31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

RUTTO AKANUSHA KUSIGANA NA UHURU

NAIROBI, KENYA


NAIBU Rais William Ruto amekanusha kuwepo kwa mgawanyiko wa kisiasa kati yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Ruto ametoa kanusho hilo akiwa muda mfupi baada ya Rais Uhuru Kenyetta kutangaza la baraza jipya la mawaziri bila kuambatana na msaidizi wake huyo wa karibu.

Kukosekana kwa Ruto wakati Rais Kenyatta akitangaza baadhi ya mawaziri wapya, kulizua mjadala huku mwandishi wa habari wa gazeti la Nation, Justus Wanga akikuelezea kwa kina.

Katika mijadala mbalimbali, baadhi ya Wakenya walieleza kuwa kukosekana kwa Ruto wakati Rais Kenyatta akitangaza baadhi ya mawaziri siyo jambo la kawaida ikizingatiwa  kuwa wawili hao walilitangaza baraza hilo pamoja mwaka 2013 na wamekuwa wakionekana pamoja katika matukio karibu yote muhimu.

Akiandika katika gazeti la National, Mwandishi Wanga alieleza kuwa kukosekana kwa Ruto katika hafla ya kutangazwa kwa baadhi ya mawaziri kulionyesha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa baina yake na Rais Kenyatta na kwamba baadhi ya washirika wake wa karibu  wameachwa kando katika safu hiyo.

Aliwataja miongoni mwao kuwa ni Msimamizi Mkuu wa Ikulu, Lawrence Lenayapa ambaye nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Gavana wa Nakuru, Kinuthia Mbugua.

Ruto pia anadaiwa kutoridhishwa na uamuzi wa Rais Kenyatta la kuwapa uwaziri John Munyes, Keriako Tobiko na Ukur Yatani.

Duru za habari kutoka nchini Kenya zilieleza kuwa Ruto hakushirikishwa na Rais Kenyatta katika uteuzi huo licha ya kuwa katika ofisi yake iliyo karibu sana na Ikulu.

Hata hivyo, taarifa hizo zilikanushwana David Mugonyi ambaye ni msemaji wa Ruto aliyekaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa Ruto wake alikuwa nje wa nchi wakati Kenyatta akitangaza uteuzi huo Ijumaa iliyopita.

Pamoja na kanusho la Mugonyi, bado mijadala mingi ya Wakenya inaonyesha kuwa uamuzi wa Rais Kenyatta unaibua mgawanyiko baridi katika mrengo wa Ruto, unaodai ‘kuonewa’ na kambi ya Rais Kenyatta.

Suala la uwezekano wa kujumuishwa kwa Seneta wa Baringo Gideon Moi katika baraza hilo pia limetajwa kumweka Rais Kenyatta katika njia panda ya kisiasa.

Kwenye kampeni yake ya urais mwaka uliopita, inaelezwa Moi alikubali kumuunga mkono kwa makubaliano kwamba Kanu ingepata nafasi serikalini.

Hilo linaelezwa kumtia wasiwasi Ruto, kwani huenda Moi akageuka kikwazo cha kisiasa hasa katika udhibiti wa eneo la Bonde la Ufa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Taarifa nyingine zilionyesha kuwa Mugonyi, juzi Jumapili alimpigia simu na kumuandikia Wanga mlolongo wa ujumbe mfupi wa maneno uliojaa vitisho.

Baadhi ya maneno yaliyokuwa kwenye ujumbe huo kama yalivyokaririwa na vyombo vya habari vya Kenya ulisomeka:  “Nataka kuwa wazi kwako, ukitaka kufutwa kazi endelea na msimamo huo huo, utafutwa, utafutwa, sikudanganyi, utafutwa.”

Aidha, inadaiwa kuwa Mugonyi alimtuhumu Wanga kwa uandishi usiozingatia maadili na taaluma ya habari akidai aliandika habari ya uongo zilizomuaibisha yeye Mugonyi ambaye naye kiitaaluma ni mwandishi wa habari.

Sehemu nyingine ya ujumbe wake uliokaririwa unasomeka kuwa; “Na iwapo mtaendelea na upuuzi huu tuna njia nyingine za kuwashughulikia. Nawaonya muache njia hiyo.”

Kwenye ujumbe alioweka katika akaunti ya Twitter juzi jioni Ruto alitaja madai hayo kama uvumi usio na msingi wowote.

“Wakenya (hasa Wanajubilee) wanapaswa kujiepusha na midahalo kuhusu siasa za ugavi wa mamlaka au 2022.

Wanapaswa kuelekeza juhudi zao katika ustawishaji wa taifa. Ni jukumu la rais kikatiba kubuni kundi ambalo litamsaidia kutimiza malengo yake,” alisema Ruto.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles