25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tume huru ya uchaguzi ‘yawaponza’ Mbowe, Zitto

Mwandishi Wetu -Mororgoro

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, kimesema hakuna tume ya uchaguzi duniani inayoongozwa na malaika kwani zote huwa na wajumbe ambao ni binadamu wanaotenda haki kwa mujibu wa viapo vyao kisheria, wakizuiwa kutoshiriki batili na kutenda haki.

CCM imesema kuwa hata kwenye uchaguzi mkuu wa Chadema uliomrudisha madarakani Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, wajumbe waliosimamia uchaguzi huo walikuwa ni binadamu.

Akizungumza jana mjini hapa, Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alisema hoja ya Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe kutaka tume huru ya uchaguzi katika uchaguzi wa mwaka 2020, lazima watambue kuwa kila nchi ina utaratibu wake na si kuongozwa kwa vitisho na kebehi.

Alisema kwa miaka yote Tume ya Uchaguzi huwa na viongozi ambao hula viapo kwa uadilifu na kutenda haki bila kuwa na upendeleo na huongozwa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.

Alisema ni vema vyama hivyo vionyeshe mfano wa kuunda tume huru ya uchaguzi kwa kuwa na wajumbe ambao watatoka katika vyama vingine vya siasa.

Shaka alisema katika uchaguzi mkuu mgombea hupigiwa kura na kushinda ambapo mchakato wake huendeshwa kikanuni na kisheria na wala si mzunguko wa tume, kwani tume haipigii kura vyama vya siasa bali uwezo binafsi wa kila chama kulingana na sera au kukubalika kwa wagombea wake.

“Vyama vya Chadema na ACT Wazalendo kwa kushirikiana na baadhi ya asasi za kiraia, zimesema zitashinikiza kufanyika mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020.

“Miongoni mwa mabadiliko hayo, vyama hivyo vinataka iundwe tume huru ya uchaguzi na kuwepo uwezekano wa kupinga matokeo ya urais mahakamani.

“Ni lazima wajue kwamba Tanzania ni nchi huru na hujipangia mambo yake kwa mujibu wa sheria na si kufuata mashinikizo kutoka kwa watu au mabeberu,” alisema Shaka.

Alisema madai hayo ni kutapatapa kwa viongozi wa vyama hivyo wakisaidiwa aidha na washirika wao wa ndani na nje au baada ya kuona hawana nafasi ya kukishinda chama tawala kutokana na utendaji wake ufanisi na uwajibikaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Shaka alisema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Rais Dk. John Magufuli katika maendeleo ya kisekta, imerudisha imani kwa wananchi, hivyo ni wazi vinajua havitapata kura badala yake upinzani utadhoofika, kupoteza dira kwa umma.

“Mbowe amelalamikiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Mashariki, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye aliyedai wazi kuwa ilifanyika mizengwe, vitisho na ghiliba.

“Uchaguzi ukafanyika na kupatikana mwenyekiti. Uchaguzi mkuu pia utafanyika kwa mujibu wa katiba na kalenda, chama chenye ubavu kijiandae kushuka dimbani kupambana na mwamba wa siasa CCM,” alisema Shaka.

Alisema ikiwa upinzani umeishiwa hoja, haulipui tena mabomu ya hujuma, ufisadi au kukosekana huduma za kijamii kwa wananchi, bila shaka wamefilisika, hivyo wanasubiri manusura, waonewe huruma na wananchi ili wasikike kama wapo, huku akidai kuwa Mbowe na Zitto wasidhani watabaki kuwa wabunge.

“Nchi moja jirani yuko mpinzani amepiga sana mayowe, akajitangaza mshindi na kujiapisha urais, amechoka badala yake amekimbilia Ikulu kupeana mkono na Rais.

“Yuko mwingine kule Zanzibar toka 1995, 2000, 2005 anatangatanga na dunia, mwishowe 2010 akamtambua Rais aliyempinga, 2015 akachomoa tena betri, sasa anaanza ukorofi kabla uchaguzi 2020, atapata kipigo cha kisiasa kuliko vipigo vyote alivyowahi kuvipata nyuma,” alisema Shaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles