24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ofisi za CUF zachomwa moto Z’bar

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

HALI ya kisiasa visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete huku siasa za visasi, chuki na uhasama zikionekana kurejea kwa kasi.

Hali hiyo imejitokeza baada ya ofisi za matawi matano ya Chama cha Wananchi (CUF) zilizopo Pemba na moja  Unguja kuchomwa moto na watu wasiojulikana.

Matukio ya kuchomwa moto kwa ofisi hizo yamekuja siku mbili baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge iliyopo mjini Unguja.

Hata hivyo Jeshi la Polisi visiwani humo limetangaza kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu waliohusika na matukio hayo.

Uchomaji huo ulifanyika usiku wa kuamkia jana saa 8 usiku, ambapo watu hao walichoma moto na kuteketeza nyaraka za chama hicho.

Matawi yaliyochomwa moto ni Kilimahewa mjini Unguja Wilaya ya Magharibi, Mkanyageni, Kiwapwa, Kiuyu Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani Pemba.

Kutokana na tukio hilo MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, ambaye alithibitisha kutokeo kwa matukio hayo.

Alisema kutokana na hali hiyo tayari ameagiza askari wake kuanza uchunguzi wa tukio hilo haraka ili waliohusika watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Ni kweli kuna hilo tukio ingawa kwa sasa nipo safari kuelekea Unguja na tayari nimeagiza kuanza kwa uchunguzi wa matukio haya ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“…siwezi kusema kama matukio haya yana uhusiano wa masuala ya kisiasa ingawa huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine,” alisema Kamanda Nassir.

Mbunge awa mbogo

Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF), alilaani tukio hilo huku akiwatuhumu wafuasi wa CCM kuhusika nalo.

Alisema hatua ya CUF kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu imekuwa ikiwaumiza CCM.

“Haya mambo yapo wazi tumeumizwa vya kutosha lakini katika hilo mimi binafsi wala sifichi hapa kuna mkono wa CCM  na sisi hatutarudi nyuma tunaendelea na msimamo wa chama,” alisema Hamad.

Maalim Seif na jino kwa jino

Machi 4, mwaka huu, Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani kwake, Katibu Mkuu wa CUF,  Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yuko tayari kukamatwa kutokana na msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio.

“Musidhani kuwa mtatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila mara tunaibiwa, tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu wajilinde, inakuwa nongwa.

“…basi tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa ndani, kufunguliwa mashtaka ya bandia, hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa yakitutokea tangu 1992 tumeshayazoea,” alisema Maalim Seif.

Alisema udhalilishwaji kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chama chake, zaidi ya kukiongezea umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku akilituhumu Jeshi la Polisi kwa kuwa ‘tawi la CCM’ ambalo litakuwa dhamana wa machafuko yoyote yatakayotokea.

Katika hatua nyengine, Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana  alirudia msimamo wa chama chake wa kutoshiriki kile alichodai uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, Machi 20, mwaka huu.

Alisema yeye alishashiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine. “Ninamwambia Jecha kuwa uchaguzi huo ni wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif.

Juzi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, aliwataka wapenzi wa CCM kuwa na subira kutokana na vitendo vya kichokozi vinavyofanywa na baadhi ya watu dhidi yao na mali za chama hicho.

Makamu mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, alisema hayo baada ya kutembelea maskani ya Mwembe Kisonge, iliyopo Michenzani mjini Unguja ambayo ililipuliwa kwa bomu mwishoni mwa wiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles