23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

NG’OMBE HUSHINDWA KUZAA ANAPOLAZWA ZIZI MOJA NA PUNDA

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


IPO misemo ya wahenga inayosema; ‘Punda haendi bila mjeledi. ‘Shukrani ya punda ni mateke.’ Misemo hii imetumiwa kumwelezea punda kama mnyama mbishi na asiye na fadhila.

Punda ni mnyama anayefugwa na binadamu ili kubeba mizigo hasa maeneo yenye matatizo ya usafiri na miundombinu mibovu ya barabara, anatajwa kuwa na faida nyingi kuliko misemo ya wahenga inayomtambulisha.

Katika makala haya, MTANZNAIA limefanya mahojiano na Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la Serikali ‘The Arusha Society Protection of Animals (ASPA), Livingstone Masija, kujua maisha na umuhimu wa punda katika jamii yetu.

ASPS inajishughulisha na utoaji wa huduma kwa wananchi wa Arusha katika tasnia ya ufugaji na kuiunganisha jamii katika kusimamia sheria ya ustawi wa wanyama tangu mwaka 1997.

Masija anamwelezea punda kuwa ni mnyama aliyetumika kwa miaka mingi kubeba mizigo, kwani tangu kale mnyama huyo alikuwa akifanyishwa kazi.

Anasema mnyama huyu ameumbwa na uvumilivu wa magonjwa na dhoruba mbalimbali zinazomzunguka na endapo atatunzwa vizuri basi huweza kuishi takribani miaka 40.

Anaiomba jamii hususani watu wanaowatumia punda kwa shughuli za maendeleo na kiuchumi kuacha kuwafanyia mambo yasiyofaa kwa kuwa ni tegemeo kwa binadamu.

Anayataja baadhi ya mambo yasiyofaa kumfanyia punda kuwa ni pamoja na kumkimbiza anapokuwa akifanya kazi hasa akiwa na mzigo mgongoni au kukokota mkokoteni wenye mzigo.

“Unapomkimbiza unaweza kumsababishia kuanguka na kumpa majeraha hivyo atashindwa kufanya kazi ya kukuingizia kipato. Lakini pia anaweza kugongwa na gari akafa.

“Jingine ambalo jamii inayotumia punda kama nguvu kazi inapaswa kutambua mnyama huyu hapaswi kufanyishwa kazi anapokuwa na mimba. Kama ilivyo kwa binadamu anapofanyishwa kazi ndivyo ilivyo kwa punda.

“Unapomfanyisha kazi akiwa na mimba kubwa uwezekano wa kutoka na kumsababishia madhara mengine ikiwamo kifo yeye na mtoto aliyetumboni ni mkubwa.

“Lakini pia hatakiwi kuchapwa fimbo kama njia elekezi, hili limekuwa tatizo kubwa kwa watumiaji wa wanyama hao, hali inayowasababishia majeraha mwilini,” anasema Masija.

Masija anaweka wazi kuhusu mijeledi kwa mnyama huyo, akisema huwa inamsababishia ukorofi na sugu ikiwamo ulemavu na kifo.

Anasema jamii inayotumia wanyama hao kama sehemu ya nguvu kazi inapaswa kuacha kuwafanyisha kazi wakiwa wagonjwa kwani huwasababishia kushindwa kuzifanya kwa kiwango kikubwa hivyo kumjengea ukorofi.

“Kuna vitendo si vya kiungwana kabisa anavyofanyiwa punda, unaweza kukuta ana vidonda mgongoni na mtu akamuweka mzigo eneo hilo. Niiombe jamii ijitahidi kuwapenda punda kama walivyo wema kwao,” anasema Masija.

Anasema endapo hatafanyishwa kazi kutwa nzima hujikuta anakuwa mzembe. Anashauri wanyama haowasihifadhiwe sehemu moja na majike ya ng’ombe kwa kuwa husababisha ng’ombe kutozaa.

Anasema punda anastahimili hali ya hewa yoyote iwe kwenye maeneo makavu, joto au milima huku akimudu kupita kwenye miteremko mikali, njia nyembamba za miguu, bonde la mto lenye mawe, njia zenye matope na sehemu zilizo ngumu kupitika.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles