23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

GAVANA NDULU ASTAAFU KWA KISHINDO

NA JOSEPH LINO


GAVANA Mkuu wa Benki ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, anastaafu kwa kishindo kwa kuweka rekodi ambayo haijawahi kutokea nchini kwa kuzifutia leseni kwa mpigo benki tano kwa kukosa kufikia kigezo cha kuwa na mtaji wa kutosha kufanyia kazi.

Benki hizo ni Covenant Bank for Women Ltd, Efatha Bank Ltd, Kagera Farmers Cooperative Bank, Njombe Community Bank na Meru Community Bank.

Benki Kuu imezifutia leseni hizo baada ya kushindwa kutekeleza mpango mkakati wa kuongeza kiwango cha mtaji kinachotakiwa baada ya kupewa muda.

Wakati huo huo, benki zingine tatu ziko chini ya usimamizi wa Benki Kuu kufuatia kuwasilisha mikakati inayokubalika kuongeza mtaji na kuwa endelevu. Benki hizo ni Kilimanjaro Cooperatives, Tanzania Women’s Bank na Tandahimba Community Bank na hivyo zitaendelea na utoaji huduma kama kawaida.

Watu wengi wametaharuki kusikia hali hiyo ambayo benki imeahidi kuanza malipo ya makato ya Sh milioni 1.5 kwa kila mteja ndani ya mwezi mmoja ikisubiri hesabu sahihi baada ya makusanyo ya madeni ya mabenki hayo kwa wateja ili kujua kiasi gani kimepatikana.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Gavana anayemaliza muda wake, Profesa Benno Ndulu alisema benki hizo zimeshindwa kukidhi matakwa ya sheria ya kufikisha mtaji wa Sh bilioni mbili kwa kipindi cha miaka mitano kama inavyotaka.

Aidha, benki za Kilimanjaro Cooperatives, Tanzania Women’s Bank na Tandahimba Community Bank zimepewa muda wa miezi sita kuanzia Januari 4, hadi Juni 30, mwaka huu kuhakikisha zinaongeza mitaji yao.

Alisema benki hizo tano zilishindwa kuandaa na kuwasilisha  BOT mpango mkakati unaokubalika wa kujinusuru wa kuongeza mtaji.

“Kutokana kutotimiza matakwa ya sheria ya kuwa na mtaji kamili na wa kutosha, Benki Kuu imeamua kuzifunga, kusitisha shughuli zake zote na kufuta leseni za biashara ya kibenki  na kuziweka chini ya ufilisi kuanzia Januari 4, mwaka huu,” alisema Profesa Ndulu.

Alisema kutokana kufutwa kwa Benki hizo tano, zinakuwa chini ya Bodi ya Bima ya Amana (DIB) ambayo itaendesha na  zoezi la ufilisi.

“Benki Kuu imeiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi wa benki tano hizo kuanzia leo (jana) kwa ajili ya ufilisi wa mali na kulipa amana za wateja, wadeni na wanahisa wa benki hizo,” alifafanua Ndulu.

Huu ni msimamo mpya kwa upande wa BoT kwani ufilisi wa zamani ulikuwa unafanywa na watu binafsi, lakini huu unafanywa na taasisi na hivyo kuonesha ukomavu wa uendeshaji mambo na ukubwa wa tatizo lenyewe.

Tathmini iliyofanyika na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Benki wa BoT, Kened Nyoni, inaonekana jumla ya amana ya benki zote nane ni Sh bilioni 67.6  ikiwa sawa na asilimia 0.38 ya amana zote za sekta ya benki.

Kwa maelezo ya Profesa Ndulu ni kuwa benki hizo zilipewa muda wa miaka mitano tangu mwaka 2012, ambapo Benki Kuu iliongeza kiwango cha chini cha mtaji wa benki za wananchi (community banks) kuwa Sh bilioni 2 kutoka Sh milioni 250.

Alisema Benki hizo zilipewa muda wa miaka mitano ili kuongeza mtaji kufikia kiwango kipya ambao muda wake uliishia Juni 30, mwaka jana na ukaongezwa kwa miezi sita zaidi iliyoishia Desemba 31, mwaka jana.

“Jumla ya benki nane hazikuweza kuongeza mtaji kufikia kiwango kamili kilichohitajika. Benki tano hizo zilishindwa kuandaa na kuwasilisha Benki Kuu mpango mkakati unaokubalika wa kuongeza mtaji na kuzifanya endelevu,” alisema Ndulu.

Hatima ya benki zilizowekwa viporo

Kwa upande wa benki za Kilimanjaro Cooperatives, Tanzania Women’s Bank (TWB) na Tandahimba Community Bank ambazo kiwango cha mtaji hakikidhi, zimewasilisha benki kuu mipango mkakati inayokubalika wa kuongeza mtaji na kuzifanya ziwe endelevu.

“Benki hizi zimepewa muda wa miezi sita hadi kufikia June 30 mwaka huu kuweka mtaji na kutekeleza mipango hiyo, endapo zikishindwa kutekeleza agizo hilo zitafutwa na kuwekwa chini ya ufilisi,” alifafanua Ndulu.

Habari zinazoaminika zinasema kuwa Benki ya NMB Plc ambayo serikali ina hisa asilimia 32 inafikiria namna ya kuinusuru Benki ya Wanawake (TWB) kwa kununua hisa zake ili kuongeza mtaji wake na kuweza kuanzisha dirisha mahsusi kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali wanawake ambao wanaonekana kushamiri siku hizi kutokana na programu mbalimbali za kuwawezesha.

Profesa Ndulu anasema Serikali ikiwa kama mmiliki pekee wa Benki ya Wananwake amekaribisha wawekezaji kutoka sekta ya umma kuja kununua hisa za TWB na NMB imeonyesha nia na mazungumzo yanaendelea  vizuri kati yao.

Habari za kuaminika za Kibenki zinadai kuwa barua ya nia ilikwisha andikwa na NMB na kwa siku za karibuni TWB inaonekana kufanya vizuri kwenye Soko kwani Robo ya tatu ya mwaka jana amana ziliongezeka kwa asilimia 14 na kufikia Sh bilioni 15.81 kutoka bilioni 13.83 ya mwezi Juni na mikopo chechefu kupungua kwa kiasi cha asilimia 6 ndani ya miezi mitatu.

Tandahimba imeingia mkataba wa miaka mitatu na benki ya CRDB na inaendelea vizuri na kuanza kupata faida wakati Kilimanjaro Cooperatives wamiliki wake vyama vya ushirika vya Kilimanjaro vimeazimia kuongeza mtaji unaotakikana na kunusuru hali ya shari.

NMB ni benki ya pili kwa ukubwa wa mizania inamapenzi na ujuzi wa kukopesha watu wa kipato cha chini na pembezoni mwa uchumi na hivyo TWB itakuwa kwenye mikono mema.

Hatima ya wateja wa benki  

Kwa mujibu wa Benki Kuu, Bodi ya Bima ya Amana (DIB) inasimamia benki yoyote iliyofilisika na kuchukua dhamana ya kulipa fidia ya bima wateja wenye amana (depositors) wanaodai benki na wanahisa.

Alisema Bodi ya Bima ya Amana inawalipa wenye amana wote kwa kiasi cha ukomo wa Sh milioni 1.5 ambapo wenye amana hupewa kipaumbele, na fedha zikibaki wanaoidai benki hulipwa na wanahisa huwa mwisho kulipwa kama fedha zimebaki.

“Wateja wote wa benki zilizofungwa  watalipwa fedha  zao na Bodi ya Bima ya Amana(DIB), ambapo kwa  wale wenye fedha chini ya Sh milioni 1.5 watalipwa fedha zote lakini wale wenye fedha nyingi kwa mfano Sh milion 10 au 300 watalipwa Sh milioni 1.5 ambacho ni kiwango cha mwisho,” alisema Ndulu. DIB ni taasisi  ndani ya mfumo wa benki kuu inayoshugulikia  majanga kama hayo yakitokea na ipo kama hadahari kwa uwekezaji wa amana katika mabenki.

“Naamini zaidi ya asilimia 90 ya wenye amana kwenye benki hizi watalipwa fedha yao kikamilifu kwa sababu wengi wao ni wadogo wadogo,”

Pia alielezea kuwa baada ya wenye amana kulipwa na fedha zimebaki wanayoidai benki watalipwa na zikibaki tena wanahisa ndio wanalipwa mwisho.

Kimsingi wenye hisa ndio wenye benki na mali na hivyo ni wenye kuchukua dhamana (risk takers)yote ya hatima ya benki na hivyo watakuwa wa mwisho kulipwa kwani kwa muda mwingi walikuwa wanalipwa faida kama gawio na huu ni wakati wa wao kuonja chungu ya biashara.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Richard Malisa alifafanua kuwa sheria inataka tufanye haraka iwezekanavyo na wanajipanga kuanza kazi ya kufuatilia benki zilizo chini ya ufilisi.

“Kwa kawaida ya sheria ya kimataifa huchukua siku saba kuanza kulipa wenye amana lakini kutokana na mfumo wetu ndani ya mwezi mmoja tutakuwa tumekamilisha na kutoa taarifa,” alisema Malisa.

Bodi ya Bima na Amana itakuwa na jukumu la kukusanya bila kukosa madeni ambayo benki zilizofilisiwa zinadai na kumiliki kila mali za benki na kufanya taratibu zote za ulipaji wa wateja wake.

Profesa Ndulu alifananua kuwa kufungwa kwa benki hizo tano hakuwezi kuathiri sekta ya fedha nchini kwa kuwa hizo ni benki ndogondogo.

“Hizi benki nyingi ni ndogo haziwezi kuleta mtikisiko kwenye sekta ya fedha kwa sababu shughuli zake ni ndogo ikifananisha sekta ilivyo kwa ujumla wake,” na kushauri wanaotoa huduma kwenye benki watafute njia mbadala kwa sababu haziwezi kufanya kazi tena.

Matatizo ya benki ndogondogo

Alifafanua kuwa  matikisiko mkubwa unaozikumba benki ndogo ni kutokana na wigo wa biashara zao.

“Mara nyingi uwigo  wa biashara yao ni mdogo na hawajawahi kufikia na wakaanza kupata faida, kitu kinachokua ni mtaji, ukubwa wa bodi, na gharama zingine za uendeshaji ambazo kwa kawaida zinahitaji kuhimili ukiwa na biashara iliyokubwa zaidi,”

“Mara nyingi benki zimeshindwa kujipanua na kufanya biashara ya kuweza kuhimili gharama za kujiendeshea.

“Tulishauri jumuiya ya benki hizi ndogo kuungana na kufanya benki kuwa moja. Tuliwaambia ili benki hizi ziweze kupata faida wafanye shirikisho la kuwa benki moja kwa sababu inapunguza gharama za uendeshaji,” alisema

Kauli hiyo ilirudiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mabenki na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Charles Kimei ambaye anasema Benki zote ndogo ndogo au za Ushirika zitawajibika kuingia umoja (merger) au kununuliwa (acquisition) kwani vinginevyo hawatamudu ushindani  mkali na mgumu uliopo sokoni kwa ajili ya udogo wao  na kwa kukosa mvuto wa kutengeneza faida kubwa kwa wawekezaji wao.

Hali ya benki ya Twiga

Ikumbukwe kuwa mwaka 2016 Benki Kuu  ilitangaza rasmi kuchukua usimamizi wa Benki ya Twiga Bancorp kutokana na upungufu wa mtaji wa benki hiyo kiasi cha kuwa na deni la Sh bilioni 21.

Profesa Ndulu Benki alisema kuwa hali ya benki hiyo  inaendelea kuimarika kwa kiwango cha kuridhisha.

“Benki ya Twiga inafanyakazi vizuri na mtaji wake umeimarika na umekua na sasa haipo kwenye hali ya wasiwasi tena.,” alisema

Wadau  washituka

Gazeti la Mtanzania lilitembelea benki ya Covenant Bank for Women Ltd iliyo maeneo ya Makumbusho jijini Dar es Salaam kwenye jengo la LAPF ambapo iliona hakuna watu kama wateja, milango ilikuwa imefungwa na tangazo la Benki Kuu  kubandikwa mlangoni huku askari polisi wanaendelea kulinda.

Pia Mtanzania ilipofika katika benki ya Efatha, mali ya Efatha Church Ministry inayoongozwa na Mtume na Nabii Josephat Mwingira iliyopo eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam pia milango ilikuwa imefungwa na kufuri na polisi na wanaendelea kulinda eneo hilo.

MTANZANIA lilizungumza na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, ambaye alisema kufungwa kwa benki hizo kunamaanisha kupungua kwa mitaji hivyo jambo la kujiuliza ni kwanini mitaji hiyo imepungua.

“Bila shaka ni kwamba biashara haziendi. Na hizo biashara haziendi pengine ni kwa sababu kuna hali ngumu ya kibiashara inayosababisha wafanyabiashara wanaokopa kushindwa kurejesha mikopo yao hivyo kula mitaji.

“Kufungwa kwa benki tano kwa mara moja sio jambo la kawaida, hivyo kama Benki Kuu itashindwa kuondoa hofu kwenye soko wenye fedha zao wanaweza kuingiwa hofu na kutoa fedha zao kwa kuhofia kuwa kuna hali mbaya ya kifedha,” alisema Profesa Ngowi.

Alisema wamiliki wa mabenki wanatakiwa kuendana na matakwa ya nchi ya mtaji ili wasifilisike kama ilivyotokea.

“Vile vile BoT iendane na matakwa ya kifedha ya mashirika ya fedha ya kimataifa kwani hali inaonesha udhaifu fulani”.

Kuhusu athari ya kufungwa kwa benki hizo katika kuelekea uchumi wa viwanda Profesa Ngowi alisema kuwa hakuwezi kukwamisha juhudi hizo kwa sababu benki zilizofungwa ni ndogo na zinahusu wateja wa kawaida na sio wawekezaji wakubwa.

“Hizi ni benki ndogo zenye mitaji ya kawaida si kama Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), lakini zingeweza kuchangia kitu fulani, kwani kupungua kwake kunapunguza kasi ya kufikia uchumi wa viwanda” alisema Ngowi.

Kufungwa kwa benki hizi kumekuja ikiwaimepita miezi minane tangu kufungiwa kwa benki zingine mbili kwa sababu mbalimbali ikiwamo FBME iliyofungwa baada ya kutuhumiwa kujihusisha na utakatishaji fedha na Mamlaka za Fedha za Marekani na Mbinga Community Bank iliyowekwa  chini ya ufilisi.

Nayo Twiga Bancorp iliwekwa chini ya usimamizi na Gavana Ndulu anasema inaendelea vizuri na karibuni itarudi ulingoni na kuanza kutoa huduma baada ya kipindi cha mpito na kufanya marekebisho mwafaka.

Mwenendo

Wakati akifungua tawi la Benki ya CRDB Tawi la LAPF mjini Dodoma Rais Magufuli alionesha kutoridhika namna baadhi ya mabenki yanavyofanya shughuli zake bila kutaja majina yake na kutaka Benki Kuu ya Tanzania iyashughulikie kama sheria inavyotaka ili kuepusha hasara kwa wenye hisa na wateja wake kama hali mbaya hiyo haitarekebishwa haraka.

Hiyo inatokana na ripoti ya Shirika la Fedha la Dunia (IMF) kutoridhishwa katika ripoti yake kuwa benki nyingi ndogo ndogo na za kati  hazina mtaji unaotakiwa na sekta ya benki kwa ujumla zina madeni mengi chechefu (NPL) ambacho kiwango chake ni maradufu ya kile kiasi kinachokubalika na hivyo kutishia ustawi wa sekta ya fedha kwa ujumla.

Madeni chechefu ni yale kwa zaidi ya siku 90 wahusika wake hawajaonesha hali ya kurejesha madeni na wala kutoa melezo ya mwenendo wa madeni yao ambayo sasa  yamefikia kiwango cha asilimia 9.5 badala ya asilimia 5 inayovumilika na hali hiyo iko kwenye asilimia kubwa ya mikopo.

Mahitaji ya Mtaji

Kanuni za Sheria ya Mabenki zilizotolewa mwaka 2014 na Benki Kuu imeainisha mahitaji mbalimbali ya mitaji kwa mabenki kuwa ni Sh bilioni 15 kwa benki kamili za biashara na kwa benki za ushirika zenye mtandao wa nchi, Sh  bilioni 5 kwa benki ndogo (microfinance) na zile za ushirika zenye mtandao wa mkoa na Sh bilioni 2 kwa benki za Jumuia (Community banks). Benki nyingine zinataka mitaji mikubwa zaidi zikiwamo Benki za Maendeleo Sh bilioni 50, benki za wafanyabiashara wakubwa (merchant banks) Sh bilioni 25 na benki za Kiislamu Sh bilioni 15.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles