28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

ULAYA WAKUBALI KUPOKEA WAKIMBIZI

BRUSSELS, UBELGIJI

NCHI kadhaa za Umoja wa Ulaya zimeafiki kupokea wakimbizi wapya baada ya tahadhari iliyotolewa na Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Ulaya umekubali kupokea wakimbizi 34,000 kutoka nchi za Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika, baada ya Umoja wa Mataifa kuzituhumu nchi za Ulaya kuwa zinashirikiana na maofisa wa Serikali ya Libya kuzuia wakimbizi wanaoomba hifadhi barani Ulaya.

Suala hili la kukubaliwa wakimbizi katika nchi 16 za Umoja wa Ulaya limekuja wakati nchi hizo kwa muda sasa si tu kwamba zimekuwa zimegoma kupokea wakimbizi wapya, bali pia zimekuwa zikiwafukuza wale waliokwisha kuwasili katika nchi za bara hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni idadi kubwa ya wakimbizi imekuwa ikielekea barani Ulaya kutoka nchi za Mashariki ya Kati na Afrika, kutokana na kushadidi machafuko na mapigano katika nchi hizo.

Japokuwa baadhi ya wakimbizi wamefanikiwa kuingia Ulaya, lakini sera zisizofaa za nchi za bara hilo na kufeli kwa usimamizi wa masuala ya wakimbizi katika nchi hizo kumezusha mivutano ya kisiasa na kijamii na kusababisha matatizo ya kiuchumi barani Ulaya.

Katika upande mwingine, mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea barani Ulaya yametumiwa na baadhi ya nchi za bara hilo kama kisingizio cha kufunga mipaka yao mbele ya wakimbizi au kuweka mashinikizo na sheria kali dhidi ya wale waliokwishaingia katika nchi hizo, hususan wakimbizi Waislamu.

Kuhusu suala hilo, Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mpaka imetangaza kuwa: “Ni aibu na fedheha kuona nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zikitumia ukatili na mabavu kwa ajili ya kuzuia wakimbizi vijana na watoto kuingia katika nchi hizo.”

Libya inatambuliwa kuwa miongoni mwa vivuko na njia kuu zinazotumiwa na wakimbizi, hususan Waafrika kwa ajili ya kuelekea barani Ulaya. Mgogoro wa kisiasa na mapigano ya ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imewapa fursa raia wa nchi za Afrika na nchi nyingine zilizokumbwa na machafuko kutumia ardhi ya Libya kwa ajili ya kuvuka Bahari ya Mediterania na kuingia Ulaya.

Vita na mapigano ya ndani, harakati na mashambulizi ya kigaidi katika baadhi ya nchi za Afrika, ukame na njaa, matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira na kazi, vinatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowalazimisha vijana na raia wengi wa Afrika na Mashariki ya Kati kuomba hifadhi katika nchi za Ulaya.

Pamoja na hayo, maofisa wa nchi za Ulaya, hususan Italia na Ugiriki, ambazo ndizo malango makuu ya kuingilia Ulaya, tofauti na ahadi zao eti za kujali masuala ya kibinadamu, wameweka sheria kali na kukabiliana vibaya na kikatili na watu wanaoelekea katika nchi hizo kwa ajili ya kupata hifadhi kwa kadiri kwamba taasisi nyingi za kimataifa zimetoa wito kwa nchi za Ulaya kutazama upya sheria na sera zao za waajiri.

Kwa sasa na kutokana na mashinikizo ya kimataifa, nchi za Ulaya zimekubali kupokea karibu wakimbizi elfu 35, wakati hali ya mambo katika baadhi ya nchi za Afrika ikiendelea kuwa mbaya zaidi. Hivyo inaonekana kuwa, hatua hiyo ya kukubali wakimbizi wapya ni sera ya muda mfupi na kwa msingi huo utatuzi wa mgogoro wa wakimbizi unahitaji maamuzi ya busara zaidi, ikiwa ni pamoja na kutazama upya sera na siasa za nchi za Magharibi za kuchochea na kuanzisha vita na machafuko katika maeneo mbalimbali ya dunia kwa maslahi ya kisiasa au kiuchumi.

Vilevile nchi za Magharibi zinapaswa kujali na kulipa kipaumbele suala la ustawi katika nchi za Afrika na kusaidia jitihada za kuanzisha miundombinu imara na ya muda mrefu, badala ya kuweka mbele misaada yenye masharti magumu ambayo mara nyingi huzidhuru nchi za Afrika badala ya kuzifaidisha.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles