24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

WALIONUSURIKA AJALI MV BUKOBA WAOMBA ELIMU YA UKOAJI

Na JUDITH NYANGE


SERIKALI imeombwa kutoa elimu ya namna ya kujiokoa kwa abiria wanaotumia usafiri wa majini   kuepusha vifo vya watu wengi kama ilivyokuwa katika ajali ya meli ya MV Bukoba iliyotokea Mei 21, mwaka 1996.

Mmoja wa watu walionusurika katika ajali hiyo,   Charles Limbu, alikuwa akizungumza  wakati wa kumbukumbu ya miaka 21 tangu kutokea kwa ajali hiyo, zilizofanyika juzi katika makaburi ya Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Alisema ni wakati sasa serikali kuhakisha elimu   na vifaa vya kujiokoa vinakuwepo katika vyombo vyote vya usafiri wa majini.

“Abiria wengi hawafahamu namna ya kutumia maboya na vifaa vingine vya kujiokoa vilivyopo katika vyombo vya usafiri wa majini.

“Ni vema serikali ikahimiza na kuhakikisha wasafiri wanapatiwa elimu ya kutumia vifaa hivyo vya kujiokoa  kupunguza madhara  inapotokea ajali.

“Katika ajali ya MV Bukoba wengi tuliopona ni kwa sababu tuliweza kuzingatia elimu tuliyopatiwa wakati tunaanza safari.

“Nilipoona meli imeanza kupoteza uelekeo nilikimbia  kuchukua boya ambalo lilinisaidia  kujiokoa, laiti kama abiria wote wangekuwa wanafahamu  namna ya kutumia vifaa hiyo kusingetokea vifo vya watu wengi,” alisema Limbu.

Limbu aliitaka serikali kuhakikisha vifaa hivyo vinakuwapo sehemu za wazi ambako abiria wote wanaweza kuvifikia na  kwa idadi sawa kulingana na uwezo wa chombo husika.  

  Kiliphece Herman ambaye pia alinusurika katika ajali hiyo, alisema chanzo cha ajali hiyo ni  umasikini wa kutumia kifaa chakavu kusafirishia abiria, ujinga wa jamii na viongozi wanaowajibika kusimamia usafiri   na uzembe kwa wanaopewa jukumu la kuendesha na kusimamia vyombo hivyo.

“Bila mambo hayo kutatuliwa ajali za mara kwa mara zitaendelea kutikoea, nawashauri viongozi wa  serikali  kuichukua jukumu la kupunguza umaskini na kuhakikisha vinakuwapo vifaa bora vya usafiri.

“Kuondoa ujinga kwa walio na jukumu  na mamlaka zinazohusika kusimamia vyombo vya usafiri hasa wa majini na kutoa adhabu kali kwa wale watakaobainika kufanya uzembe kwa kukiuka na kuvunja sheria zilizopo,” alisema Herman.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSC), Eric Hamissi, aliwataka wananchi kuacha kuwa na hofu.

Aliwashauri  wasione baada ya ajali hamna usalama wa usafiri wa majini kwa sababu  baada ya tukio hilo zilichukuliwa  hatua kubwa za kuhakikisha halijirudii na usalama wa abiria  katika meli zao unazingatiwa kwa kiwango cha juu.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema serikali ipo mbioni kununua meli mpya kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri ndani ya Ziwa Victoria pamoja na kuzifanyia marekebisho na ukaguzi wa mara kwa mara  kuhakikisha usalama wa abiria wakati wote.

“Kila  mtanzania kwa imani yake aendelea kuwaombea marehemu wote waliotangulia mbele ya haki na  wote wenye jukumu na dhamana ya suala la usafirishaji.

“Kila mmoja ahakikishe anatimiza wajibu wake katika eneo lake ili kukomesha kabisa matukio ya ajali,”  alisema Mongella.

Tukio hilo kubwa la historia la kuzama kwa meli  ya MV Bukoba  lilitokea alfajiri ya Mei 21, mwaka 1996 zikiwa zimebaki kilometa 56   kufika Bandari ya Mwanza.

Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 800  ambako watano kati yao  walitambulika na familia zao na 130 waliweza kuokolewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles