25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UREMBO WAWAFANYA WATOTO WA KIKE KUGOMA KUSOMEA MAKENIKA

Na Gurian Adolf


KUNA baadhi ya watoto hawafahamu umuhimu wa elimu, hivyo hata uwashauri juu ya umuhimu wa elimu hawawezi kukuelewa.

Hivi karibuni Shirika la Plan International liliamua kujitolea kuwasomesha watoto wa kike wilayani Nkasi mkoani Rukwa, mafunzo ya ufundi wa aina mbalimbali ikiwamo ujasiliamali na makenika.

Jambo la kusikitisha ni kwamba watoto hao walikataa kujifunza ufundi huo wakidai kuwa wao ni warembo hivyo hawawezi kusomea makenika.

Akizungumzia kusikitishwa kwake na suala hilo, Mratibu wa Ndoa za Utotoni wa shirika hilo wilayani Nkasi, Nestory Frank alisema kwa hali hiyo watoto wa kike watakuwa wanaishia mitaani kwa sababu ya kuchagua kazi.

Anasema shirika hilo liliandaa programu maalumu ya kuwapatia mafunzo watoto wa kike waliopata ujauzito katika umri mdogo kutoka kata tatu za Mtenga, Mkwamba na Nkandasi ili waweze kujikwamua na umasikini lakini walikataa kisa ni warembo.

Frank anasema kuwa baadhi ya watoto hao waliacha ghafla kuhudhuria mafunzo hayo.

“Katika kundi hilo la tulioamua kuwasaidia kuwapa elimu ya ufundi, wamo pia wasiojua kusoma wala kuandika lakini wanang'ang'ania kusomea fani ambazo zinahitaji elimu kubwa, sijui wataelewa vipi darasani,” anasema Frank.

Anasema kuwa baadhi ya watoto hao wanataka kusomea ufundi umeme ambao unahitaji elimu kubwa lakini wanaposhauriwa wajifunze makenika wanakataa wakidai kuwa wao ni  warembo na hawawezi kusomea kazi kama hiyo.

Mratibu huyo wa ndoa za utotoni anasema kuwa baadhi ya watoto hao wamekuwa na masharti magumu ambayo hayatekelezeki.

“Kuna ambao tulitaka kuwasomesha ufundi cherehani, lakini wanakwambia hawapo tayari kusomea fani hiyo hadi tuwanunulie cherehani sisi ambao tunawalipia ada, tuwakabidhi ziwe mali yao ndipo wakubali kusomea mafunzo hayo,” anasema.

Anasema kuwa kuna madarasa yalikuwa na wanafunzi 25 lakini 21 wameacha na sasa wamebakia wanafunzi wanne tu.

Anasema kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa kwani lengo la  shirika hilo ni kuwasaidia wao waweze kujikomboa kiuchumi kwa kuwa baadhi yao walikatishwa masomo na hawana ujuzi wowote utakao wasaidia kukabiliana na hali ya maisha.

Frank anataja changamoto nyingine wanayokabiliana nayo katika kujitolea kuwasomesha watoto hao kuwa ni baadhi yao kupata ujauzito wakiwa wanaendelea na mafunzo.

“Yaani hawa watoto walikatisha masomo yao huko nyuma kwa sababu mbalimbali ikiwamo ujauzito, tukaamua kujitolea kuwasaidia lakini cha kushangaza wamekuja hapa na sasa wana ujauzito mwingine,” anasema Frank na kuongeza kuwa hali hiyo imewalazimu kukatisha masomo yao hivyo hawajui watawasaidiaje.

Anasema kuwa Shirika la Plan International kupitia programu hiyo inamlipia kila mtoto hadi Sh 150,000 ili wajifunze ufundi lakini wanaamua kuacha na kurejea mtaani. Wanavyoonekana hawahitaji kabisa mafunzo hayo hivyo wanasababisha fedha kupotea kwa kuwalipia watu wasiotaka kupata ujuzi.

Anasema wanajitahidi kuwabembeleza ili warejee na kupata mafunzo hayo lakini baadhi yao hawataki kabisa na kuacha hali ambayo inasababisha changamoto kubwa katika utekelezaji wa mradi huo ambao unania ya kuwasaidia.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya kuwasaidia watoto hao, Josephat Joseph anasema miongoni mwa matatizo wanayokumbana nayo ni wanawake ambao wazazi wa watoto hao wanaonekana kuridhika na vitendo vinavyofanywa na watoto wao.

“Tunadhani hawa wazazi hawafahamu umuhimu wa elimu ndio maana hata hawahangaiki kuwakazania watoto wao kuja kupata ujuzi.

“Hawafahamu ya kuwa ujuzi huu tunaowapatia watoto wao utawasaidia kuinua kipato cha familia hatimaye kuondokana na mzogo wa kulea wajukuu wasiokuwa na baba,” anasema Joseph.

Anasema inatia aibu kuona mtoto wa kike aliyekatishwa ndoto zake kwa kupewa mimba akiwa katika umri mdogo, lakini amepata fursa ya kupata mafunzo kwa kulipiwa ada na wasamaria wema lakini hawathamini jambo hilo.

Anasema kuwa programu hiyo ni ya muda tu na itakapo malizika itawaacha katika umasikini kwani wameshindwa kuitumia vizuri na hata watoto waliozaa watakuwa masikini kwa kuwa wazazi wao watashindwa kuwalea vizuri kutokana na kukosa kipato cha uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles