25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAWAKATISHA TAMAA WABUNIFU UJENZI WA VIWANDA

Na Gordon Kalulunga,

WAKATI nia ya kuwa nchi ya viwanda ikiwa tayari imetangazwa na Rais John Magufuli, Novemba 20, mwaka 2015, Serikali inadaiwa kuwakatisha tamaa wabunifu wasio wasomi kuendeleza viwanda vidogo.

Pamoja na kuwepo kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ambayo moja ya majukumu yake ni kutafuta, kutunza na kusambaza taarifa za sayansi na teknolojia na kuzikuza nchini, bado jitihada za utekelezwaji wa majukumu ya tume hiyo ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hazijaonekana kwa wabunifu hao ambao wengi wao hawana elimu
za vyuo vikuu.

Hivi karibuni, Mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, Adam Kinyekile (34), kwa mara ya kwanza ametengeneza Helikopta nchini Tanzania lakini amekatazwa na Serikali kuendelea kutengeneza Helikopita hiyo.

Katazo hilo ambalo liliwalenga wabunifu wote wa Helikopta au ndege hapa nchini bila kutaja majina, lilikuja baada ya kijana huyo kuonyesha ubunifu wake na baada ya katazo hilo kupitia taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania  ya Julai 2016.

Kinyekile ambaye ni fundi magari, alitumia ubunifu wake kutengeneza helikopta ambayo ilimvutia kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, GeorgeMbijima, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka huu 2016.

Hata hivyo, baada ya taarifa za kijana huyo kutangazwa kwenye vyombo vya habari, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilipiga marufuku mtu yeyote kujihusisha na ubunifu au utengenezaji wa ndege ya aina yoyote ile bila kufuata utaratibu maalumu. 

Onyo hilo lilionekana kumlenga Kinyekile ambaye alisitisha kuendelea na maboresho ya helikopta hiyo, licha ya kudai kwamba ilikuwa imebaki kurushwa tu.

Pamoja na Serikali kupiga marufuku wabunifu kutoendelea na kazi zao za ubunifu, baadhi ya wahunzi wanaoishi mikoa ya Mbeya na Rukwa amemtaka Rais Magufuli kuwapatia mtaji ili kuwawezesha kufikia malengo ya uanzishwaji wa viwanda.

Wakiwa katika mahojiano na mwandishi wa makala haya, wamesema ili taifa lifikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, wanamuomba rais Magufuli kuwapunguzia kero wazipatazo kutoka katika taasisi za Serikali.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalumu, wanasema walimwambia rais kuwa kwa vile maendeleo ya nchi yanaletwa na wananchi wenyewe, wana uhakika wakipatiwa miradi wana uwezo wa kutengeneza vifaa vingi ambavyo vinaagizwa nje kwa kutumia fedha nyingi za kigeni.

Mkurugenzi wa Kiwanda cha Tekumwenzo Blacksmith kilichopo Sumbawanga mkoani Rukwa, kinachotengeneza vifaa vya kilimo kama mashoka  anayotengenezwa kutokana na Springi za magari, Renatus Chasuka, anasema Serikali inapaswa kutafuta jinsi ya kuboresha kazi zao badala ya  uwauliza elimu za vyeti.

“Mungu kaweka vitu vingi katika maghala, yaani vichwani mwa kila binadamu. Wengine ametuwekea ubunifu ingawa hatuna elimu za darasani. Serikali inapaswa ituulize tunawezaje kuboresha bidhaa zetu na kuziuza ndani na nje ya nchi kama wafanyavyo Wachina,” anasema mbunifu huyo.

Amedai kuwa Serikali haiwathamini wabunifu wa ndani kwa sababu tu hawana vyeti vya vyuo, wakati wenye vyeti wengi hawana ubunifu wa kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa viwanda, maana unategemea ukuaji wa viwanda vidogo.

“Mungu aliwatumia Malaika kwenda kuwaonya na kuwaambia wafalme mambo yajayo, nasi tukitumika na kuthaminika kama Malaika hata kama hatuna elimu, tutatoa mchango mkubwa kufikia malengo ya viwanda nchini,” anasema.

Anaeleza kwamba mashoka anayotengeneza pamoja na majembe ya mkono anayauza kwa wenye maduka ya vifaa vya ujenzi katika mikoa mbalimbali
hapa nchini kwa kuwa bidhaa zake hazijathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Naye Olika Loti Mwaya, Mkazi wa Madabaga mkoani Mbeya, ambaye anajishughulisha na utengenezaji wa mashine mbalimbali za kupepeta mpunga, anasema yeye hajawahi kukutana na viongozi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Anasema ameanza ubunifu muda mrefu huku akitumia baiskeli kufunga mashine ndogo. Anaongeza kuwa mwaka 2015, alianza uzalishaji wa mashine kubwa zenye uwezo wa kupepeta mpunga kwa saa 6 bila kusimama, huku akitumia mota ambayo inatumia mafuta ya petroli lita moja tu kwa muda huo.

“Hadi sasa mimi na baadhi ya wabunifu wenzangu wilayani Mbarali, tumeamua kuunda kikundi kiitwacho Safi Group, baada ya vifaa tulivyobuni kuungwa mkono na Shirika la Kimataifa la Land ‘O’ Lakes.

Katika kikundi hiki, mimi ni Katibu na hivi ninavyozungumza mwenyekiti wetu kapelekwa nchini Kenya,” anasema.

Pamoja na kukiri kuwa hawajawahi kutembelewa wala kuonana na TBS, anakiri kulisikia shirika hilo la viwango na kwamba wanapanga kuonana nao.

Hata hivyo, Katibu huyo anasema anafurahia mafanikio waliyoyapata kutokana na ubunifu wa utengenezaji wa mitambo ya kupepeta mpunga na
mahindi. Amedai kwamba tayari wamepewa kazi na Shirika la Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kuwatengenezea mashine 86 kwa gharama ya Sh 1, 600,000 kwa kila moja.

Elison Pashira (50), Mkazi wa Kijiji cha Utengule, Jimbo la Mbeya Vijijini, ni mbunifu wa mashine ya kukamulia juisi inayotokana na malighafi inazopatikana nchini yakiwemo machungwa, nyanya, miwa, maparachichi na mananasi. Kama wengine, mkazi huyo anasema hajawahi kuwaona maofisa wa TBS kuangalia bidhaa zao.

Anasema kabla ya kuunda kikundi cha wajasiriamali wabunifu katika eneo lao, walikuwa wakitengeneza mashine za namna hiyo kwa mfumo wa ndoo ya lita ishirini kwa ajili ya kukamua matunda ya juisi na baadaye wakaunda kikundi kiitwacho Uteite Group na kuanza kutengeneza mashine kubwa kwa ufadhili wa Shirika la Land O’Lakes ambazo wanaziuza kwa Sh laki saba kila moja.

Mmoja wa wanakikundi hicho cha wabunifu, Sarah Mwanyembe (50), anasema furaha yao kubwa ni kwamba pamoja na kikundi chao kuwa ni cha watu wazima, lakini kwa sasa wanatoa mafunzo kwa vijana ili kuwarithisha  maarifa yao.

“Tanzania tunaweza kufikia azma ya kuwa na viwanda lakini lazima tuthamini viwanda vidogo vya wabunifu,” anasema Sarah.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda kisicho rasmi cha Ngoley Extension cha jijini Mbeya, Charles Antony Sanga ambaye anajishugulisha na utengenezaji wa Extension Cable za umeme kwa kutumia waya kubwa na mbao, anasema wabunifu hawana mitaji zaidi ya akili angavu, lakini masharti ya uendelezaji vipaji vyao kufikia uchumi wa viwanda ni magumu mno.

Anaeleza kuwa ili mbunifu aweze kutambulika na Serikali, kuna vipingamizi vingi kutoka katika taasisi za Serikali ikiwemo kupewa leseni za biashara.

“Kwa mfano, changamoto ninazokabiliwa nazo kwenye karakana yangu ni ukosefu wa mtaji, hivyo nachonga mbao ili kuweka njia za umeme kwa kutumia kisu cha kawaida, nikitumia mkono natoboa matundu, nakata mbao na kuranda,” alisema Sanga.

Anasema amewahi kwenda katika ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya akiomba msaada zaidi na kuwaeleza kuwa yeye ni
mbunifu, jibu ambalo alilipata ni kwamba kwa sasa Serikali haina chochote cha kumsaidia na alitakiwa akasome kwa gharama zake.

“Serikali wakitaka kunisomesha nipo tayari, lakini jiji walisema hawana mfuko wa kusomesha wabunifu na TBS nilipokwenda walinitaka niwe na kiwanda, jambo ambalo nimefanikiwa kununua uwanja na kujenga nyumba yangu na ofisi na walinitaka nijenge sehemu ya mapokezi, ofisi, karakana, stoo na vyoo.

“Rais Magufuli  hana shida lakini baadhi ya watendaji wake ni siasa tupu.

Mimi nimethibitishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia lakini anakuja mhandisi  wa jiji ananiambia kuwa nisitishe uzalishaji na kwamba nimpe
kifaa akapime, kisha niende kusoma na baadaye nikaombe kibali kwao cha kuendeleza ubunifu wangu, yaani kutengeneza hizi nyaya za umeme,”
anaeleza huku akitikisa kichwa.

Kwa sasa anaeleza kuwa tayari ameajiri wafanyakazi wanne na bidhaa zake zinasambazwa katika maduka ya vifaa vya ujenzi na anauza kuanzia Sh 5,000 kwa kifaa kimoja.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles