Anna Potinus
Makamu wa rais Samia Suluhu amefanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa mazingira Mkoani Tabora, ambapo amewataka kuboresha usafi na kuacha kukata miti kutokana na matumizi ya mkaa na kuni kuchangia uharibifu wa mazingira mkoani humo kwa kiasi kikubwa.
Ameyasema hayo leo Februari 25, mwaka huu katika kongamano la kujadili mustakabali wa mazingira mkoani humo ambapo amewataka wazazi kuwafundisha watoto na vijana juu ya utunzaji wa mazingira ili waweze kusaidia kupambana na uharibifu huo.
“Fursa mliyo nayo ni wingi wa watu hapa nimeona kuna vijana na watoto wengi sana na wanakuwa hivyo tusipowafundisha jinsi ya kutunza na kuhifadhi mazingira tutaiweka nchi yetu katika hali ambayo sio nzuri, tuangalie ni kazi gani tunawapangia ili wanavyozidi kukua waweze kujua wanatunza vipi mazingira yao,” amesema.
Aidha amesema kuwa mazao yanayolimwa mkoani humo ni ya uchumi wa viwanda na uchumi huo unahitaji umeme ili viwanda viweze kufanya kazi vizuri hivyo amesisitiza utunzaji wa mazingira ili bwawa liweze kujazwa na kuwe na umeme wa kutosha.
“Makundi ya ng’ombe yakikanyaga ardhi wanaaribu mfuko wa ikolojia na kinyesi cha wanyama kinafanya ardhi inakuwa ngumu na kupasuka hivyo jaribuni kutumia utajiri huo mlio nao vizuri kwaajili ya kuleta maendeleo,” amesema.
Baada ya Samia Suluhu kuzungumza wadau mbalimbali walitoa maoni yao juu ya vyanzo vya uharibifu wa mazingira na nini kifanyike ili kuondokana na uharibifu huo.
January Makamba
Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira January Makamba amempongeza Makamu wa Rais, Samia Suluhu kwa kuongoza mazungumzo juu ya suala la mazingira kwa kusema kuwa maendeleo ya nchi na mazingira haviwezi kutenganishwa na kuwataka wakazi wa Tabora kuchukua hatua juu ya utunzaji wa mazingira ili kuepukana na madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
“Kama hatutachukua hatua mapema sifa za Mkoa wa Tabora zitabaki kuwa simulizi na jambo hili tuliloelekezwa na makamu wa rais ni la mbele la kuokoa mustakabali wa maendeleo ya mji huu kwa sasa,” amesema
Amesema kuwa duniani kuna nchi karibu 43 ambazo zina hali ngumu ya upatikanaji wa maji na mwaka juzi Tanzania iliingia katika nchi zenye hali ya hatari ya upatikanaji wa maji na kwamba jitihada zinazofanywa na viongozi mbalimbali hazitafanikiwa iwapo mazingira na mali asili hazitalindwa.
“Kama nchi yetu inategemea kilimo ufugaji na maliasili lazima tutunze na kuhifadhi mazingira yetu na kwa Mkoa wa Tabora leo Makamu wa rais ametusaidia kuonyesha njia ni kwa namna gani tutafanikiwa katika jambo hili,” amesema.
Constantine Kanyasu
Naibu Waziri Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu amesema taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa juu wa upandaji wa miti ni za uongo na kwamba katika Wilaya ambazo walizotembelea kuhakiki iwapo miti hiyo imepandwa hawakukuta kulingana na taarifa zinazotolewa.
“Vichocheo vikubwa vya uharibifu wa mazingira ni kama Kilimo kwani watu wanakata miti ili waeze kipata eneo na ulimia lakini kwa kilimo cha sasa unaweza ukalima miti ikiwepo ndani ya shamba mfano mzuri ukienda Kilimanjaro au Biharamlo wananchi wanagombania maeneo yenye miti ili waweze kufanya kilimo chao,” amesema.
Amesema kuwa Katika suala la ujenzi wamepiga marufuku kukata miti yote ya Mininga kwani sasa hivi maeneo mbalimbali watu wameacha kutumia miti badala yake wanatumia vyumba na mambo mengi hivyo ili kupunguza ukatataji miti.
“Suala lingine ni ufugaji, ninawapenda sana wafugaji lakini kama hatutakuwa na mfumo wa kupunguza mifungo kulingana na maeneo tuliyonayo tutaendelea kuwa na migogoro kila siku,” amesema.
Mwita Waitara
Naye Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara amesema viongozi wa juu wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uharibifu wa mazingira kwa kutetea vitendo vibaya vinavyofanywa na baadhi ya watu ambavyo vinapelekea kuyaweka mazingira katika hali ya hatari.
“Tunajua wazi kuwa bila miti hakuna mvua na bila mvua hakuna miti, mtendaji anaweza kuwa amemkamata mtu mwenye mifugo inayokula mazao lakini wanaowatetea ni hawa viongozi wa juu,” amesema.
Aidha ameongeza kwa kuwataka wadau kuchngamkia fursa ya uzungumza mbele ya Makamu wa rasi juu ya changamoto wanazokutana nazo kwani nafasi ya kukutana na viongozi wakubwa haiji mara mbili hivyo hawana budi kutumia muda vizuri kwa kuchangia hoja nzuri na zinazoeleweka.
Juma Aweso
Kwa upande wake Naibu Waziri wa maji Juma Aweso amesema kuwa Suala la mazingira sio la Mama Samia peke yake bali ni la watu wote ambapo amesisitiza watanzania kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa ya baadae.
“Tuamue katika utekelezaji wa kulinda vyanzo vyetu vya maji, Nchi yetu ilivyopata uhuru kila mtanzania alikwa anapata mita za ujazo 7862 laini sasa hivi wanapata mita za ujazo 1800 tu,” amesema
Aidha amesema kuwa Wizara yake imetangaza maeneo zaidi ya 84 ambayo watahakikisha vyanzo vyake vya maji haviwezi kuvamiwa kwa namna yoyote.