23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO KABWE NINAYEMTAKA

Na ADO SHAIBU

PANGANI Msigwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA mkoani Njombe, ni swahiba wangu tuliyeshibana. Tumesoma wote UDSM, yeye akichukua Shahada ya Kiswahili, nami nikiogelea kwenye Sheria. Sote tulikuwa pia viongozi wa serikali ya wanafunzi, yeye akiwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI), nami nikiwa Katibu wa Shule ya Sheria na Bodi (Mahakama ya DARUSO).

Serikali ya wanafunzi ilipoamua mwaka 2012 kuchukua mkondo wa kimapambano dhidi ya utawala wa Chuo ili kuwatetea wanaharakati waliofukuzwa chuoni kwa kupigania mikopo, Pangani alikuwa msiri wangu mkubwa.

Nilikuwa huru kumwambia lolote la kimapambano bila hofu ya jambo hilo kuvujishwa kwa watawala wa Chuo. Hivyo basi, haikushangaza pale utawala wa Chuo ulipoamua kuwasimamisha na baadaye kuwafukuza kabisa baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi, mimi na Pangani tulikuwa moja ya wale waliozawadiwa kadi nyekundu.

Hadi sasa, Pangani ni rafiki yangu, licha ya kutenganishwa na umbali na itikadi. Nikimpigia simu lazima nianze kwa mbwembwe: “Ndimi Mwana wa Mungwe Mvunja vichwa kwa mkuki”. Naye angejibu kwa tambo “Ndimi Mwana Shupavu wa Azania ninayeweza kuyaamuru majabali hama yakahama”.

Baada ya tambo hizi tulizoziiba kwenye tamthilia inayosisimua ya CHUANO na kuziongezea chumvi hapa na pale, ndipo tungeendelea na mazungumzo mengine.

Urafiki wangu na Pangani haumaanishi kuwa tulikubaliana kwenye kila jambo. Moja ya mambo tuliyopishana ni kuhusu kusimamishwa kwa Zitto Kabwe ndani ya Chadema. Wakati mimi nilikitazama kinachoendelea kama mnyukano wa madaraka, Pangani alimuona Zitto kama mtu anayevuruga chama.

Miaka imepita. Sasa hatuzungumzi tena sana mambo haya. Rais John Magufuli ametengeneza mazingira ambayo yanawalazimisha wapinzani kusahau tofauti zao na kumkabili kwa pamoja adui anayetishia ustawi wa kidemokrasia.

Nikiwa UDSM, ingawa sikuvutiwa kujiunga na vyama vya siasa kutokana na nakisi ya kiitikadi na vyama kutojibidiisha na matatizo ya msingi ya wanyonge, hasa wakulima vijijini, ni ukweli wa mambo kuwa niliyakubali mambo mengi ya Zitto Kabwe, hasa umahiri wake kwenye kujenga hoja.

Nilimweleza Pangani “wamungwe, katikati ya uhaba mkubwa wa viongozi wachambuzi na wajenzi wa hoja hatuwezi kumpoteza Zitto Kabwe kwa sababu za kutunga”.

ACT Wazalendo kilipoanzishwa, Pangani na marafiki wengine walibashiri kwamba nitajiunga nacho. Ndivyo ilivyokuwa. Nilifanya kwanza kazi kama mtafiti wa mgombea urais, Anna Mghwira na baadaye Katibu Mwenezi wa chama.

Nilikutana na Zitto Kabwe kwa mara ya kwanza 2013, alipoalikwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere kufanya uchambuzi linganishi (Comparative Analysis) wa Azimio la Arusha na Dira ya Maendeleo mwaka 2025.

Baada ya kongamano nilimsogelea akiwa anaondoka. “Naitwa Ado Shaibu, naomba namba yako ya simu”. Aliichukua simu yangu na kuandika namba yake, kisha akanitazama usoni: “Wewe ndio umeandika ile makala? Umetusema sana”.
Tangu hapo mimi na Zitto tumekuwa na mahusiano. Kwanza tuliunganishwa na vitabu na baadaye tukaunganishwa na siasa.

Licha ya umahiri wake wa kujenga hoja, bado ndani ya moyo wangu kuna Zitto fulani niliyemtaka. Kazi ya siasa ni mwendo. Nilitamani Zitto ausome moyo wangu juu ya “Zitto Nimtakaye” ili kwenye mwendo wake akazanie yale yanigusayo na ajiepushe na yale nisiyoyapenda. Pengine na wengine ndani na nje ya chama wanaye Zitto Wanayemtaka.

Ambacho nilikisahau ni kuwa sifa na tabia za kiongozi yeyote ni zao la mambo mawili; mazingira ya kisiasa ya wakati husika na msukumo wa watu wenye ushawishi wanaomzunguka.

Kwa bahati nzuri, mazingira ya sasa yanatoa fursa ya kumpata Zitto nimtakaye. Na kwa bahati, yeye mwenyewe anaitikia kwa kasi matakwa ya kimazingira.

Ni Zitto gani nimtakaye?

Ninamtaka Zitto ambaye licha ya kupigania maendeleo, atambue wajibu wa kimapambano wa wanasiasa na vyama vya siasa kupigania demokrasia na haki za raia ndani na nje ya Bunge. Zitto nimtakaye ni lazima atambue kuwa, wajibu huu ni hatari wenye gharama kubwa.

Zitto nimtakaye anapaswa kufahamu kuwa, CCM haitaki ustawi wa vyama makini vya upinzani.. Hata sasa, mipango hiyo haijakoma na haitakoma. Upinzani goigoi ni nafuu kwa CCM.

Kwa hiyo, Zitto Kabwe nimtakaye akiwaona akina Humphrey Polepole wanatokwa povu kwa taharuki kutokana na hoja zake, ashikilie hapohapo asiache, kwani ni dalili ya “sindano kuingia”. Zitto nimtakaye ni lazima ajue uimara wa Chama cha upinzani hauwezi kupimwa na CCM. Chama cha upinzani hakihitaji hata punje, sifa wala hisani kutoka CCM.

Zitto nimtakaye ni lazima awekeze kwa vijana. Niliguswa alipoulizwa na wanahabari kuhusu viongozi kuhama chama.
Zitto: “Ado pita mbele. Mlimjua huyu tarehe kama hii mwaka jana?” Wanahabari: “Hapana”.
Zitto: “Ni kweli wengi wenu hamkumjua. Lakini sasa mnamtafuta wenyewe kwa ‘kumnukuu’. Wenyewe mnapenda kumuweka na Humphrey Polepole. Na Polepole akimuona huyu anajificha kwenye meza. Tunawekeza kwa vijana.”

Tunawekeza kwa vijana wanaoabudu misingi badala ya kuabudu watu. Vijana imara watakaoielewa, kuboresha na kuipigania itikadi, falsafa na sera za chama.

Zitto nimtakaye ni lazima atambue kuwa, adui wa Watanzania ni ufukara wa watu wetu unaozalishwa na ubepari. Kwa hiyo, kumwangamiza adui huyo ni lazima kwanza kumwangamiza wakala wake. Kwa hiyo, nguvu, fikra na hisia lazima zielekezwe katika kukabiliana na CCM. Ni muhimu kutambua kwamba, si watu wote watafurahi yeye na chama wakitekeleza wajibu huo. Cha msingi ni kusonga mbele hadi CCM wapagawe. Pa kusifia tusifie. Pa kukosoa tukosoe bila kumtazama mtu usoni.

Zitto nimtakaye ni lazima aendeleze siasa za masuala. Azungumze kilimo, hali ya maisha, viwanda, biashara, elimu, afya, umoja na mshikamano wa Afrika.

Nina imani, Zitto nimtakaye atakuwa na wajibu wa kihistoria kwa Tanzania na Afrika. Wajibu huo ni kikombe ambacho ni lazima akinywe.

Mwandishi wa makala haya ni Katibu, Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT Wazalendo. Simu: 0653619906. Baruapepe: [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles