29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

URITHI WA KIHISTORIA ULIOACHWA KILWA KISIWANI

Na NORA DAMIAN-ALIYEKUWA LINDI


HIVI majuzi nilibahatika kufika katika Mji wa Kilwa Kisiwani ulioko mkoani Lindi ambao ni miongoni mwa miji iliyobeba historia ya Bara la Afrika.

Kutoka Mji wa Kilwa Masoko hadi kufika Kilwa Kisiwani ni mwendo wa dakika 15 hadi 20 kwa kutumia boti iendayo kasi.

Wanaikolojia wanakadiria kwamba mji huo ulikuwapo kuanzia karne ya nane.

Uhalisia, uhalali na historia yake ndivyo vinafanya mji huo kuwa na umuhimu wa kipekee kwani kila jamii iliyoishi eneo hilo imeacha aina fulani ya kumbukumbu.

 

MAJENGO MUHIMU

Katika mji huo kuna majengo kadhaa yaliyoacha historia kubwa duniani ambayo hivi sasa yamebaki kama makumbusho.

Kuna eneo la makutano lililoanza kujengwa karne ya 15, msikiti wa Malindi, msikiti mdogo, nyumba ya Sultani, msikiti mkuu uliokuwa ukitumiwa na Washirazi, msikiti wa jangwani, makaburi ya masultani, makaburi ya mashehe 40 na katika kila msikiti kuna kisima.

Miongoni mwa majengo yaliyopo eneo hilo ni msikiti ambao unakadiriwa kujengwa karne ya 11.

“Huu ni msikiti mkubwa zaidi kuwahi kujengwa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ulijengwa katika karne ya 11 na ndio msikiti wenye sifa ya kipekee,” anasema Mkuu wa Kituo cha Mambo ya Kale Kilwa, Revocatus Bugumba.

Anasema msikiti huo umegawanyika mara mbili kwa sababu katika karne ya 13 uliongezwa mwingine.

Ndani ya msikiti huo kuna chumba maalumu kilichokuwa kikitumiwa na Sultani kuswalia ambacho kimenakishiwa kwa mapambo sehemu ya juu.

Pia kuna msikiti mdogo uliokuwa umejengwa kando ya bahari ambao ndani yake ulikuwa na kisima kilichotumika kuchota maji ya kutawazia, mawe maalumu ya kufutia miguu na ukumbi wa kuswalia.

Pembeni ya msikiti huo kulikuwa na makaburi ambayo yalitumiwa na watu waliokuwa wakiishi katika kisiwa hicho waliokuwa na asili ya Kenya.

“Makaburi haya inasadikika kuwa yalitumiwa na watu wa Malindi kutoka Kenya na katika miaka ya karibuni walikuja kudai fidia na serikali iliwalipa,” anasema.

Pia kuna majengo yaliyokuwa yakitumiwa na wakoloni kama ofisi za utawala, kumbi za mikutano na gereza lililojengwa na Wareno mwaka 1505 ambao waliongozwa na Fransisco De Almeida.

Anasema eneo hilo liliingizwa katika urithi wa dunia Oktoba 30 mwaka 1981 na kwamba tangu wakati huo mji umendelea kupata umaarufu hadi sasa.

“Kilwa ndio eneo la kwanza kabla ya Zanzibar na katika Afrika Mashariki kuingizwa katika urithi wa dunia. Tangu mwaka jana tumeanza kufanya matamasha ili kukumbuka siku hii,” anasema Bugumba.

 

MJI ULIKUWAPO KUANZIA KARNE YA NANE

Katika eneo hilo pia kuna sehemu ambazo kila panapochimbwa huonekana mawe yaliyojengwa jambo linaloonyesha kwamba kuna miji mingine imefukiwa chini.

“Ushahidi unaonyesha kuwa kuna majengo mengine ambayo yamefukiwa kwa sababu kadiri unavyofukua unakuta mawe yaliyojengwa.

“Kuna kanuni mbalimbali za kitafiti tunazotumia kama vyungu ambavyo vinatusaidia kuona aina ya michoro, hivyo tutaweza kubaini awamu tofauti za watawala mbalimbali kwa sababu walikuwa na aina za vyombo walivyovitumia.

“Katika karne ya 11 vyombo vya udongo vya kichina vilivyotumika ni vile vya familia za kitajiri na kuna staili mbalimbali za ujenzi zinazotusaaida kupata taarifa sahihi,” anasema Bugumba.

Anasema ukuaji wa mji huo unahusishwa zaidi na Washirazi katika miaka ya 1200 ambao walijigamba kwamba ndio walinunua eneo hilo kutokana na migogoro iliyokuwapo Ushirazi.

“Mtoto wa Sultani, Ali Hassan ndio aliyekuja hapa na kununua eneo hili lote kwa kitambaa kilichoweza kuzunguka kisiwa kizima mwaka 1200.

“Kukua kwa Kilwa kulitokana na mazingira yake ya utulivu, utawala wa kibiashara kuanzia Sofara hadi katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Pwani ambapo miji hiyo ilikuwa chini ya dola ya Kilwa,” anasema.

Anasema Kilwa ilikuwa ni dola iliyokuwa na sarafu yake (sarafu ya Kilwa) iliyonakishiwa kwa fedha na baadaye mwaka 1310 fedha zao zilinakishiwa kwa dhahabu iliyopatikana Zimbabwe.

“Tafiti za kiikolojia za mwaka 1970 zilithibitisha kuwapo kwa uhusiano wa kibiashara baina ya Kilwa na Zimbabwe, kwa sababu ilipatikana sarafu ya Kilwa iliyokuwa ikitumika karne ya 14,” anasema.

Anasema kati ya karne ya 16 hadi 18 Kilwa ilianza kunyanyuka tena wakati wa Biashara ya Utumwa ambapo palikuwa na Sultani Ibrahim ambaye aliingia mkataba na mfaransa kwa ajili ya kukusanya watumwa 1,000 kila mwaka waliokuwa wakipelekwa kwenye mashamba ya miwa maeneo ya Mauritius, Ushelisheli na Mauritania.

 

CHANGAMOTO

Mji wote ulikuwa umezungushiwa ukuta lakini kwa sababu ya mmomonyoko kuta zingine zimelika na wakati kinaanza kuwa kijiji baadhi ya watu walitumia kuta za kale kujengea.

“Baadhi ya wananchi wa maeneo haya wamekuwa wakifukua na kuchukua mawe kwa ajili ya kujengea, hii pia ni changamoto,” anasema.

Anasema hata mlango uliokuwa kwenye gereza lililojengwa na Wareno walilazimika kuuondoa mwaka 2011 na kuweka mpya baada ya wananchi kukata baadhi ya sehemu.

“Sisi ni waswahili na tuna tamaduni zetu kwahiyo kuna baadhi ya watu walikuwa wanakata vipande vya mlango kwa imani kwamba watapata ajira ama kufanikiwa katika baadhi ya mambo waliyoyataka,” anasema.

Kuhusu biashara ya utalii, anasema; “Ni bahati mbaya kwamba miundombinu si mizuri sana hivyo biashara ya utalii si kubwa.

Kwa mujibu wa Bugumba, watalii wa ndani wakitembelea kisiwa hicho hulipa Sh 3,000 wakati wageni hulipa Sh 27,000 na wanafunzi wageni wenye umri chini ya miaka 18 hulipa Sh 13,000.

 

KUFA KWA KILWA

Kulikuwa na sababu kadhaa zilizosababisha kufa kwa mji huo.

“Baada ya kufariki kwa Hassan Ibin Suleman, aliyefuata Sultan Daudi hakuwa mtawala mzuri, alisababisha maasi mengi na kwa kuwa walikuwa na utajiri mkubwa wakaanza kugombana.

“Mwaka 1698 walianza kuingia Wazimba (wala watu) ambao walivamia kisiwa hiki na kufanya mauaji makubwa.

“Mwingereza Richard Burton aliingia kisiwani hapa miaka ya 1800 na kukuta kikiwa kimekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu ulioua watu wengi,” anasema.

Anasema pia baada ya kukua kwa biashara ya utumwa kulisababisha watu wengi kuhamia Kilwa Kivinje kuanzia miaka ya 1700 – 1800.

“Miaka ya 1900 walipokuja Wajerumani walifanya makao makuu yao Kivinje hivyo mambo yote ya msingi yalifanyika huko.

“Mwaka 1940 Waingereza walihamishia makao makuu ya wilaya na kuleta Masoko na kwa misingi hiyo Kilwa Kisiwani ikabaki kijiji kama ilivyo sasa,” anasema Bugumba.

 

MIKAKATI YA HALMASHAURI

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilwa, Zablon Bugingo, anasema wataendelea kuimarisha majengo yaliyoko katika mji huo ili urithi wa dunia usipotee.

“Tutaendelea kusimamia mji na mandhari ya Kisiwa cha Kilwa Kisiwani kuhakikisha kuwa eneo la urithi wa dunia linahifadhiwa ipasavyo,” anasema Bugingo.

Endapo miundombinu ya mji huo itaboreshwa upo uwezekano wa uchumi wa Mkoa wa Lindi kukua zaidi kupitia vivutio vilivyopo katika mji huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles