28.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

TANZANITE YA MABILIONI YATOROSHWA

*Ukiukwaji wa Sheria ya Madini 2010, minada, kodi, vyatajwa

Na MASYAGA MATINYI -MANYARA

MADINI ya vito yenye thamani kubwa yanayopatikana Tanzania pekee, Tanzanite, yamekuwa yakitoroshwa nchini kwa njia za panya na minada na kulikosesha Taifa mabilioni ya shilingi.

Kutokana na utoroshwaji huo, Tanzania imejikuta ikiwa nyuma ya mataifa ya India na Kenya, ambayo ndiyo yanaongoza duniani kwa usafirishaji wa Tanzanite.

Marekani ndio soko kubwa la madini hayo ambayo huuzwa nchini humo yakiwa tayari yamekatwa na kusanifiwa.

Madini yanayotoroshwa kwa njia za magendo na minada kutoka Tanzania, ni ghafi kinyume cha maelekezo ya Serikali yaliyotolewa Desemba 2010, ambayo yalitamka bayana kuwa hairuhusiwi kuuza Tanzanite ghafi zaidi ya gramu moja kwenda nje.

Hatua ya Serikali kupiga marufuku uuzwaji wa madini ghafi nje, ilikuwa na lengo la kuyaongezea thamani (kuyakata na kuyasanifu), hivyo kuliingizia fedha zaidi za kigeni taifa na kutoa ajira kwa Watanzania.

Katika nchi ya India ambayo inaongoza duniani kwa kuuzwa madini ghafi kutoka Mererani mkoani Manyara yalipo machimbo ya tanzanite, viwanda vya kukata na kusanifu madini hayo vimeajiri watu kati ya 200,000 hadi 300,000 katika mji maarufu kwa biashara ya vito wa Jaipur.

Minada mikubwa ya tanzanite hufanywa na Kampuni ya Tanzanite One Ltd, ambayo ni wawekezaji wenye ubia na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Mwaka huu pekee imefanyika minada mikubwa miwili jijini Arusha. Mnada wa kwanza ulifanyika Februari 9 hadi 12 na wa pili ulifanyika Mei 3 hadi 18. Zaidi ya Dola za Marekani milioni 8 zilipatikana.

Kampuni zilizoshinda zabuni na kununua tanzanite ghafi ni kutoka Jaipur, India, Hong Kong, Thailand na kampuni moja tu ya Tanzania iitwayo M/S Tomgems.

Mojawapo ya kampuni iliyoshinda zabuni nyingi kwenye minada hiyo ni M/S Vaibhav Global Limited ya Jaipur, India, ambayo inatajwa kuwa na uhusiano na mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates Group Limited, ambayo ndiyo mmiliki wa Tanzanite One Limited.

UTOROSHAJI KUPITIA MINADA

Chanzo cha habari cha kuaminika (jina tunalihifadhi) kimesema kuwa utoroshaji wa madini kupitia minada unafanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa Serikali wasiokuwa waaminifu wanaohusika na madini kwa kushirikiana na wauzaji na wanunuzi.

“Kimsingi ile minada sawa ni minada, lakini kwa kiasi fulani ni kiini macho. Mawe (tanzanite) yanayopelekwa mnadani mengi si yenye ubora.

“Sasa utakuta pale mnadani thamani yake inakuwa chini kutokana na ubora hafifu, na baada ya mnunuzi kununua, ufuatiliaji wa Serikali kabla mzigo haujasafirishwa nje si makini, kwa sababu kabla mzigo kusafirishwa inachukua siku kadhaa.

“Kwa hiyo kwa kutumia mwanya huo, madini ghafi yasiyokuwa na ubora yaliyonunuliwa mnadani hubadilishwa na kuwekwa madini ghafi yenye ubora na wahusika kupata fedha nyingi yanapokwenda sokoni.

“Kwa kiasi kikubwa tanzanite inayoonekana mnadani si ile inayosafirishwa kwenda India na kwingineko, kwa kweli usimamizi wa Serikali inabidi utazamwe upya kuanzia kwenye uzalishaji mgodini hadi mzigo unapotoka nje ya nchi. Kuna udanganyifu mwingi sana.

“Pia tunaiomba Serikali kupitia vyombo vyake kama Takukuru viwachunguze maofisa wa Serikali waliowahi kufanya kazi Mererani na waliopo, hasa kuhusu fedha, mali na vitegauchumi kadha wa kadha wanavyomiliki, wana ukwasi wa kutisha,” kilisema chanzo chetu.

Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa wakurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates Group Limited, Faisal Shahbhai, alisema madai dhidi ya minada mikubwa ya tanzanite hayana msingi wowote, kwa sababu taratibu zote hufuatwa, ikiwa ni pamoja na maofisa wa Serikali kuhusishwa katika hatua zote.

Kuhusu uuzaji wa madini ghafi kinyume cha maelekezo ya Serikali, alisema wanalazimika kuyauza kwa sababu hakuna viwanda wala utaalamu wa kutosha kuweza kuyakata na kuyasanifu.

“Kwa kiasi cha madini yanayopatikana pale Mererani, kisha tusema yasiuzwe nje ya nchi yakiwa ghafi, ni sawa na kuchukua gunia mbili za mchele, kisha umchukue mtu mmoja na kumfungia kwenye chumba na gunia hizo, kisha umwambie unaondoka na baada ya siku mbili ukirudi ukute ameusaga mchele wote gunia mbili kwa kutumia meno. Ni jambo haliwezekani hata kidogo.

“Sawa sisi ni wawekezaji, hatupingani na Serikali, lakini ikumbukwe tunafanya biashara, gharama za kuendesha mgodi ni kubwa sana, sasa hatuwezi kuchimba madini na kuyaweka stoo, lazima tuyauze ili tuendelee mbele, siku kukiwa na ‘facilities’ husika na wataalamu wa kutosha, basi biashara ya madini ghafi itakufa yenyewe,” alisema.

UTOROSHAJI NA MILOLONGO YA KODI

Utoroshaji wa tanzanite kwa kiasi kikubwa unawagusa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara (dealers) wasiokuwa waaminifu, na uchangiwa kwa kiasi kikubwa na mlolongo wa kodi, hasa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambayo wageni wanapokuja kununua madini hawalipi, lakini mzawa anatakiwa kulipa.

Kuna jumla ya kodi 13 ukiondoa VAT, ambazo wafanyabiashara wa madini ya vito wanalipa, jambo linalochangia kwa kiasi kikubwa baadhi yao kufanya biashara nje ya utaratibu uliopo.

Kodi hizo ni Pay roll levy 6%, NSSF 10%, SDL 6%, House levy, Director’s fees, mrabaha 1% – kwa madini yaliyokatwa, mrabaha 5% kwa madini ghafi, leseni uchimbaji (PML) hadi Sh 800,000, leseni ya biashara madini ya vito dola za Marekani 1,000 (Kenya dola za Marekani 200), tozo zinazokusanywa na Serikali za Mitaa 0.3%, (Kenya 0%), Corporate tax 30% na kodi zinazotozwa na mamlaka za miji, Sh 3,000.

Akizungumzia kuhusu wingi wa kodi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kwamba tayari wamewasilisha malalamiko yao serikalini.

Mollel alisema: “Kumekuwepo na kodi lukuki zinazowaandama wafanyabiashara halali wa madini na hivyo kuwa mzigo, mzigo huo umekuwa ni pingamizi kwetu kushindana na walanguzi wa vito. Kodi (zilizotajwa hapo juu) ni mzigo, hasa kwa VAT ambayo ni asilimia 18.

“Tunaishauri Serikali kwamba kodi zipunguzwe au ziangaliwe upya na kufanyiwa marekebisho, na vile vile utaratibu ufanyike zilipwe sehemu moja kuliko kodi hizi lukuki zilipwe sehemu tofauti tofauti.

“Kwa mfano ni vyema zilipwe kwenye mirabaha ili kuweza kuboresha mazingira bora ya biashara na hivyo kustawisha uchumi imara katika sekta ndogo ya uchimbaji na biashara ya madini.

“Aidha kodi zote na ushuru ambazo haziko chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati na Madini ziondolewe.

“Ni rai ya wafanyabiashara ya madini kuwa uwepo wa kodi hizi ni mzigo, hasa VAT asilimia 18 iondolewe moja kwa moja, kwani inadhoofisha sekta nzima ya madini ya vito, na hivyo kusababisha wafanyabiashara wengi wa madini kutomudu biashara hiyo.

“Wengi hawana mitaji ya kutosha na kuwafaidisha hasa wanunuzi wa nchi za nje kwani wao ndio walaji ambao kodi ya VAT 18% haiwagusi katika kusafirisha madini nje.

“Asilimia 99 ya vito vinasafirishwa nje ya nchi, na ni ukweli usiopingika kwamba walaji wako nje ya nchi, kwa hiyo VAT haiwagusi.

“Aidha sheria ya kodi iweke bayana kuwa madini yanayosafirishwa nje ya nchi hayatozwi VAT,” alisema.

Mollel alisema utoroshwaji wa madini pia unaongezeka kwani wachimbaji na wafanyabiashara wasio waaminifu hutumia njia za panya kutorosha madini ili kukwepa VAT.

Akizungumzia utoroshwaji wa madini jijini Arusha wiki iliyopita, Kamishna wa Madini, Benjamin Mchampaka, aliliambia na MTANZANIA kuwa tatizo hilo haliwezi kukosekana, lakini Serikali inaendelea kuchukua hatua kadha wa kadha kulidhibiti.

Mchampaka alisema miongoni mwa hatua hizo ni kuongeza maofisa wake katika maeneo yote, ili kuweka usimamizi na kuhakikisha hakuna utoroshaji unaofanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles