Imechapishwa: Wed, Sep 13th, 2017

TRUMP ADAIWA KUSHINDWA MGOGORO WA QATAR

NEW YORK, MAREKANI


GAZETI la New York Times limesema kuwa Rais Donald Trump ameshindwa kutatua mgogoro wa Qatar na nchi nne za Kiarabu zinazoongozwa na Saudi Arabia.

New York Times limegusia safari ya Amir wa Kuwait, Sabah Ahmad Jabir al Sabah nchini Marekani na mazungumzo ya simu ya Trump na Amir wa Qatar na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia.

Gazeti hilo liliandika juhudi za Trump za kutatua mgogoro wa nchi hizo za Kiarabu kwa mazungumzo ya moja kwa moja baina ya Riyadh na Doha zimeshindwa kiasi kwamba Saudia imetangaza hadharani kuwa imesimamisha kikamilifu mazungumzo yake na Qatar.

Gazeti hilo liliongeza: “Trump alizungumza kwa simu na Amir wa Qatar, Tamim bin Hamad Aal Thani na mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman na kuwataka watatue mgogoro wao. Pamoja na hayo Saudia ilisema imesimamisha kikamilifu mazungumzo yake yote na Qatar.”

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Mohammad bin Abdul Rahman Aal Thani, alisema nchi yake haiwezi kukubaliana na masharti 13 yaliyowekwa na Saudia na washirika wake, kwa vile yanakwenda kinyume na haki yao ya kujitawala.

Saudia, Muungano wa Falme za Kiarabu,  Bahrain na Misri ziliiwekea vikwazo vya kila upande Qatar Juni 5, mwaka huu kwa madai inaunga mkono ugaidi na kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

TRUMP ADAIWA KUSHINDWA MGOGORO WA QATAR