30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Krismasi chungu kwa vigogo 29

MWANDISHI WETU – Dar es Salaam

WAKATI keshokutwa Wakristo wote duniani wataadhimisha Sikukuu ya Krismasi na wiki ijayo Mwaka Mpya wa 2019, vigogo 29 watasherehekea wakiwa mahabusu katika magereza mbalimbali nchini.

Vigogo hao ni wale wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakituhumiwa kwa kesi mbalimbali, zikiwamo za uhujumu uchumi, biashara ya dawa za kulevya na meno ya tembo.

Miongoni mwa vigogo hao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Mbowe na Matiko watasherehekea Krismasi na Mwaka Mpya gerezani baada ya kufutiwa dhamana zao katika kesi ya uchochezi inayowakabili pamoja na wengine saba wa chama hicho.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Januari 3, mwakani ikiwajumuisha washtakiwa wengine; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu. 

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam.

Mbali na hao, vigogo wengine wanaosherehekea Krismasi mahabusu ni aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, Katibu wake, Celestine Mwesiga na Mhasibu Nsiande Mwanga.

Malinzi na wenzake wanatuhumiwa kwa makosa 28 yakiwamo matatu ya utakatishaji fedha na kughushi nyaraka walipofanya malipo. Katika tuhuma hizo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 25.

Wengine wanaosota rumande ni aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kwa jina la Kaburu.

Wawili hao wanakabiliwa na makosa ya kuhamisha kinyemela Dola za Marekani 300,000 na kutakatisha fedha.

Si hao tu, mwingine anayeendelea kusota rumande ni Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya.

Kitila yuko katika kesi moja na waliokuwa maofisa wawili waandamizi wa Benki ya Stanbic Tanzania; Sioi Solomon na Mrembo wa Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare ambao nao wanasota mahabusu.

Sioi aliwahi kugombea ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki mwaka 2012 kwa tiketi ya CCM baada ya baba yake aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari kufariki dunia.

Kitilya na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali likiwamo la utakatishaji fedha na kwa mara ya kwanza walisomewa mashtaka yao Aprili, mwaka juzi.

Mashtaka mengine wanayotuhumiwa nayo ni kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni sita sawa na Sh bilioni 12, kwamba katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013 jijini Dar es Salaam walipanga kwa ushirikiano na watu wengine kujipatia fedha kutoka serikalini kwa njia ya udanganyifu.

Ukiacha vigogo hao, wengine wanaosota rumande baada ya kufikishwa mahakamani hapo ni wafanyabiashara Harbinder Sethi na mwenzake James Rugemalira wanaodaiwa kuhusika na uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow.

Sethi akiwa ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL)/Pan Africa Power (PAP) na Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, walipandishwa kwa mara ya kwanza kizimbani Juni 19, mwaka jana na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi, kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu na kutoa nyaraka za kughushi.

Wengine wanaokula sikukuu hizo mahabusu ni Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki) maarufu kamaUamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed.

Farid alishtakiwa na wenzake saba kwa makosa ya ugaidi na wameendelea kusota rumande tangu mwaka 2012 wakitokea Zanzibar.

Pia katika orodha ya wanaokula Krismasi mahabusu ni raia wa China, Yang Feng Glan(maarufu kwa jina la Malkia wa Pembe za Ndovu), anayekabiliwa na kesi ya biashara ya pembe za ndovu ambaye yuko rumande tangu mwaka 2014.

Si hao tu, mwingine anayesota rumande ni Yusuf Ali maarufu kwa jina la Mpemba kutokana na mashtaka ya biashara ya pembe za ndovu.

Mpemba na wenzake wawili; Pius Kulagwa na Ahmed Nyagongo wanakabiliwa na mashtaka manne ya kukutwa na pembe za ndovu kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara.

Mfanyabiashara Mharami Mohamed Abdallah maarufu kwa jina la Chonji yumo katika orodha ya wanaokula Krismasi akiwa rumande.

Kwa Chonji hii ni Krismasi ya nne kwa sababu yupo mahabusu tangu mwaka 2014 baada ya kutuhumiwa kukutwa na dawa za kulevya katika makazi yake yaliyopo Dar es Salaam.

Wengine wanaokula sikukuu hizi wakiwa mahabusu ni wakurugenzi wa Kampuni ya Six Telecoms; wakili maarufu wa kujitegemea, Dk. Ringo Tenga, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), Peter Noni na Hafidhi Shamte maarufu kwa jina la Rashidi Shamte.

Mwingine ni Ofisa Mkuu wa Fedha wa kampuni hiyo, Noel Chacha ambao wote kwa pamoja wanaendelea kusota mahabusu tangu Novemba, mwaka jana kwa kukabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi, likiwamo la utakatishaji wa fedha na kuisababisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22 sawa na Sh bilioni nane.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,688FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles