24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wakurugenzi ruksa kusimamia uchaguzi

NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Rufaa imeruhusu wakurugenzi wa halmashauri, manispaa na majiji kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kutengua uamuzi uliotolewa awali na Mahakama Kuu wa kuwazuia.

Uamuzi huo ulitolewa jana Dar es Salaam na jopo la majaji watano, likiongozwa na Jaji Augustine Mwarija baada ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na Serikali ikipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Majaji wengine katika jopo hilo walikuwa ni Stella Mugasha, Richard Mziray, Rehema Mkuye na Jacobs Mwambegele.

Jopo hilo likitoa sababu za kutengua uamuzi huo wa Mahakama Kuu, lilisema kabla ya wakurugenzi kufanya kazi, huwa wanaapishwa, kwahiyo si kweli kwamba wanapochaguliwa moja kwa moja wanakuwa wasimamizi wa uchaguzi. Hivyo wanafuata utaratibu wa kisheria.

Kuhusu hoja ya wakurugenzi ni wateuliwa wa Rais na  hawawezi kuzingatia matakwa ya Katiba, jopo hilo la majaji lilikubaliana na upande wa Serikali kuwa hayo madai ni ya kufikirika.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Serikali kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi hao kusimamia uchaguzi.

HUKUMU YA MAHAKAMA KUU

Mei 11, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilibatilisha kifungu 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa NEC kuwateua wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Mahakama hiyo pia ilibatilisha kifungu 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu; Dk. Atuganile Ngwala, Dk. Benhajj Masoud na Firmin Matogolo.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Ngwala alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, vifungu hivyo ni batili kwa sababu vinatoa nafasi kwa wateule wa Rais ambao pia si waajiriwa wa NEC kusimamia uchaguzi.

Alisema kifungu cha 7(1), kinasema kuwa kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na Katiba mama ambayo inasimamia nchi.

Alisema lakini pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Alisema lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Alisema kutokana na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa waleta maombi, vimeonyesha pasi na shaka kuwa wasimamizi wa uchaguzi wana masilahi na wateule wao.

Alisema kutokana na hali hiyo, mahakama imeona kuwa vifungu hivyo ni batili na kwamba havifai kutumika wakati wa kusimamia uchaguzi.

“Mahakama imebatilisha vifungu vya Sheria ya Uchaguzi namba 7(1) na 7(3) kutokana na NEC kuteua wakurugenzi wa Jiji, halmashauri na manispaa kuwa wasimamizi wa uchaguzi wakati ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC,” alisema Jaji Ngwala.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na kesi iliyofunguliwa na mashirika kadhaa ya wanaharakati kupitia kwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Wangwe, akitetewa na Wakili Fatma Karume.

Kesi hiyo namba 8/2018 ambayo mjibu maombi alikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), awali ilikuwa inasikilizwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na aliyekua Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambari, ambaye kwa sasa amehamishiwa Mahakama ya Rufaa, Jaji Rehema Sameji, ambaye pia yupo Mahakama ya Rufaa na Jaji Temba amestaafu.

RUFAA YA SERIKALI

Mei 13, mwaka huu Serikali ilitangaza kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia Wakurugenzi (DEDs) kusimamia uchaguzi.

Uamuzi huo ulitangazwa na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Aderladus Kilangi, katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu msimamo wa Serikali kuhusu hukumu hiyo ya Mahakama Kuu.

Serikali kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu, ilikata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga sehemu ya hukumu hiyo hasa uamuzi wa kubatilisha vifungu hivyo.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani vya Julai, mwaka huu rufaa hiyo ambapo yalianza kusilizwa Julai 30 na jopo la majaji watano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles