23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mwanjelwa awabana waajiri, maofisa utumishi

AGATHA CHARLES – dar es salaam

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa amesema mishahara ya waajiri na maofisa utumishi watakaobainika kuwasilisha taarifa zisizo sahihi kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara Serikalini (HCMIS) itasimamishwa mara moja.

Alisema Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndiyo itahusika na zoezi hilo ili kuwakumbusha waajiri na maofisa hao kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi na kwa wakati.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais (Utumishi).

Dk. Mwanjelwa alizungumza hayo jijini Dodoma alipokutana na watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kufahamu vema majukumu ya idara hiyo.

Alisema ili kuimarisha nidhamu na utendaji kazi, watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini wasisite kusimamisha mshahara wa mwajiri au ofisa utumishi atakayebainika kuwasilisha taarifa zenye udanganyifu na kuwataka  kutozifanyia kazi na kuzirejesha mara moja kwa waajiri na maofisa hao.

Dk. Mwanjelwa alisema lawama nyingi zimekuwa zikielekezwa Ofisi ya Rais-Utumishi hata kosa linapokuwa kwa waajiri.

“Haiwezekani mtumishi wa umma kukatwa mshahara wake kwa madai ya kukopa kwenye taasisi ya kifedha wakati hajakopa,” alisema.

Dk. Mwanjelwa alisema kuna uwezekano baadhi ya waajiri na maofisa utumishi wanashiriki mchezo mchafu wa kutumia mishahara ya watumishi kujinufaisha, hivyo watakaobainika wachukuliwe hatua za kinidhamu, kisheria na kusimamishiwa mishahara yao pale inapobidi.

Alisema lengo ni kurejesha nidhamu ya kazi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Dk. Mwanjelwa pia alihoji uwepo wa maofisa utumishi wakati watumishi wa umma wakidai malimbikizo ya mishahara ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwa wingi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tena kwa kuchelewa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ibrahim Mahumi, alisema idara yake itatekeleza maagizo hayo na tayari ilianza kuchukua hatua kwa kuwasimamishia mishahara maofisa utumishi zaidi ya 56 walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

Alisema watumishi wengine zaidi ya 500 wenye dhamana ya kufanya kazi kwenye mfumo wamefikishwa kwenye vyombo vya kisheria kwa makosa mbalimbali yanayohusu kuuchezea, ikiwa ni pamoja na baadhi ya waajiri waliohusika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles