni asilimia 31 ya wanawake wenye umri wa miaka 20-24 waliolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18,”alisema.

Akielezea upande wa elimu, Mkurugenzi huyo alisema asilimia 80ya wasichana humaliza shule ya msingi lakini asilimia 68 hujiunga na masomo ya sekondari na kati ya hao asilimia 38.7 ndio hufanikiwa kumaliza masomo yao.

Tume ya kudhibiti Ukimwi Tanzania, imeshirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto(UNICEF) na wadau wengine, kuzindua program hiyo ili kuelimisha vijana hususani wa umri wa miaka 15-19 walio ndani na nje ya shule kuhusu kujikinga na VVU na magonjwa mengine .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles