24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

Takukuru yapiga marufuku viongozi wa kuchaguliwa kutoa zawadi kwa wananchi

Hadija Omary -Lindi

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Lindi, imepiga marufuku kiongozi yeyote  aliyepo madarakani kwa kuchaguliwa na wananchi au anayetarajia kugombea uongozi, kutoa misaada au zawadi kwa wananchi.

Viongozi waliopigwa marufuku ni wabunge na madiwani waliopo madarakani na ambao wanahitaji kugombea nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Lindi, Steveni Chami, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Kauli hiyo ya Chami imekuja baada ya kuwapo kwa taarifa ya baadhi ya watu ambao wanadhaniwa kutaka kugombea udiwani na ubunge katika mkoa huo kuanza kugawa vitu mbalimbali kwa wananchi.

View Post

Alisema ili kuzuia mianya ya rushwa ni marufuku kwa watu wanaotarajia kugombea nafasi hizo kutoa zawadi hadi Uchaguzi Mkuu utakapopita.

“Tumefuatilia watu hao pamoja na kwamba hawajaweka bayana kuwa wanahitaji nafasi fulani ya uongozi, lakini wameshaanza kugawa vitu mbalimbali ikiwemo mashine za kufyatulia matofali katika vikundi vya vijana, jezi za mpira na pesa taslimu kwa vikundi vya mama lishe.

“Tunachokifanya sisi kama taasisi, kwanza kuwatambua wale wote ambao wanataka madaraka pamoja na kuwafuatilia nyendo zao na tumeshaanza kuwajua, na niwatahadharishe, tunao maofisa wengi wa Takukuru ambao watakuwa wanawafuatilia watu hao kuanzia asubuhi anapoamka mpaka usiku anapoenda kulala.

“Bahati nzuri Rais ameshaagiza wale wote watakaonunua uongozi hawafai na sisi kazi yetu ni kufikisha majina ya wale wanaohitaji uongozi kwa kugawa rushwa kwa Mheshimiwa Rais.

“Sasa niwaambie tu wanaotumia fedha kwa ajili ya kupata uongozi wanajisumbua  kwa  kupoteza fedha zao na muda wao bure,” alisema Chami.

Pia atumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Lindi kuendelea kutoa ushirikiano na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa pale ambapo wataona kuna dalili yoyote ya uwepo wa mianya ya rushwa katika maeneo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles