25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TMAA YADHIBITI UTOROSHAJI MADINI, UKWEPAJI KODI

Na ESTHER MNYIKA,

TANZANIA ina kila aina ya utajiri. Ardhi  yake ina madini  ya dhahabu, almasi, tanzanite, makaa ya mawe, gesi na rasilimali nyingine nyingi.

Sekta ya madini imeweza kutoa ajira na uwekezaji kwenye sekta hii umeiwezesha Serikali kupata mapato kupitia kodi na leseni.

Madini ya tanzanite na dhahabu, ni kati ya madini yenye thamani na soko kubwa duniani. Kutokana na uweli huu, yamekuwa yakitoroshwa na kuipa Serikali wakati mgumu wa kuweza kudhibiti biashara hii haramu.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari wa  Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Mhandisi Yisambi Shiwa, anasema lengo la kuanzisha wakala ni kuhakikisha Serikali inapata mapato  stahiki kutokana na  shughuli za uzalishaji na biashara ya kupitia usimamizi  madhubuti na ukaguzi  makini wa shughuli za uchimbaji.

Pia anasema Wakala unahakikisha shughuli hizo zinafanya kazi  kwa kuzingitia uhifadhi  na utunzaji thabiti wa mazingira katika maeneo ya migodi .

“Pamoja na kuweka wakurugenzi katika maeneo yote yanayojishughulisha na uzalishaji na biashara ya madini  kote nchini, wakala umeweka wakaguzi maalumu katika migodi mikubwa ya dhahabu, Mgodi wa Williamson Diamond uliopo Mwadui, Shinyanga wa Madini ya Almasi, Tanzanite One uliopo Mererani na Manyara unaozalisha madini ya tanzanite,” anasema Mhandisi Shiwa.

Anasema changamoto wanayokabiliana nayo kwa sasa ni kutoroshwa kwa madini na haswa dhahabu na tazanite  kutokana na kuwa na matumizi  ya juu na thamani kubwa duniani.

Anasema katika matukio 100 ya utoroshwaji wa madini kuanzia  Julai mwaka 2012 hadi kufikia Desemba mwaka jana, madini ya dhahabu ni matukio 21 na tanzanite 19 na madini mengine.

"Madini yanayotupa shida hadi sasa ni dhahabu na tanzanite na bado kuna changamoto kubwa kwenye madini haya kutokana kuwa na thamani kubwa na yanawashawishi watu kuendelea kuyatorosha," anasema Mhandisi Shiwa.

Aidha, anasema  kuwa  jumla ya matukio  matatu ya utoroshwaji wa madini yaliripotiwa kati ya Julai na Desemba mwaka jana, ambapo madini yenye thamani ya Dola za Marekani 91,924.38  yalikamatwa na wahusika walichukuliwa hatua za kisheria.

Anasema  kupitia madawati ya ukaguzi  yaliyopo katika viwanja vya ndege nchini, Wakala kwa kushirikiana na taasisi nyingine wamekuwa wakikamata  watu wasio  waaminifu  wanaosafirisha  madini  nje ya nchi kinyume cha  sheria.

Mhandisi Shiwa anasema katika kipindi  cha Julai na Desemba, ukaguzi uliofanywa  na TMAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) uliwezesha  baadhi ya kampuni  za uchimbaji na biashara ya madini kulipa  serikalini jumla ya Sh bilioni 79.26  kama kodi ya mapato.

Alizitaja  baadhi ya kampuni  zilizolipa kodi kuwa ni pamoja na, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGM) iliyolipa Sh bilioni 45.76 na Kampuni ya North Mara Limited Sh bilioni 33.5.

Anasema katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, kiasi  cha karati 100,950 za almasi zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 24.3 ziliuzwa na kulipiwa mrabaha wa Dola za Marekani  milioni 1.2.

Mhandisi Shiwa anasema mgodi wa Tanzanite One uliuza karati 3,275 na tanzanite iliyokatwa gramu 590,057 za tanzanite ghafi na gramu 968,821 za tanzanite daraja D na E; zote zikiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 4.29.

Anasema ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwanda  uliofanywa na wakala  kwa kushirikiana na ofisi za madini  za kanda za kaskazini, mashariki, kusini, magharibi, kati, Ziwa Nyasa na Victoria uliwezesha  kupatikana kiasi cha Sh bilioni 3.8 na kulipwa serikalini kama  mrabaha stahiki katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana.

Mhandisi Shiwa anasema  kiasi hicho cha mrabaha kilitokana na uzalishaji wa jumla ya tani milioni 6.8 za madini  ya ujenzi na viwanda  vyenye thamani  ya Sh bilioni 119.5.

Anasema  ukaguzi wa uzalishaji na mauzo ya dhahabu kutoka kwa wazalishaji wanaotumia teknolojia  ya ‘vat leaching’ uliofanywa na wakala kwa kushirikiana na ofisi za madini Kanda za Ziwa Victoria Magharibi, Mashariki, Kati Magharibi, Magharibi na Kusini Magharibi umewezesha kupatikana kiasi cha Sh bilioni 2.3.

Anasema kulipwa kama mrabaha katika kipindi cha Julai na Desemba mwaka jana, malipo hayo yametokana na uzalishaji na mauzo ya jumla ya kilogramu 776.8 za dhahabu zenye thamani ya Sh biloni 58.4 katika mikoa ya Geita, Katavi, Mara, Mbeya , Mwanza, Shinyanga na Tabora.

Aidha, alitoa wito kwa wadau kuendelea kutoa ushirikiano ili sekta ya madini nchini  iendelee kuchangia katika maendeleo na uchumi wa taifa.

 

Wizi wa mali

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Biashara ya Madini kwenye migodi mikubwa, ya kati na midogo wa TMAA, Mhandisi Baraka Manyama, anasema viwanja vya ndege vilivyopo mgodini  havitumiki kutoroshea madini,  bali vina majukumu tofauti kama usafiri wa wafanyakazi  kwa sababu ratiba za mgodini ni ngumu kutumia usafiri wa kawaida wa umma (public), kwani viwanja vingi vinatumika kwa safari zao.

“Viwanja  hivi kipindi cha nyuma vilikuwa vinatumika kusafirishia mazao yanayotokana na migodi, lakini kutokana  na matatizo ya kiusalama, kama mtakumbuka tukio la Geita kutaka kuvamiwa  na kunyang’anywa dhahabu, siku hizi migodi yote haisafirishi mali zao kwa ndege sasa wanatumia helikopta  na zinaingia ndani ya migodi.

“Sisi tunajiridhisha vipi kwamba helikopta hizo na ndege hizo haziibi mali zetu? Wakala umeweka wakaguzi waliofundishwa na wako saa 24 kwenye migodi yote mikubwa, kati na midogo,” anasema Mhandisi Manyama.

Anasema kwa sasa viwanja vya ndege vinatumika kusafirisha  abiria na madini yanasafirishwa kwa helikopta.

Mhandisi Manyama anasema  kwa sasa wanaimarisha ulinzi kwa  sababu watu hao wana mbinu nyingi na kwamba ni lazima wadhibiti maeneo yote.

Rais  John Magufuli aliwahi kueleza kuwa zipo ndege  zinazoingia migodini na kutoka  na  hazina na hivyo kuzitaka mamlaka husika kuwa na usimamizi thabiti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles