24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TRA YAENDESHA ZOEZI LA KUSAJILI WALIPAKODI KWA MAFANIKIO  

 

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAAM


MIONGONI mwa majukumu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni kuhakikisha inasajili walipakodi na kuwatambua pia.

Lengo la jukumu hili kwa TRA ni kuongeza idadi ya walipakodi, kupanua wigo wa ulipaji wa kodi ikiwa ni pamoja na kuongeza makusanyo.

Sambamba na hayo lengo, lingine ni kuweza kuwa na taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi ili kuchangia pato la Taifa.

Hivi karibuni TRA ilizindua Kampeni ya Usajili wa Walipakodi nchini kwa lengo la kuongeza idadi ya walipakodi pamoja na wigo wa ulipaji kodi na makusanyo.

Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya, anasema TRA ina jukumu la kuhakikisha inakusanya mapato lakini pia kuwatambua walipakodi wake na kuwatengenezea mazingira mazuri yatakayowawezesha kulipa kodi bila usumbufu na kwa hiyari.

Anasema pia TRA ina jukumu la kuhakikisha kila mwananchi anayestahili kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), anasajiliwa na kuipata kwa urahisi.

Anasema kampeni hiyo itasaidia kuongeza idadi ya walipakodi pamoja na kupanua wigo wa ulipaji kodi utakaowezesha makusanyo kuongezeka.

Mwandumbya anasema kampeni hiyo itafanya usajili wa TIN kwa walipakodi bila malipo yoyote na kwamba usajili huo utafanyika katika ofisi za TRA katika vituo maalumu vitakavyokuwa vimeteuliwa.

Anaongeza kuwa walipakodi wadogo wanaostahili kulipa kodi kwa njia ya makadirio badala ya kutayarisha hesabu, robo ya ya kwanza ya malipo watatakiwa kuilipa ndani ya siku tisini kuanzia siku waliposajiliwa.

Anasema kutokana na mikakati madhubuti ambayo TRA imejiwekea katika kuhakikisha inawarahisishia walipakodi ulipaji wa kodi, waliamua kuubadili utaratibu wa zamani uliokuwa ukiwataka wafanyabiashara kulipa kodi hata kabla hawajaanza kufanya biashara.

Anasema ili kuepuka udanganyifu kutoka kwa watu ambao si waaminifu, TRA haijatoa jukumu kwa wakala yeyote la kusajili au kutoa fomu za usajili wa walipakodi na kwamba wananchi wanatakiwa kuwa makini na vishoka ambao wanaweza kuwalia pesa zao.

Anasema ili mlipakodi aweze kusajiliwa, anatakiwa kuwa na mkataba wa pango au uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua ya mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ikiwa na muhuri pamoja na namba ya simu ya mwenyekiti.

Anaongeza kuwa kitambulisho cha mhusika kama hati ya kusafiria, leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura.

Anasema mhusika anatakiwa kufika ili aweze kupigwa picha pamoja na kuchukuliwa alama za vidole vyake.

Mwandumbya anasema TRA inawataka wafanyabiashara wote nchini wanaofanya biashara bila ya kuwa na namba ya utambulisho au walikwamishwa  katika siku zilizopita, kujitokeza ili waweze kusajiliwa na kupatiwa TIN ambazo hutolewa bure.

Anasema wananchi wanatakiwa kuwa wazalendo kwa Taifa lao kwa kulipa kodi kwa hiyari ili kuepuka usumbufu wa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Anasema kwa kulipa kodi kutaiwezesha Serikali kufikia lengo lake la kutekeleza majukumu yake kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vitakavyozalisha ajira kwa wingi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles