24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ODINGA AWATAKA WAFUASI WAKE WASIENDE KAZINI LEO

NAIROBI, KENYA

KIONGOZI wa muungano mkuu wa upinzani wa National Super Alliance nchini Kenya (NASA), Raila Odinga amewataka wafuasi wake wasiende kazini leo.

Vilevile , Odinga kesho anatarajia kutangaza hatua ambazo muungano wao utachukua   baada ya kutosikilizwa  madai yao kuwa ameporwa ushindi wa urais katika uchaguzi mkuu mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Uamuzi huo aliutangaza   Nairobi jana, alipozungumza na wafuasi wake wa kitongoji wa Kibera.

Alisema pamoja na matokeo yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo,   bado hajakata tamaa na harakati za mageuzi.

“Tulitabiri wataiba kura katika uchaguzi ule wa Jumanne iliyopita na hilo ndilo lililotokea. Na bado hatutakata tamaa katika harakati zetu.

“Subirini kitakachofuata ambacho nitakitangaza keshokutwa (kesho). Lakini kwa sasa ninachotaka kuwaambia ni kwamba msiende kazini kesho (leo),” aliuambia umati wa wafuasi wake katika kitongoji kikubwa  cha Nairobi cha Kibera.

Wakati kiongozi huyo akihutubia wakazi wa Kibera, baadhi walikuwa wamepanda juu ya paa za nyumba na miti  waweze kumwona.

Odinga  alikuwa akizungumza kwa mara ya kwanza tangu mpinzani wake Rais Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee atangazwe mshindi katika uchaguzi wa urais ambao Odinga anadai ulichakachuliwa.

Uamuzi wake huo ulisababisha maandamano ya kupinga matokeo katika ngome za Odinga magharibi mwa Kenya na vitongoji vya Nairobi vikiwamo Kibera na Mathare, ambayo yalisababisha vifo vya watu 16.

“Utawala huu ulioshindwa unachagua kuua watu badala ya kushughulikia tatizo halisi. Kura ziliibwa. Hakuna siri kuhusu hili.

“Njama za kuua wafuasi wa NASA walizipanga hata kabla ya uchaguzi,” alisema.

Alitoa kauli hiyo baada ya jumuiya ya kimataifa   na wengine nchini humo kumtaka awatulize wafuasi wake.

Hiyo ni siku moja baada wa watu kadhaa kuripotiwa kuuawa maeneo tofauti ya miji ya Nairobi na Kisumu  wakati wafuasi wa upinzani walipojitokeza kulalamikia matokeo hayo.

Idadi ya watu 16 walioelezwa kuuawa ni kama ifuatavyo:  Watu wanane   Nairobi, wanne Kisumu, wawili Siaya, mmoja Migori na mwingine Homabay.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa, Fred Matiang’I, alikanusha polisi kuwapiga risasi watu waliokuwa wanaandamana kwa utulivu bali alisema watu hao walikuwa wahalifu.

Jeshi la Polisi la Kenya pia lilikanusha ripoti iliyotolewa na Shirika la Taifa la Kutetea Haki za Binadamu nchini humo kwamba maofisa wa polisi wamewaua watu 24 katika vurugu za uchaguzi.

Kwa sasa maeneo mengi yaliyokumbwa na vurugu yamerejea katika utulivu huku viongozi wa dini wakiendelea kuwahamasisha waumini wao wadumishe amani.

Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kura 8,203,290 huku Odinga akipata kura 6,762,224.

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa siasa  Kenya miaka 10 iliyopita, ametoa wito kwa Odinga kutumia mifumo ya sheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais.

“Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia,” alisema Dk. Annan kupitia taarifa.

“Kwa hivyo namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya  sheria iliyowekwa na aweke maslahi ya taifa mbele  kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara”.

Mwaka 2007  watu zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine 600,000 kukosa makazi wakati wa ghasia za ukabila zilizozuka baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi yenye utata.

MWISHO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles