23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri agoma kufungua machinjio Dodoma

Ramadhan Hassan -Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, George Simbachawene, amegoma kuzindua machinjio ya ng’ombe na mbuzi ya Msalato jijini hapa kwa madai kwamba majengo yamejengwa chini ya kiwango.

Kutokana na hali hiyo, ametoa wiki moja kwa Jiji la Dodoma kuhakikisha sehemu ambazo hazijakamilika zinakamilika.

Oktoba 31 mwaka jana, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ilikagua machijio hayo na kutokuridhishwa na hali ya usafi ambayo ilikuwapo.

Kutokana na hali hiyo, Baraza la Taifa la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira (NEMC), liliyafungia machinjio hayo na kulitaka Jiji la Dodoma kuyakarabati, huku pia ikilipiga faini ya Sh milioni tano kutokana na eneo hilo kuwa chafu.

Akizungumza jana mara baada ya kukagua machinjio hiyo, Simbachawene alisema ni aibu kwa waliohusika kujenga jengo hilo kwani lipo chini ya kiwango, huku baadhi ya maeneo yakiwa hayajakamilika.

“Hivi nyumba zenu mnajenga hivi? Hivi nyinyi wasomi wa Tanzania hamuoni aibu? Huu ni uchafu mtupu, aliyejenga hapa kalipwa kweli! Mmemtoa wapi maana hata mafundi wa kule kwetu Kibakwe hawawezi kujenga hivi, sifungui mpaka mmalize kujenga.

“Kila kitu kipo hovyo hovyo tu, tanki lipo chini, huko nje hamjamalizia, Serikali inapenda vitu vizuri nyinyi Jiji mnapenda vitu vibaya, vigae vimevunjika vunjika, vitu ni vya kibabaishaji tu kwanini lakini mnafanya hivi?” alisema Simbachawene.

Kutokana na hali hiyo, aliondoka katika machinjio hayo huku akigoma kuyafungua hadi ukarabati umalizike na alitoa wiki moja ujenzi uweze kukamilika.

“Sifungui mpaka mmalize, nawapeni wiki moja muwe mmemaliza kila kitu, ila huu ni uchafu, hata nyumba ya mtu binafsi haiwezi kujengwa hivi, Jiji la Dodoma mjitafakari,” alisema Simbachawene.

Kwa upande wake, Ofisa Mifugo wa Jiji la Dodoma, Gratian Mwesigwa alisema wametumia Sh milioni 22 kukarabati jengo hilo.

“Akisema mkubwa ni kutekeleza tu, hayo tuliyoagizwa tutayatekeleza,” alisema Mwesigwa.

Naye, Diwani wa Kata ya Msalato, Ally Mohammes (CCM) alisema kwa sababu mchumi wa jiji alikuwepo, anaamini  mambo yote yatarekebishwa na kukaa vizuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles