Magufuli awaweka vigogo tumbo joto

0
643
Rais Dk. John Magufuli akifurahia jambo na wanafunzi wa Shule ya Lukuledi ambayo ni maalumu kwa wenye ulemavu wa kusikia, aliposimama kusalimia wananchi wa Lukuledi, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati akiendelea na ziara yake mikoa ya Kusini jana.

Na ANDREW MSECHU – Dar es Salaam

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nachingwea, Bakari Mohamed, jana walijikuta katika wakati mgumu, baada ya Rais Dk. John Magufuli kukerwa na utekelezaji wa baadhi ya miradi iliyokuwa inawahusu maeneo yao ya usimamizi.

Profesa Mbarawa alikutana na moto wa Rais Magufuli walipofika mjini Masasi, ambako alitakiwa aidha kumfukuza mhandisi aliyekuwa akisimamia ukandarasi wa ujenzi wa chujio la maji au aondoke yeye.

Hata hivyo Rais Magufuli aliamua kubadili maagizo yake na kumtaka mhandisi huyo apewe muda wa kufanya kazi.

“Ninadhani huyu apewe muda, usimfukuze tena kwa sababu hata yeye ana familia inayomtegemea. Basi apewe muda wa kurekebisha hayo matatizo yanayolalamikiwa,” alisema Rais Magufuli.

Kauli hiyo ilitokana na Profesa Mbarawa mara kadhaa wakati Rais akieleza kukerwa na mkandarasi huyo, kusema; “tumekuelewa Mheshimiwa Rais, tutamfukuza tujenge wenyewe.” 

Awali, akiwa wilayani Nachingwea, wananchi waliwashtaki viongozi wa wilaya hiyo kwa Rais Magufuli.

Hali ilibadilika baada ya Rais Magufuli kuamua kutembelea soko lililokuwa likilalamikiwa na kituo cha mabasi, ambavyo ujenzi wake unadaiwa kuchelewa.

Rais Magufuli aliamua kwenda kuliona soko hilo baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mohamed kueleza Sh milioni 71 zimeshatumika, lakini ujenzi haujakamilika kwa mwaka mzima sasa.

Alieleza kukasirishwa kwake na kutotumika kwa fedha zinazotengwa kwa miradi ya maendeleo, hivyo kuwataka watendaji wa Serikali, kuanzia Mkuu wa Mkoa, Zambi, Mkuu wa Wilaya, Muwango na DED Mohamed wahakikishe wanatekeleza wajibu wao.

“Ninataka fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitumike na watu wazione, kuna bilioni 27/- zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo, lakini hazitumiki. Huyu DED anadai tukusanye kwanza mapato, sasa kwanini usitumie kwanza hizi ili ukusanye zaidi?” alihoji.

Akiwa katika eneo la Nachingwea, Rais Magufuli alisema Mkurugenzi Mohamed amemuudhi na kumtaka DC Muwango awe mkali kwa kuwa yeye ndiye Mkuu wa Kamati ya Usalama ya Wilaya.

“Na wewe Mkuu wa Mkoa unapotoa maagizo ni lazima uyafuatilie yanatekelezwaje, ninataka watendaji wanaofanya kazi, kero niliyoikuta pale Nachingwea lazima nyie viongozi muwajibike.

“Soko halijamaliza kujengwa, milioni 71 zimetumika, Mkurugenzi anajifanya amekaa Marekani sijui Marekani alikuwa anokota makopo huko, kwa sababu mambo mengine yanaudhi sana kwa sababu fedha zinazotolewa na Serikali zinatakiwa zikatumike kwa ajili ya maendeleo.

“Stendi mmewahamisha watu, mmewapeleka stendi nyingine wakati bado haijakamilika. Sasa ninaagiza watendaji wa wilaya hii ya Nachingwea mkajipange upya, kama kuna anayetaka kufanya kazi afanye na asiyetaka aondoke,” alisema.

BASHE NA KOROSHO

Katika ziara hiyo ya jana, Rais Magufuli alimsifu Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa amekuwa akifanya vizuri na anachapa kazi, huku akimwagiza kuhakikisha wakulima wote wa korosho wanaoidai Serikali wanalipwa kuanzia Jumanne wiki ijayo.

“Ninakuagiza kuwa Jumanne nahitaji kuona watu wanaanza kulipwa, ninaamini wewe ni mtendaji mzuri, tena kijana  na kwa sababu kwangu wewe ni kama mwanangu, ninaweza hata kukuchapa vikoko kama nitaona hakuna utekelezaji, kwa sababu wewe ni sawa tu na mwanagu,” alisema huku akiangua kicheko.

Awali, Bashe alisema wakulima wa korosho wilayani Nachingwea wanaidai Serikali Sh bilioni 3.4 ambazo zipo tayari na zitaanza kulipwa Jumanne ya wiki ijayo.

Alisema tayari ameshaagiza kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya ushirika waliokula fedha za wakulima na wameshawekwa ndani, na hawataachiwa hadi fedha zilizopotea zipatikane.

Kwa hatua hiyo, Rais Magufuli aliingilia kati huku akimsifu Bashe kuwa ndio aina ya viongozi anaowataka na alitaka kujua jina la kiongozi mwingine wa Amcos ambaye alikuwa bado hajakamatwa.

Alielezwa kuwa kiongozi huyo anaitwa Seif Misele na kuagiza akamatwe haraka na asiachiwe hadi fedha zitakapopatikana.

Awali, akiwa katika eneo la Likungu, Nachingwea, Bashe alisema Serikali inadaiwa Sh bilioni 72 na wakulima wa korosho ambazo zote zitalipwa kabla ya kuanza kwa msimu ujao.

Bashe alisema kutokana na maelekezo ya Rais, safari hii korosho zitauzwa kwa uwazi, hakutakuwa na suala la ushirika kujifungia na kuwaletea bei wakulima.

Alisema wanunuzi wataweka tenda zao mbele ya Amcos na wakulima watajua aliyetenda bei ya juu na wakiridhika nayo watauza na hakutakuweko mtu wa kuwapangia bei.

“Lakini pia tunafahamu mnapulizia dawa zenu kuanzia mwezi wa nne na wa tano, kumekuwa na tatizo la ucheleweshaji wa viuatilifu na mwisho mnanunua kwa bei ghali, tunatengeneza utaratibu kuanzia mwakani Januari, Februari na Machi viuatilifu vyote vitakuwa vimefika kwenye maeneo ya wakulima na Amcos,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here