33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

USIMPE MTU SAMAKI, BALI MFUNDISHE KUVUA

Na Mwandishi Wetu-DAR ES SALAAM

KUNA msemo maarufu wa Kichina usemao kuwa 'Usimpe mtu samaki, mfundishe kuvua' ili asiendelee kuomba Samaki bali aweze kuvua mwenyewe.

Usemi huu umeonekana ukitekelezwa kwa vitendo na Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation ambapo imewawezesha wanawake wa vikundi vya 2Seeds vilivyopo katika Kijiji cha Tabora wilayani Korogwe kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha na familia zao.

Kikundi hiki kilichopo chini ya mtandao wa shirika lisilo la kiserikali la 2Seeds, kinajumuisha wanawake wajasiriamali kutoka vijiji vinane vilivyopo wilayani Korogwe na Handeni mkoani Tanga.

Wanakikundi wanawake wajasiriamali mbali na kupatiwa mtaji wa kufanya biashara kama ambavyo taasisi nyingi zimekuwa  zikifanya na walengwa kuishiwa kukwama katika shughuli zao, wao wamepewa kitu cha ziada na chenye manufaa makubwa katika biashara zao ambacho ni kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali na mbinu za biashara.

Mafunzo haya ambayo yamewezeshwa na Vodacom Tanzania Foundation, yanawawezesha akina mama kujua mbinu za biashara, kuibua miradi, utunzaji wa kumbukumbu za mahesabu, usambazaji wa bidhaa zenye ubora, upanuzi wa masoko, kubadilishana uzoefu wa kibiashara na mbinu nyinginezo za biashara.

Wanawake waliopo kwenye kikundi hiki wamekuwa wakipewa fursa ya kuibua miradi yenye kuleta maendeleo endelevu kwenye jamii, ambapo miradi mitatu imekuwa ikipigiwa kura na inayoonekana ni bora zaidi kupata ufadhili wa kuiendesha. Chini ya utaratibu huu, mshindi wa kwanza amekuwa akipatiwa ufadhili kwa asilimia 100, mshindi wa pili asilimia 75 na mshindi wa tatu asilimia 50.

Mpango huu wa kushindanisha wanakikundi kuibua miradi endelevu na kupatiwa ufadhili, umewanufaisha wanawake wengi na jamii kwa ujumla  kama ambavyo baadhi ya walionufaika wanawavyotoa shuhuda za mafanikio yao katika Makala hii.

Rehema Jambia, Mkazi wa Kijiji cha Bungu kilichopo katika milima ya Usambara, ni mwanachama wa kikundi cha Neema2Seeds  na alinufaika kwa kupata ufadhili wa asilimia 100 kuendesha mradi wa ng’ombe wa maziwa.

Mjasiriamali huyo aliweza kununua ng’ombe wa maziwa ambaye alimpatia jina la ‘Mkombozi’ kutokana na kuchangia kukuza pato la familia yake. katika kikao cha wanawake kilichofanyika hivi karibuni, mama Jambia aliahidi kutoa ndama atakayezaliwa na ng’ombe wake kwa mwanakikundi mwingine ili mradi uzidi kukua, kuwa endelevu na kuleta mabadiliko kwa jamii.

Kwa upande wake, mwanakikundi mwingine, Rose Kimweli, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Wakulima Lutindi na Mwanachama wa kikundi cha 2Seeds, anasimulia kuwa amenufaika kwa kupata ufadhili wa asilimia 75 kupitia mradi wake wa ushonaji nguo ambao alikuwa amekwama kuuendesha kutokana na changamoto mbalimbali.

Anasema baada ya kununua cherahani mpya, alianza kazi ya ushonaji nguo na alimfundisha binti yake kazi ya ushonaji. Ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, anasema aliweza kupata kazi za kushona sare za shule na kipato cha familia yake kiliongezeka ambapo aliweza kujiwekea akiba na kuweza kununua cherahani ya pili inayotumiwa na binti yake anayefanyia shughuli zake mjini Tanga.

Naye Frida Madege kutoka Kijiji cha Lutindi, ambaye anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, anasema kuwa kutokana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, aliamua kuanzisha biashara ya duka la rejareja katika Kitongoji cha Kana na mradi wa ukodishaji wa viti na meza wakati wa matukio mbalimbali kitongojini hapo, alibahatika kupata ufadhili wa asilimia 50  katika uanzishaji wa mradi huu, akanunua jokofu la kupoza vinywaji na viti 100, hivi sasa biashara yake inamwezesha kupata kipato cha kuendesha na kufidia kipato alichokuwa anakipata kutokana na kilimo ambacho kimekuwa hakiendi vizuri.

Lydia Masabo, Mkazi wa Kijiji cha Tabora, naye ni mmoja wa washindi wa ruzuku hizi za kujikwamua katika mzunguko wa pili, aliibua mradi wa kuuza mbogamboga na bidhaa nyingine ndogondogo za matumizi ya kila siku ambao ataanza kuutekeleza katika siku za karibuni, akiwa na matumaini kuwa utaweza kumuongezea kipato.

Naye Aziza Yahya, Mjasiriamali na mama mwenye watoto watatu, ni mmoja wa wanawake walionufaika na mpango huu kwa kukuza biashara yake ambapo awali alikuwa akiuza nguo na vipodozi kijijini Handeni, hivi sasa amejenga duka la kisasa la kuuza nguo na amefungua saluni ya kisasa ya kutengeneza nywele, biashara yake imekua na anajipatia wateja wengi wanawake kutoka sehemu mbalimbali za Mkoa wa Tanga.

Miriam Mdoe ni mkazi wa Kitongoji cha Kuga kilichopo katika milima ya Usambara, eneo ambalo kwa kiasi kikubwa liko mbali na maeneo ya kupata huduma za mahitaji mbalimbali kwa urahisi.

Kwa kipindi kirefu anasimulia kuwa amekuwa akifanya biashara ya maandazi na kuuza chai kwa wananchi waliokuwa wakienda mashambani kwao. Ameweza kunufaika kwa ufadhili wa asilimia 25 kwa ajili ya kuanzisha mgahawa mdogo wa kisasa kitongojini hapo ambao anaamini utakuza kipato chake na kutoa huduma bora kwa wateja wake.

Mwanamke mwingine, Aziza Abdallah, mkazi wa Kijiji cha Bungu, naye kwa muda mrefu alikuwa na ndoto ya kuendesha biashara na amefanikiwa kuibua mradi wa kuuza mbogamboga, bidhaa ndogondogo za matumizi ya nyumbani na mafuta ya taa.

“Nimefanikiwa kupata ufadhili wa asilimia 50 na yuko mbioni kuanzisha duka kwa ajili ya kujiongezea kipato,” anasema.

Pamoja na hali hiyo, kwa upande wa Tabora Women’s Group  ambao ni mtandao wa kikundi cha wanawake wajasiriamali wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula vilivyofungwa kwenye vifungashio maalumu kwa ajili ya kuviuza mjini Korogwe na jijini Dar es Salaam, wao wamefanikiwa kuongoza vizuri katika uzalishaji kwa kutafuta fursa za masoko.

Katika kipindi cha mwaka jana, biashara yao imeweza kuongoza kufanya vizuri katika vikundi vya  2 Seeds  kwa kufikia mapato ya zaidi ya Sh milioni 15 mwaka jana licha ya changamoto mbalimbali,  mojawapo kubwa ikiwa ni ugumu wa kupata masoko ya uhakika wa bidhaa zao.

Katika mikakati ya kusonga mbele zaidi, kikundi hiki kimeazimia kupanua mtandao wa masoko yake kwa bidhaa mbalimbali kinachouza, ikiwemo matunda yaliyokaushwa kwa jua na vinywaji  vya matunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles